Mpenzi anayekuja kwako kwa ajili ya kutimiza matakwa yake binafsi huyo ni kirusi. Maana yake, ulichonacho ndiyo kimemvuta. Siku hicho kitu kikiondoka, hawezi kuwa nawe tena. Ipo mifano mingi ya watu wanaolia leo hii, angalia nawe usije ukaingia kwenye orodha.
Mathalan, amekupenda kwa sababu ya cheo chako. Siku hicho cheo kikiondoka hawezi kukupenda tena. Zaidi ni kwamba si kweli kuwa alikupenda, ila aliingia kwako kwa mtego wa fedha, kazi na kadhalika. Wewe siyo ATM wala daraja la ajira, usikubali kutumiwa.
Unatakiwa kuulinda moyo wako usitoneshwe, kwa hiyo fuatilia uhusika wa mwenzi wako katika matukio mbalimbali. Kama ni hasi, basi tazama mahali uliposimamia. Ikiwa wewe upo chanya, basi iwe ni sababu ya kumtambua kwamba ni kirusi, kwa hiyo mdiliti haraka.
Kwa kupitia tangu mwanzo wa makala haya, nimekuwa nikieleza vitu mbalimbali vyenye sura ya kirusi kwenye mapenzi. Ni vizuri sasa kuvichambua kimoja baada ya kingine kwa lengo la kukuwezesha kukijua kirusi ndani ya uhusiano wako. Kirusi kinaweza kuwa wewe mwenyewe, mpenzi wako au watu wa pembeni.
Muhimu kwako ni kutambua thamani ya maisha yako. Hupaswi kurudi nyuma kwa sababu umetendwa. Ni sawa kuumia lakini hutakiwi kuinamisha kichwa muda wote kwa sababu ya mtu ambaye ameonesha kutojali mapenzi uliyompa. Inua macho juu, weka imani kwamba Mungu yupo anakulinda. Tazama mbele kwa matumaini kuwa akupendaye kwa dhati anakuja na akifika, hutateseka tena.
MKATAE MAPEMA MPENZI HUYU
Kuna falsafa inavyoeleza kuwa, rafiki wa rafiki yako ni rafiki yako. Rafiki wa adui yako ni adui yako. Adui wa adui yako ni rafiki yako. Hii iwe sababu ya wewe kuchunguza jinsi mpenzi wako alivyo kisha upate majibu ya kukusaidia mbele ya safari.
Siku zote mpenzi anatakiwa awe adui wa adui yako, ikiwa ni rafiki wa adui yako, huna sababu ya kuendelea naye. Fikiria kwamba mtu fulani kwako ni adui na hapendi mafanikio yako kiasi kwamba amejionesha hivyo waziwazi. Inakuwaje mwenzi wako awe rafiki yake?
Hatua ya kwanza muonye. Siku zote napenda uamini katika kufundisha. Muelekeze mara kwa mara kuwa anachokifanya siyo sahihi kwa afya ya uhusiano wenu. Maelekezo yako ndivyo unavyoskani kirusi. Akishindwa kubadilika, basi mdiliti.
Naomba uelewe kuwa unapomdiliti unakuwa umejiokoa. Kuwa na mpenzi rafiki wa adui yako ni sawa na kuzungukwa na maadui wawili. Huwezi kujua faida anazopata kutoka kwa huyo adui yako, kama hakuna faida, basi angeachana naye. Tazama mbele kwa faida ya maisha yako.
Kirusi pia unaweza kuwa wewe pale unapokuwa rafiki wa adui wa mpenzi wako. Iweje kuwa rafiki na mtu ambaye hampendi mwenzi wako? Unapaswa kumlinda na kumtetea mwandani wako mahali popote na wakati wowote. Achana na huyo mtu ili kumfanya mpenzi wako awe na furaha.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment