ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 18, 2012

Hoseah alia na sheria mbovu kesi za ufisadi


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah
Boniface Meena  
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah amelia na Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 akieleza kuwa ni mbovu kwa kuwa inambana na kumfanya ashindwe kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa kubwa mahakamani. Alisema sheria hiyo inamruhusu kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wadogo wa rushwa na wale wakubwa inamtaka apeleke kwanza jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), jambo ambalo linafanya aonekane hafanyi kazi yake ipasavyo.

 Dk Hoseah alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kufafanua kauli yake aliyoitoa katika Kipindi cha Baragumu kilichorushwa na Televisheni ya Channel Ten. Alisema anajua matarajio ya wananchi ni makubwa kwa Takukuru, lakini akasema sheria hiyo imewafunga mikono kwa kuwa hawawezi kuchukua uamuzi dhidi ya kesi kubwa za ufisadi bila ushauri wa DPP. 

“Sina mamlaka ya kumpeleka mtuhumiwa wa rushwa kubwa mahakamani. Uwezo wangu ni kupeleka wala rushwa ndogondogo tu na kwamba kazi yangu ni kuchunguza tu,” alisema Dk Hoseah na kuongeza: “Sheria yetu imetufunga mikono kwa kuwa kumpeleka mtu mahakamani siyo uamuzi wangu, bali wa DPP.”

 Alisema Kifungu cha 37 cha Sheria ya Takukuru hakimruhusu kutaja majina ya watuhumiwa wa rushwa na kwamba sheria hiyo katika Kifungu cha 57 inamzuia kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wakubwa wa rushwa, mpaka awafikishe kwa DPP.

 Kifungu hicho cha 57 (1) kinasema kuwa shtaka lolote la kosa lililoelezwa kwenye Sheria ya Takukuru lazima lifunguliwe kwa ruhusa ya maandishi kutoka kwa DPP. Kifungu cha 57 (2) kinamtaka DPP ndani ya siku 60 kutoa au kukataa ruhusa ya kushtakiwa. Dk Hoseah alisema hiyo ni moja ya changamoto zinazoikabili taasisi yake na kwamba wananchi wasubiri mabadiliko ya kiutendaji kama sheria itabadilika na kumruhusu kufanya hivyo. “Tusaidieni sheria hii ibadilishwe ili iweze kuturuhusu kufanikisha kupambana na rushwa nchini,” alisema Dk Hoseah. Jitihada za kumpata DPP Eliezer Feleshi, ziligonga mwamba baada ya kumtafuta muda mwingi kwa simu bila kupatikana. 

Hata hivyo, baadaye alipiga simu na kusema: “Niko kikaoni ila nimetoka mara moja. Siwezi kusema chochote leo na nahisi kesho (leo) sitakuwa Dar es Salaam.”  Takukuru na mabilioni Uswisi 
Kuhusu fedha zinazodaiwa kufichwa na vigogo nchini Uswisi, Dk Hoseah alisema Takukuru inafuatilia kwa karibu suala hilo kujua ukweli wake. 

Juzi, akiwasilisha maoni ya upinzani, Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Fedha, Zitto  Kabwe alisema anawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja kwa majina ikiwa Serikali haitawataja. Zitto aliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na wafanyabiashara wakubwa walioficha Sh315.5 bilioni Uswisi akisema wanafahamika. 

Jana, Dk Hoseah alisema ofisi yake inazo taarifa kuna mabilioni ya fedha yamefichwa Uswisi na kwamba taasisi yake inayafuatilia. Alisema Takukuru imewasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG),  ili awasiliane na Uswisi kujua ni kiasi gani cha fedha kimehifadhiwa nchini humo na hatua zichukuliwe. “Takukuru imewasiliana na AG ili awasiliane na Uswisi kujua wana kiasi gani huko, kina nani wenye fedha hizo na zimepelekwa huko lini,” alisema Dk Hoseah. 

Dk Hoseah alisema hivi sasa wanasubiri Uswisi imjibu AG kuhusu maombi yao na baada ya majibu hayo ataikabidhi Takukuru kwa ajili ya hatua zaidi. Juni mwaka huu, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa inayoonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara. 

Akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha juzi, Zitto alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa Serikali za Awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo. “Kambi ya Upinzani bungeni imepata taarifa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni mwa wenye fedha hizi,” alisema Zitto. Aliitaka Serikali kuliambia Taifa ni hatua gani itakazochukua kurejesha fedha hizo na pia kuwataja wamiliki wake na kama ikishindwa, kambi ya upinzani itawataja. 

“Tunaitaka Serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa,” alisema Zitto na kuongeza: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha hizo iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi.”

Fedha hizo zinadaiwa kutokana na biashara zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye sekta za nishati na madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Mwananchi

No comments: