Nina imani msomaji wangu una hamu ya kujua leo nimekuja na mada ipi. Nimekuja na mada inayohusu ahadi zisizotimia, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya sikukuu.
Wapo watu huwaahidi wapenzi wao kuwanunulia vitu kabla ya sikukuu, lakini kwa bahati mbaya mambo huenda ndivyo sivyo.
Mambo yaliwahi kumuendea vibaya rafiki yangu mmoja ambaye alitoa ahadi kwa mpenzi wake lakini hakuweza kuitimiza mpaka sikukuu ikafika, hali iliyoleta mgogoro ndani ya nyumba.
Pia, jamaa yangu mmoja alikwenda kwake na wageni kula sikukuu, kilichomkuta ni aibu, mkewe hakugusa jiko, ilibidi jamaa awapeleke hotelini, kisa ni kutotimiza ahadi aliyomuahidi bebi wake huyo.
Mgomo wa mkewe haukuishia kwenye kupika tu, hata haki yake ya ndoa alinyimwa, kila alipomgusa usiku aliambulia matusi, ilifikia hatua mkewe akawa analala na nguo.
Swali linakuja, ni ahadi hiyo hiyo au kuna kitu kingine?
Ni kweli ahadi au zawadi kwa mpenzi wako ndizo zinazolinda penzi lenu?
Japokuwa ahadi ni deni, lazima tujue kuna kupata na kukosa na mapenzi ya kweli hayalindwi na kitu bali ninyi wenyewe, zawadi ni matokeo na inapokosekana, isipunguze mapenzi.
Inapofikia hatua ya kumnyima haki yake ya ndoa eti kwa sababu hajatekeleza alichoahidi, hapo utakuwa umevuka mipaka ya mapenzi, utajionyesha unampa haki yake kwa gharama.
Siku zote inapotokea hitilafu ndani ya ndoa, iwe siri yenu, hata wageni wakija wasijue mpo kwenye hali gani, ni kweli umekasirika kukosa kitu ulichokisubiri kwa hamu kubwa, lakini ndiyo hivyo hakikupatikana. Japo umeudhika, hilo usiliingize kwenye mapenzi.
Unapoombwa haki ya ndoa, itoe tena kwa nguvu zote kuonyesha unampenda mpenzio, si kwa kitu bali yeye mwenyewe na umalizapo kumtoa kijasho chembamba, una nafasi ya kumueleza; “Mpenzi umeniudhi sana.”
Naye ataeleza sababu zilizomfanya asitimize ahadi yake. Ili kuongeza mapenzi, unapaswa kujionyesha unamjali mpenzio katika hali yoyote, hata anapokuudhi, usiku ukiingia akikugusa usiweke kisasi cha kumjibu maneno ya kifedhuli: “Ooh unikome.” au “Achana na mimi.”
Unapoitwa na mpenzio, itikia wito, mwenzio ameshikika, mpe haki yake ili kuongeza mapenzi na kujionyesha unampenda yeye mwenyewe alivyo, wala siyo kitu.
Mwisho, nimalizie kwa kusema penzi la kweli halilindwi na uzuri wa mtu wala fedha.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment