ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 24, 2012

Maalim Seif aigeuka SMZ

Salma Said, Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif amesema kuwa vurugu zilizotokea kwenye uchaguzi mdogo wa Bububu zilisababishwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya SMZ, hivyo kumtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuchukua hatua.

Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema hatakubali kuona Zanzibar ikirejea katika machafuko, hivyo anataka SMZ iwashughulikie watu wote wanaotaka Zanzibar iendelee kumwaga damu kwa uhasama wa kisiasa.


“Mimi nashangaa sana kwa sababu askari ni walewale waliosimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mbona katika uchaguzi ule walikuwa na nidhamu na hawakumbughudhi mtu? Inakuwaje katika uchaguzi huu mdogo walete vurugu na kuwadhalilisha watu?” alihoji Seif.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Viwanja vya Kwa Geji Kijichi, jimbo la Bububu. 

Alikuwa akizungumzia matukio na matokeo ya uchaguzi wa Bububu uliofanyika hivi karibuni.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Hussein Ibrahim Makungu alishinda kwa kura 3,371 sawa na asilimia 50.7, dhidi ya mgombea wa CUF, Issa Khamis Issa aliyepata kura 3,204 sawa na asilimia 48.2

Huu ni mkutano wa kwanza wa hadhara kufanywa na chama hicho katika jimbo hilo tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo Septemba 16, 2012.

“Hakuna chama wala mtu mwenye hati miliki ya nchi hii (Zanzibar). Nchi hii ni ya Wazanzibari wote kabisa,” alisema Maalim Seif.

Seif alieleza kusikitishwa na vurugu alizodai kuwa zilisababishwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya SMZ, akisema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa maadili yao ya kazi na vinaijengea picha mbaya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

CUF inadai kuwa watu wapatao 22 akiwamo Mbunge wa Jimbo Mtoni, Faki Haji Makame wa chama hicho walijeruhiwa na kudhalilishwa wakati wa uchaguzi huo.

Alisema umoja wa Wazanzibari umetafutwa kwa taabu, hivyo akaeleza kushangazwa na baadhi ya watu wanaotaka kuuharibu na kuirejesha nchi katika migogoro.

Maalim Seif aliitaka Serikali kuwa makini na watu hao ili umoja na mshikamano wa Wazanzibari uliokuwapo usiharibiwe tena.

Kauli kuhusu Muungano
“Mimi binafsi ni muumini wa Muungano wa Mkataba,” alisisitiza Maalim Seif akirudia kauli hiyo mara kadhaa huku akishangiliwa na umati wa wafuasi na wapenzi wa CUF.

"Mimi sitafuni maneno wala sioni kama ni vibaya kutetea Muungano wa mkataba kwani naamini ndiyo suluhisho la malalamiko yote ya Zanzibar.

Alisema ana shaka kwamba vurugu zilizotokea katika uchaguzi mdogo wa Bububu zilipangwa ili kuvuruga Umoja wa Kitaifa, lakini wenye nia hiyo hawatafanikiwa kwa kuwa Wazanzibari wengi wameelewa umuhimu wa amani na umoja kwa maendeleo ya nchi yao.

Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema ni wajibu wa vyama vya siasa na viongozi kuelewa kuwa hakuna chama wala mtu mwenye hatimiliki ya nchi, bali wenye mamlaka hiyo ni wananchi wenyewe. 

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismal Jussa Ladhu aliwataka wafuasi wa chama hicho Jimbo la Bububu kuwa wastahimilivu wakati chama kikifuatilia changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo.

Jussa alisema Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na akamtaka ajiuzulu kwa kile alichoeleza kuwa aliingilia uchuguzi huo.

Naye Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma wa CUF, Salim Bimani alisema hawakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo na kwamba waliotangazwa washindi wanaweza kulitema jimbo hilo.

Katika risala yao wapenzi wa CUF Jimbo la Bububu waliishutumu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Vikosi vya Ulinzi na Usalama wakidai kuwa ndiyo waliochochea vurugu hizo.

Akisoma risala kwa niaba yao,  Mgeni Ali Suleiman aliishutumu ZEC kwa kushirikiana na Vikosi vya Ulinzi kuvuga uchaguzi huo uliompa ushindi mgombea wa CCM na kuonya kuwa hawamtambui na hawatampa ushirikiano mwakilishi huyo mteule.

"Iwapo Serikali ya Umoja wa Kitaifa haitakuwa makini kurekebisha kasoro zilizopo, hakuna sababu ya CUF kubakia serikalini kwani kiini cha mgogoro wa kisiasa kinatokana na matokeo ya uchaguzi tangu kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania 1995," ilisema sehemu ya risala hiyo.

No comments: