ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 25, 2012

Yanga yakopa mil.200/ kumlipa Saintfiet



Kuna  taarifa kuwa klabu ya Yanga imejiingiza mtegoni baada ya kukubali kukopa zaidi ya Sh. milioni 200 ili kumlipa kocha Tom Saintfiet waliyemtimua Ijumaa baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa siku 80 tu.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo gazeti hili imezipata jana, zinaeleza kuwa Yanga imejiingiza katika deni hilo baada ya kiongozi mmoja kuamua kuvunja mkataba na kumlipa Saintfiet kiasi hicho kikubwa cha pesa kutoka mfukoni mwake, lakini kwa sharti kwamba klabu hiyo ni lazima imrejeshee fedha hizo.



Chanzo kimedai kwamba hadi mkataba wao wa miaka miwili na Saintfiet ukivunjwa, tayari kocha huyo raia wa Ubelgiji alishaitumikia kwa miezi mitatu na kwamba, Yanga imelazimika kumlipa mishahara yake yote ya miezi 21 iliyobaki.

Imeelezwa zaidi kwamba katika mkataba wake na Yanga, Saintfiet alikuwa akilipwa mshahara wa takriban dola za Marekani 6,500 kwa mwezi, hivyo jumla ya fedha zote alizolipwa kama fidia kutokana na kuvunjwa kwa mkataba huo kabla ya kumalizika kwa miezi 21 iliyobaki, ni dola za Marekani 136,500 (Sh. milioni 212.3).

Chanzo kimedai kuwa hadi anatimuliwa mwishoni mwa wiki, kocha huyo aliyetua Yanga Julai 4 na kupokewa kwa ngoma na matarumbeta wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari alishalipwa mishahara ya miezi mitatu ambayo jumla yake ni dola za Marekani 19,500 (Sh. milioni 30.3)
Taarifa hizo zimedai kuwa hadi sasa, tayari Saintfiet ameshalipwa na kilichobaki ni kwa klabu ya Yanga kumlipa kiongozi (wa klabu hiyo hiyo) aliyetoa fedha zake ili kumalizana na kocha huyo.

"Cha kusikitisha ni kwamba, hata maamuzi haya ya kumtimua kocha yalifanywa na mtu mmoja ambaye ndiye aliyetoa fedha zake na kumlipa Saintfiet. Mtihani uliobaki ni kwa klabu (Yanga) kumlipa huyu kiongozi (jina tunalihifadhi)... maana ameikopesha klabu kwa maamuzi ambayo kwakweli hayakupitishwa na Kamati ya Utendaji ya klabu kama katiba inavyoeleza," kilieleza chanzo hicho.

Gazeti hili liliwasiliana na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga ili kupata uthibitisho wa taarifa kwamba klabu imejiingiza katika deni la mamilioni ya fedha ili kumalizana na Saintfiet. 

Hata hivyo, yeye alishangaa na kusema kwamba hatambui jambo hilo kwani suala lake wameliweka pembeni na jukumu la kumlipa madai yake bado halijafanyanyiwa kazi na Kamati ya Utendaji.

Sanga alisema pia mchakato wa kupata mrithi wa kocha huyo bado haujaanza ingawa wanafahamu tayari wapo makocha watakaokuwa tayari kuifundisha Yanga pale watakapotakiwa kufanya hivyo.

"Mimi sina taarifa zozote kuhusiana na suala la kumlipa kocha fidia... taarifa kamili juu ya kinachoendelea kwa pamoja hatujakijadili," alisema Sanga.

Hata hivyo, Saintfiet alilithibitishia NIPASHE jana kuwa tayari ameshalipwa fedha zake zote na kwamba sasa, anachosubiri ni kufika kwa siku yake ya kuondoka kulingana na tiketi ya ndege aliyokatiwa na Yanga.

Taarifa zaidi zilizopatikana zinasema kwamba uongozi wa hoteli anayoishi  Saintfiet iliyoko Oysterbay umewapa taarifa Yanga inayowataka wawe wamelipa deni la pango na pia wanataka kocha huyo aondoke hotelini hapo haraka.

Katika kipindi chake kifupi cha kuiongoza Yanga, Saintfiet aliwasaidia 'Wanajangwani' kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), lakini akapata matokeo ya sare ya 0-0 katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Bara na baadaye akashuhudia timu yake ikilala kwa mabao 3-0 katika raundi ya pili dhidi ya Mtibwa wiki iliyopita.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Ni bora wangemuacha akafundisha hata yanga kids kuliko kumlipa fedha za bure