ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 24, 2012

Wagombea CCM wapumulia mashine

Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Abdulrahaman Kinana

  Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
  *Ni waliotishia wakienguliwa, patachimbika
  *Kinana ajiengua kuwania ujumbe wa Nec

Wagombea wa nafasi mbalimbali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kama wanapumulia mashine kutokana na idadi kubwa kujitokeza kuwania nafasi moja ikilinganishwa na nafasi halisi.

Kwa siku ya tatu mfululizo, Kamati ya Maadili ya CCM imeendelea kupitia majina ya wagombea mjini Dodoma huku ikieleza kuwa kazi hiyo imekuwa kubwa kutokana na wagombea kuwa wengi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ameonya kwamba wagombea wanaolumbana nje  badala ya kwenye vikao halali vya ndani vya chama hicho , wakitishia  patachimbika iwapo Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho itawaengua, wanaonyesha jinsi walivyo na uwezo mdogo wa kuongoza. 



Walioingia katika malumbano ya kisiasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja; Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa:

“Unapotaka kuwa kiongozi wa taasisi kubwa moja ya sifa ni uwezo wako wa kuhimili presha, ukiona mtu anapiga kelele barabarani ujue uwezo wake wa kuhimili presha ni mdogo, presha imekuwa kubwa kiasi kwamba hawezi kuhimili inabidi aende kupumua barabarani.”alisema.

Aliongeza kuwa: “Busara itatumika kuamua nani arudi nani asirudi…siasa za leo ni za presha hasa inapofika wakati wa uchaguzi na inapofika siasa za  jumuiya. Sasa kama unataka kuiongoza taasisi kubwa kama hiyo lazima uwe na kifua cha kuhimili presha.”

Kuhusu malumbano ya hivi karibuni kati ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Nape alisema kuwa: “Hawa wote ni wajumbe wa vikao halali wanasema barabarani sijui labda wamelewa, hawa ni viongozi kama mtu ana agenda yake aje kwenye vikao.”

Nape aliongeza kuwa “Kwa hili nalo wasubiri vikao vitakapofanya maamuzi, wakiona wana maoni hai wanayofursa ya kuja kusema katika vikao, kwa sababu hatutafanyia kazi maoni barabarani."

Kuhusu mgogoro wa kada wa chama hicho, Hussein Bashe na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kingwallah, alisema hilo linashughulikiwa na Kamati ya Maadili ya Chama hicho.

Alisema kama watabainika kuwa na makosa basi kikao hicho kitatoa adhabu ambayo si lazima itangazwe hadharani.

Akizungumzia kuhusiana na kuchelewa kuanza kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, Nape alisema idadi kubwa ya waliojitokeza kugombea inaonyesha kukubalika kwa chama mbele ya wananchi.

“Vikao vya chini vinachokifanya ni kuweka alama tu kuanzia A hadi E ambayo inaonyesha kuwa haufai kabisa…Tafsiri kwamba vikao vya chini havikufanya kazi yake vizuri si kweli, vikao vya chini vilifanya kazi nzuri sana,”alisema Nape.

Alisema kuna watu ambao watakuwa wametoa malalamiko ni lazima vikao hivyo viangalie kwa kigezo cha mahitaji ya wakati huo yakoje.

Aidha imebainisha kuwa mchujo wa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM inaweza kuchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kutokana na idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hizo.

Alisema Kamati ya Maadili ya chama hicho ilitakiwa kufanya kikao kimoja kwa ajili ya kupitia na kutoa mapendekezo ya wagombea lakini kutokana na wingi wao kamati hiyo imelazimika kuchukua siku tatu kufanya kazi hiyo.

“Hata hivyo kazi kubwa ni hii inayofanywa na Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) watakuwa na kazi ndogo kwa kuwa watakuwa wanayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kamati hii ya maadili,” alisema Nnauye.

Alitaka idadi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hizo mbalimbali ndani ya chama hicho kuwa ni wenyeviti wa mikoa ambako kuna nafasi 31, lakini waliojitokeza kuwania nafasi hizo ni 187 na Katibu Siasa na Uenezi Mkoa nafasi 21 walioomba ni 170.

Wengine ni Makatibu wa Uchumi/Fedha mkoa nafasi 31 walioomba 148, wenyeviti wa wilaya nafasi 161 walioomba 965 na wajumbe wa NEC taifa nafasi 221 walioomba 1,380.

Katika nafasi za wenyeviti wa jumuiya za taifa, kwa upande wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) nafasi ni moja walioomba 47 wote kutoka Zanzibar, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) nafasi moja walioomba tisa na Jumuiya ya Wazazi nafasi moja walioomba ni 22.

Kwa upande wa makamu wenyeviti wa jumuiya ndani ya chama hicho, UVCCM nafasi ni moja walioomba ni 27 wote kutoka Tanzania Bara, UWT nafasi moja walioomba watatu na Wazazi nafasi moja walioomba ni 10.

Aidha katika nafasi za wenyeviti wa jumuiya wa mikoa zipo 93 walioomba ni 502 na kwa wajumbe wa Nec nafasi za jumuiya zipo nafasi 30 walioomba ni 279.

“Kazi ni kubwa kinachofanyika ni Kamati hii ya Maadili kupitia jina moja moja la kila mgombea,” alisema Nape.

Alipoulizwa kuwa haoni idadi kubwa ya wagombea iliyojitokeza inaweza kuleta makundi, Nape alijibu kuwa chama hicho kinauzoefu wa miaka 50 kuhusiana na watu wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Mkono aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kama jina lake halitarejeshwa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa, patachimbika.

Mkono alitoa kauli hiyo wiki iliyopita baada ya kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa jina lake limeenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.

Hii itakuwa ni mara ya pili iwapo Mkono ataenguliwa. Katika kikao cha NEC mwaka 2007, chini ya Rais Jakaya Kikwete alienguliwa kwa sababu ambazo hadi leo hazijaelezwa.
Kwa upande wake Lembeli, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hatakubali kuenguliwa  kwa sababu ya misimamo yake hasa ile anayoonyesha bungeni.

Wakati huo huo; nyumba nyingi za wageni mjini hapa zimejaa wapambe wa wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika baadhi ya nyumba za wageni zilizoko katikati ya jiji zimebaini kuwa wapambe wengi wameomba kupatiwa nafasi katika nyumba hizo.

“Zimejaa, kuna waliofika jana (juzi) na leo (jana), wapo wanaokuja na tayari wameshalipia vyumba…hatujui watatoka lini,”alisema mmoja wa wahudumu wa nyumba hizo zilizopo katika mji wa Dodoma.

Pia mabasi ya abiria kutoka jijini Dar es Salaam kuja mjini hapa, karibu yote yalikuwa yamejaa abiria kuanza juzi kwa madai kuwa yamekodishwa na wanachama wa chama hicho.

Hata hivyo, habari zilidai wapambe hao ambao hawako katika vikao vya maamuzi wapo kwa ajili ya kusaidia kuwashawishi wajumbe wa Nec waweze kupitisha majina ya wagombea wao.

Naye Mwanasiasa mkongwe nchini, Abraham Kinana, hatagombea tena ujumbe wa chombo hicho cha juu cha maamuzi.

Kwa mujibu wa Kinana hatowania tena nafasi hiyo kwa sababu miaka 25 aliyoshikilia nafasi hiyo inatosha.

Alisema ni anaamini kitendo cha kung’atuka kwake ni kizuri na kitatoa nafasi kwa wana CCM wengine wazuri nao watoe mchango wao kwa chama hicho.

“Sijagombea kwa kuwa miaka 25 ya kushiriki katika vikao vya vya juu inatosha na ni vizuri kung’atuka, naamini kuna wana CCM wengi wenye sifa na uwezo wa kuongoza chama,” alisema.

Kinana ambaye alikuwa mpiga debe wa Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema suala la uongozi ni sawa na mbio za kupokezana vijiti.

Alisema sasa ni wakati wake kukabidhi kijiti alichonacho  kwa wanachama wengine wa chama hicho.

Akizungumza mjini jana Dodoma kuhusiana na uamuzi huo, Nape, alimsifu Kinana kwa uamuzi wake.

Alisema kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo na kushukuru kwa kujitolea katika shughuli za chama ikiwemo vikao vya juu vya maamuzi.

“Tunashukuru kwa uzalendo, ujuzi na uzoefu alionyesha katika kipindi chote alichoshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, hata hivyo, napenda nisisitize kutokana na sifa alizonazo bado chama chetu kinamhitaji,” alisema.

Alisema pamoja na kuamua kuachia ngazi bado Kinana anaendelea kushika nyadhifa nyingine ndani ya chama hicho ikiwemo Uenyekiti wa Bodi ya vyombo vya habari vya CCM vya Uhuru na Mzalendo. 





 
CHANZO: NIPASHE

No comments: