Elias Msuya
MAOFISA wa Tume ya Uchaguzi wa Malawi (Mec), wameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kujifunza baadhi ya mambo yanayoweza kuifanya kuwa huru, kuliko ilivyo sasa.Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na maOfisa hao waliokuwa wameitembelea Nec, ili kubadilishana uzoefu kati ya tume hizo mbili.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kutoa maelezo ya Mec, Kamishna Gloria Chingota, alisema jambo ambalo Nec inaweza kujifunza kutoka katika tume yake ni jinsi ya kupata viongozi wa tume na hasa makamishina, tofauti ilivyo sasa wanapoteuliwa na Rais.
“Jambo ambalo Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanaweza kujifunza kutoka kwetu ni jinsi ya kuwapata makamishna wa tume. Kule kwetu vyama vya siasa hupendekeza majina kisha Rais huyapitisha. Ni mwenyekiti tu ndiyo anayeteuliwa na Rais, lakini wengine hupendekezwa na vyama na siyo lazima wawe wanasheria, wapo hata viongozi wa dini,” alisema Chingota.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Malawi iko huru kiasi cha kutosha kuendesha chaguzi zilizo huru na za haki.
Chingota alisema Malawi, inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwaka 2014 na kwamba kuna makamishna 10 walioteuliwa mwaka huu ambao sasa wameamua kuja kujifunza baadhi ya mambo kutoka katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Tunatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwaka 2014 na kuna uwezekano wa Mec kuchanganya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa pamoja na uchaguzi huo miaka miwili ijayo,” alisema Chingota.
Alitaja mambo wanayotarajia kujifunza kutoka Nec kuwa ni pamoja na vyanzo vya mapato vya tume, upatikanaji wa viongozi, usajili wa wapiga kura, upigaji kura, uhusiano na wadau, elimu ya mpiga kura na utunzaji wa rasilimali za tume.
Mapema, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, alikiri kuwapo kwa malalamiko hasa kuhusu viongozi wa tume hiyo kuteuliwa na Rais ambaye pia Mwenyekiti wa chama tawala kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kuwa makamishna wa Tume huteuliwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala, kumekuwa na malalamiko mengi ya kutokuridhishwa hasa kwa vyama vya siasa na wanaharakati wa kiraia kuwa tume hii siyo huru,” alisema Jaji Lubuva.
Licha ya kukiri upungufu huo, Jaji Lubuva alisema utaratibu huo utaendelea hadi hapo katiba itakapobadilishwa katika mchakato wa katiba mpya unaoendelea.“Hatukatai mabadiliko, kama wananchi hawaridhishwi, watoe maoni kwenye mchakato wa katiba ili ibadilishwe,” alisema.
Alisisitiza kuwa utaratibu uliopo, unafuata katiba na kwamba tume hiyo inafanya kazi yake kwa uhuru.
“Kama nilivyosema awali kwamba, uhuru wa tume katika utendaji kazi wake unalindwa na ibara ya 74(7) na 11 ya katiba. Hadi sasa tume haijapata maelekezo au maagizo kutoka serikalini au kwa mtu yeyote. Inafanya kazi kwa uhuru,” alisema Jaji Lubuva.
Kuhusu uhuru wa tume hiyo kifedha, Jaji Lubuva alisema licha ya fedha zake kutolewa na Serikali, bado uhuru wake uko palepale
“Ni kweli kwamba fedha za kuendeshea Nec hutoka kwenye mfuko wa pamoja wa Serikali na kwa masuala ya bajeti hupitia kwenye ofisi ya Waziri Mkuu. Hata hivyo uhuru wa tume katika kutekeleza majukumu yake unabaki palepale,” alisema.
Alitaja changamoto nyingine zinazoikabili tume hiyo kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, usimamizi wa uchaguzi, usajili wa wapiga kura, elimu ya wapifa kura, upitiaji upya wa daftari la kudumu la wapiga kura, miundombinu, mawasiliano na teknolojia hafifu na watu wachache kujitokeza katika uchaguzi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment