Mshiriki wa Maisha Plus, Swaumu Shabani (katikati) akifanyiwa usaili kwa ajili ya mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Oktoba 13 mwaka huu. Kulia ni Mratibu wa Maisha Plus Ally Masoud 'Kipanya' na kushoto ni mshindi wa mashindano hayo wa mwaka 2009, Abdulhafidh Haleem (Picha na Victor Mkumbo)
Na Victor MkumboVIJANA 400, jana wamejitokeza katika usaili wa mashindano ya Maisha Plus 2012 katika Ukumbi wa Millenium Tower, Dar es Salaam.
Katika mashindano ya mwaka huu kutakuwa na utofauti mkubwa na yaliyopita kutokana na kuboreshwa kwa kuingiza shindano jipya la Mama Shujaa wa Chakula.
Akizungumza katika usaili huo jana, Mratibu wa mashindano hayo Ally Masoud 'Kipanya', alisema shindano la Mama Shujaa wa Chakula linatarajiwa kuanza Oktoba 2 hadi Oktoba 16, mwaka huu huku mshindi na washiriki wa Maisha Plus wataingia katika kijiji hicho ambacho kipo nje ya mji Oktoba 13, ili kukaa kwa siku tatu..
Alisema mshindi katika mashindano ya Mama Shujaa wa Chakula ataondoka na zana za kilimo pamoja na fedha, ambazo kiwango chake kitatajwa hivi karibuni.
Kipanya alisema usaili umeshafanyika katika mikoa 17 ambapo jana, walimalizia Dar es Salaam na washiriki 400 walijitokeza ambapo mshindi kwa mwaka huu ataondoka na sh. milioni 20.
Mratibu huyo aliitaja mikoa ambayo wameshafanya usaili kuwa ni Tanga, Kilimanjaro, Bukoba, Iringa, Mbeya, Singida, Dodoma, Mwanza Shinyanga, Katavi na Morogoro.
"Tunatarajia mashindano ya mwaka huu yatakuwa tofauti kutokana na kuyaboresha zaidi, ambapo tutaanza na mashindano ya Mama Shujaa wa Chakula na baadaye vijana wa Maisha Plus wataingia kijijini," alisema.
Alisema katika usaili huo wamechukua vijana wenye vigezo mbalimbali, ikiwa ni kujiamini na uwezo wa kuishi sehemu yoyote.
Majira
No comments:
Post a Comment