Zahanati ya Kijiji cha Dareda Kati inayotoa pia huduma ya uzazi haina choo wala bafu hali ambayo inawafanya wagonjwa wakiwemo wajawazito na wauguzi kuwa katika wakati mgumu wa kutoa na kupata huduma za maabara, choo na bafu.
Habari ambazo NIPASHE imezipata zinasema wajawazito wanaolazimika kujifungua katika zahanati hiyo hupata shida ya kujisitiri.
“Wapo wanaokwenda kupata huduma ya choo na bafu kwenye nyumba za watu binafsi na wengine huenda baa za jirani,” alisema mfanyakazi mmoja.
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Karimu Help Fund la California nchini Marekani, kupitia kwa mkurugenzi wake mkazi, Joas Kahembe, limejitolewa kujenga choo na bafu kwa thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 10.
Ujenzi wa shimo la majitaka kwa ajili ya choo na bafu tayari umeanza, na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Msaada huo ni wa pili kutolewa na shirika hilo, ambapo miaka mitatu iliyopita Wamarekani hao walitoa dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali.
Kahembe, alisema pia shirika hilo huwapatia fedha akina mama wajawazito wanaoishi kwa matumaini ili wanunulie chakula cha lishe pamoja na kutoa huduma kwa watoto wenye utindio wa ubongo.
Muuguzi Mkuu wa Zahanati hiyo, Rose Mary Baha alisema, “kazi ya maabara imesimama kwa sasa kwa sababu hakuna choo…wagonjwa wanapata shida sana kwa wakati huu, wanatumia choo cha baa za jirani.”
Kwa upande wake, mtaalam wa maabara, Jaina Msuya, alisema, wanashindwa kuitumia maabara hiyo kwa sababu haina sehemu ya kumwaga uchafu wanaouchunguza.
Pamoja na matatizo hayo, zahanati hiyo haina daktari kwa sasa baada ya aliyekuwepo kwenda masomoni.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment