Sunday, August 19, 2012

JK:Hatuna mpango kupigana na Malawi

Rais  Jakaya Kikwete,  amesema Tanzania haina nia wala mpango wa kuingia katika vita na  Malawi, kufuatia tofauti zao kuhusu mpaka  wa  Ziwa Nyasa.
Rais  alitoa maelezo hayo baada ya mazungumzo kati yake na Rais wa Malawi Joyce Banda, yaliyofanyika Maputo Msumbiji.
"Namhakikishia dada yangu na watu wote wa Malawi kwamba hatuna nia wala mpango we kuingia vitani, hatuna matayarisho ya jeshi wala jeshi halijasogea popote kwani hakuna sababu" alisema.


Aliongeza kwa msisitiza zaidi kuwa  "Mimi ndiye Kamanda Mkuu wa Majeshi na sijapanga wala kutoa maelekezo ya vita".
Rais alisema hayo, mbele ya Rais Banda na kuongeza kuwa kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu kuhusu suala la mpaka na tayari maafisa wa pande zote mbili wameanza kulizungumzia kwa nia ya kulitatua  kwa amani.

"Tuviachie vyombo vyetu vifanye kazi, hebu tuvipe nafasi, wanasiasa na waandishi wa habari wajiepushe na maneno haya yanayosababisha taharuki na chokochoko, hayana maana waiachie diplomasia ifanye kazi yake" Rais alisisitiza.

Naye Rais Banda alisema amefurahishwa na kufarijika baada ya kuhakikishiwa kuwa hakuna vita na Rais Kikwete.

"Nimefarijika sana, suala hili limetusumbua sana, mpaka  Wamalawi wotewakaungana na kuwa kitu kimoja na kuzuia tofauti zao" alisema nakuvishukuru vyombo vya habari vya Malawi kwa kuonyesha uzalendo na  ukomavu katika suala hili.

Rais Kikwete yuko Maputo, Msumbiji kuhudhuria kikao cha viongozi waJumuiya ya Maendeleo Kusini Kwa Afrika (SADC) ulioanza Ijumaa na ambao ulitarajiwa kumalizika jana jioni, ambapo Rais Kikwete anatarajia kurejea nyumbani mara baada ya kikao hiki.

Katika mkutano huo  Tanzania ilichukua uenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Afrika ya Kusini ambapo uenyekiti wa SADC umekwenda kwa  Msumbiji  baada ya Angola kumaliza muda wake. Nafasi hizi za uongozi  hushikiliwa kwa  mwaka mmoja kwa  zamu miongoni mwa nchi wanachama.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: