HATMA ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) waliosimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi, itajulikana baada ya wiki mbili.
Jumatano iliyopita, bodi ya shirika hilo ilimfukuza kazi Mhando baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa tuhuma dhidi yake zilikuwa za kweli.
Vigogo wengine waliosimamishwa kazi Julai 15 mwaka huu, lakini bado hawajafahamu hatma yao, ni Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Manunuzi, Harun Mattambo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Bodi wa Tanesco, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, alisema bado tuhuma za maofisa hao zinachunguzwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utouh.
“ Baada ya wiki mbili kuanzia sasa, uchunguzi huo utakuwa umekamilika na CAG atatukabidhi ripoti hiyo, ili tuifanyie kazi,” alisema Jenerali Mboma.
Alisema CAG akionyesha kwamba tuhuma zinazowakabili watendaji hao si za kweli, bodi itawarudisha kazini. Jenerali Mboma alisema ikiwa CAG atabaini kwamba tuhuma za ubadhirifu zinazowakabili maofisa hao ni za kweli, bodi itaunda kamati maalumu ya kuwahoji.
“Bodi itaunda kamati maalumu ya kuwahoji maofisa hao ili nao wapate nafasi ya kujitetea kuhusu tuhuma hizo,” alisema Jenerali Mboma. Alisema katika utetezi huo, bodi itapokea taarifa kutoka kwa kamati hiyo kwa ajili ya uamuzi.
“Kwa hiyo unaona jinsi tunavyoshirikisha watu mbalimbali katika kushughulikia tatizo hili, lengo ni kuhakikisha kuwa haki inatendeka, bodi iliwasimamisha kazi, uchunguzi umefanywa na CAG, kamati itawahoji na bodi kutoa uamuzi, huko ndiko kutenda haki,” alisema Jenerali Mboma.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment