ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 3, 2012

IGP Mwema ateua mrithi wa Barlow

Raymond Kaminyoge
INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema amemteua Ernest Mangu kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, kuziba pengo lililoachwa na Liberatus Barlow aliyeauawa kwa risasi hivi karibuni.
Hata hivyo, katika uteuzi huo ulioambatana na uhamisho wa baadhi ya makamanda wa mikoa na vikosi vingine vya jeshi hilo, IGP Mwema hakumgusa Kamanda wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda ambaye kumekuwa na shinikizo la kutaka awajibishwe kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari, Daud Mwangosi mkoani huo yaliyotokea Septemba 2, mwaka huu.
Kamanda Barlow aliuawa Oktoba 13, mwaka huu baada ya kupigwa risasi na watu katika tukio ambalo chanzo chake bado hakijafahamika wakati akitoka katika kikao cha harusi. Kabla ya kuhamishiwa Mwanza, Mangu alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, Kamanda wa Mkoa wa Polisi Temeke, David Misime anahamishiwa Mkoa wa Dodoma kuchukua nafasi ya, Zelothe Stephen anayestaafu.
Katika uhamisho huo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Ulrich Matei amehamishiwa Pwani kuchukua nafasi ya Mangu.
Taarifa hiyo ilisema Engelbert Kiondo aliyekuwa Idara ya Upelelezi makao makuu, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke.
Kamanda mpya wa Kikosi cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), anakuwa Rashid Seif ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa pia Idara ya Upelelezi makao makuu. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema aliyekuwa kamanda wa Tazara amepangiwa kazi gani na juhudi za kumpata Senso kutoa ufafanuzi hazikufanikiwa.
Nafasi ya Matei Viwanja vya Ndege imechukuliwa na Deusdedit Kato ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa makao makuu ya jeshi hilo.
Katika mabadiliko hayo, Kamanda wa Kikosi cha Ufundi, Shaban Hiki anahamia Makao Makuu ya Polisi na nafasi yake inachukuliwa na Lucas Mkondya aliyekuwa makao makuu.
Mabadiliko hayo pia yamemhusisha aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Johansen Kahatano anakwenda kusimamia Mradi wa Smatter Traffic na nafasi yake imechukuliwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabani (RTO) Mkoa wa Pwani, Swalehe Mbaga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhamisho huo pia umewahusisha baadhi ya wakuu wa operesheni wa mikoa, wakuu wa vikosi vya kutuliza ghasia, wakuu wa polisi wa wilaya na wakuu wa upelelezi wa wilaya.
Jeshi hilo limesema kwamba uhamisho huo ni wa kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo yake.

Mwananchi

No comments: