ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 20, 2012

Nyumba za wadaiwa sugu Tanesco kupigwa mnada


Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud
Boniface Meena 
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kuwa linaandaa utaratibu wa kupiga mnada nyumba za watu na kampuni kubwa binafsi ambazo wamiliki wake ni wadaiwa sugu wa shirika hilo. 

Shirika hilo sasa limetoa wiki mbili kwa wadaiwa hao kulipa malimbikizo ya madeni yao kabla hatua ya kufidia madeni hayo kwa kuuzwa nyumba, haijaanza kutekelezwa. 
Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, utaratibu huo mpya wa kufidia madeni ya Tanesco utaanza baada ya kipindi hicho cha wiki mbili kumalizika. 

"Tutapiga nyumba hizo mnada kwa kutumia Sheria ya Mwenendo wa Madai, Sura ya 33 ya Sheria za Tanzania, Amri ya 35 Kanuni ya 1(d) inayoipa mamlaka Tanesco kupiga mnada nyumba za wadaiwa ili kufidia deni ambalo shirika linamdai mteja wake," alisema Badra na kuongeza:

 “Baada ya mwezi huu (Agosti) kwisha, tunasisitiza kwamba utaratibu utabadilika kabisa na kwamba wale wote wanaodaiwa na Tanesco na hawajalipa kwa kipindi cha wiki mbili tangu sasa nyumba zao zitapigwa mnada,” alisema Badra. 
“Hakuna meneja anayekaa ofisini kwa sasa na hakuna nyumba yenye nyaya za umeme za Tanesco ambayo haitakaguliwa kwa maana kwamba ni zoezi la nyumba hadi nyumba,” alisema Masoud. 

Alisema shirika hilo limeanza mikakati ya kupambana na wezi wa umeme tofauti na wateja wao walivyokuwa wamezoea. 

Masoud alisema katika mikakati hiyo mtu yeyote atakayegundulika kuchezea mita au amejiunganishia mita kwa njia  isiyo halali au kuwatumia vishoka atafikishwa katika vyombo vya sheria ikiwamo polisi na hatimaye mahakamani.

 “Kampeni hii dhidi ya watu wanaoihujumu Tanesco itakuwa ya uwazi kwa kuwa tutakuwa tunashirikiana na vyombo vya habari, dola kwa sababu nia yetu ni kukomesha vitendo vyote viovu dhidi ya Tanesco vinavyorudisha nyuma maendeleo ya shirika na kukosesha mapato Taifa letu,” alisema Masoud. 

Alisema Tanesco imetoa wiki mbili kwa wateja wote sugu kulipa madeni yao na pia wale wateja wenye wasiwasi na matatizo ya mita zao wajisalimishe katika shirika hilo mapema. 

Masoud alisema uongozi wa shirika hilo umetoa tahadhari kwamba ifikapo mwisho wa mwezi huu wale wote ambao wanaiba umeme kwa njia yoyote ile wajisalimishe wenyewe mapema kabla muda uliotolewa haujamalizika. 

“Watakaojisalimisha wenyewe kwenye ofisi zetu hawatatangazwa kwenye vyombo vya habari na wala hawatapelekwa mahakamani bali watapigiwa hesabu kwa ajili ya kulipia gharama za umeme walioutumia na mita zao kuingizwa kwenye mfumo halisi wa Tanesco,” alisema Masoud. 
Alisema zoezi hilo litahusisha pia watumiaji wa umeme wote ambao wananunua umeme kwenye mifumo isiyotambulika na shirika hilo. 

“Tunaomba wateja wetu kuhakiki risiti zao na kujiridhisha kuwa umeme wanaotumia ni halali,”alisema. 

Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

SHAME ON YOU TANESCO YAANI MNAUZA NYUMBA TO PAY FOR ELECTRICAL BILL???HUU NI UONEVU WATANZANIA MSIKUBALI KABISA AWA MAFGISADI WANATAKA KUCHUKUA HATA KILE KIDOGO MLICHONACHO.KAMA HILI NDILO WAZO LA MKURUGENZI WA TANESCO AU AMEAFIKIANA NA WAZO HILI BASI INAONYESHA NI JINSI GANI ALIVYO NA UFINYU WA FIKIRA ,WAZIRI WA NISHATI NA MADINI NAOMBA HUYU KIONGOZI AWAJIBISHWE