ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, September 25, 2012
Hakimu kizimbani kwa rushwa
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Bi. Pamela Kalala akiwa na ndugu yake wakati akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, mara baada kupata dhamana baada ya kutajwa kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 3 na kupokea sh. 900,000. (Picha na Heri Shaaban)
Na Rehema Mohamed
HAKIMU wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Bi. Pamela Kalala, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matatu ya kuomba na kupokea rushwa.
Hakimu Kalala ambaye amefunguliwa kesi namba 223 ya 2012, anadaiwa kuomba rushwa ya sh. milioni 3 na kupokea sh. 900,000 ambapo kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Aloyce Katemana.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa alisomewa mashtaka na wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Alen Kasamala.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, katika terehe tofauti Februari mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa aliomba rushwa ya sh. milioni 3 kutoka kwa Bi. Josephine Wage, ambaye ni mke wa mmoja wa washtakiwa wa kesi ya jinai namba 703 ya mwaka 2008.
Kesi hiyo ni ya jamhuri dhidi ya Abubakari Mzirahi na wenzake ambapo mshtakiwa aliomba fedha hizo ili iwe kishawishi cha kutoa upendeleo kwa mume wa Bi. Wage, wakati wa kutoa uamuzi.
Kosa la pili ilidaiwa kuwa, katika tarehe zisizofahamika, Februari mwaka huu, mshtakiwa akiwa kama Hakimu Mkazi na wakala wa kuzuia na kupambana na rushwa, kinyume na kifungu namba 11/2007 cha sheria ya TAKUKURU alipokea rushwa ya sh. 800,000 kutoka kwa Bi. Wage.
Kosa la tatu, ilidaiwa Februari 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alipokea rushwa sh.100,000 kutoka kwa Bi. Wage ili iwe kishawishi cha kutoa upendeleo kwa mumewe wakati wa kutoa uwamuzi katika kesi inayomkabili.
Mshtakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Hata hivyo, mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya sh. milioni moja, pamoja na mshtakiwa kusaini bondi ya kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 23 mwaka huu kwa ajili ya kuitwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment