ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 12, 2012

Twite aanza mambo Yanga ikiua 3




Yanga  ilizinduka kutoka kwenye kipigo cha pili ndani ya mechi sita na kuifunga Toto African ya hapa 3-1 katika mechi ya raundi ya saba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jana.

Magoli kutoka kwa beki Mbuyu Twite na washambuliaji Didier Kavumbagu na Jerryson Tegete yaliifanya Yanga ipande hadi nafasi ya tatu katika msimamo kwa kufikisha pointi 11, tano nyuma ya vinara Simba na mbili nyuma ya Azam wanaoshika nafasi ya pili. Simba imecheza mechi moja pungufu wakati Azam ina mechi mbili mkononi.

Wageni walianza mechi kwa kasi na walipata goli la kuongoza mapema katika dakika ya pili kupitia kwa Kavumbagu, aliyeuwahi mpira wa kona iliyopigwa na Haruna Niyonzima na kipa wa Toto, Eric Ngwengwe kushindwa kuuokoa.



Selemani Kibuta alipoteza fursa ya mapema ya kuisawazishia Toto katika dakika ya 11 pale alipopiga mpira nje wakati akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga baada ya mabeki Nadir Haroub 'Cannavaro' na Twite kugongana na kuanguka chini.  

Kavumbangu alikaribia kuiongezea Yanga goli la pili katika dakika 20 kwa shuti kali kufuatia pasi ya Oscar Joshua lakini wakati kipa Ngwengwe akiwa ameshakubali matokeo, mpira uligonga nguzo ya lango na kutoka nje.

Mabeki wa kati wa Yanga ambao 'hunogewa' na kupenda kupanda kusaidia mashambulizi walishirikiana kupata goli la pili pale Twite alipofungua akaunti ya mabao katika timu yake aliyojiunga nayo katika kipindi kilichopita cha usajili katika dakika ya 21 kufuatia pasi Cannavaro.

Kipa wa Yanga, Yaw Berko naye hakuwa likizo. Alilazimika kuokoa kiufundi shuti la Hamisi Msafiri katika dakika ya 39 na kuinyima Toto goli.
.
Dakika mbili baadaye, Toto walikuwa na nafasi ya kufunga wakati walipopata penalti iliyotolewa refa Ronald Swai wa Arusha baada ya Twite 'kuunawa' mpira akiwa ndani ya boksi, hata hivyo Emmanuel Swita alipiga nje penalti hiyo. Timu hizo zilienda mapumziko matokeo yakiwa 2-0.

Wenyeji walianza vyema kipindi cha pili na walihitaji dakika 9 tu kupata bao lao kupitia kwa Mussa Said baada ya kumzunguka Cannavaro aliyekuwa mbele yake na kufumua shuti lililokwenda wavuni.

Jerryson Tegete aliifungia Yanga goli la tatu katika dakika ya 68 na kuongeza maumivu kwenye timu inayofundishwa na baba yake, John.

John Tegete aliilalamikia safu yake ya ulinzi kwa kuruhusu magoli ya kizembe, akisema wachezaji walishindwa kuelewana lakini alisema hajakata tamaa kwa sababu ni mechi yao ya pili tu kufungwa.

Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alisema bada ya mechi hiyo kuwa ushindi huo ulitokana na wachezaji wake kucheza kwa kujiamini kutokana na mawaidha waliyowapa na pia wachezaji walioingia kutokea benchi waliimarisha timu lakini alikiri kwamba mechi ilikuwa ngumu sana.

Ligi hiyo itaendelea kesho wakati mabingwa Simba watakaposhuka ugenini Mkwakwani, Tanga kuikabili Coastal Union, huku Azam wakiwa wageni wa Polisi Morogoro kwenyenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Mechi nyingi za kesho zitazikutanisha Prisons dhidi ya JKT Oljoro (Sokoine, Mbeya), Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Vikosi jijini Mwanza jana vilikuwa; Toto Africans: Eric Ngwengwe, Kulwa Aryson, Erick Mulilo, Evarist Maganga/ Eric Kyaruzi (dk.73), Peter Mutabuzi, Hamis Msafiri, Emmanuel Swita, Haruna Athumani/ Suleiman Jingo, Mohammed Hussein, Selemani Kibuta na Mussa Said/ Kheri Mohammed (dk.73).

Yanga: Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athuman Idd 'Chuji'/ David Luhende (dk.60), Frank Domayo/ Shamte Ally (dk. 60), Nurdin Bakari, Didier Kavumbagu, Jerryson Tegete na Haruna Niyonzima.
CHANZO: NIPASHE

No comments: