ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 1, 2012

UWAJIBIKAJI HAFIFU KIKWAZO CHA MAENDELEO YA MIRADI MKOANI SINGIDA


Mjumbe wa halmashauri kuu CCM taifa (NEC), Hassan Mazala akifungua mafunzo kwa wakulima 70 wa vitongoji vya kaya ya Mwankoko jimbo la Singida mjini.Kushoto ni mwenyekiti wa kijiji cha Mwankoko,Yahaya na kulia ni afisa mtendaji wa kata ya Mwankoko,Ramadhani Ng'imba.
Mjumbe wa halmashauri kuu CCM taifa (NEC) kutoka manispaa ya Singida, Hassan Mazala (wa tatu kutoka kulia) akimkabidhi mbegu bora ya choroko mama mmoja mkulima mkazi wa kijiji cha Mwankoko.Mbegu hizo ni sehemu ya msaada wa tani 50 za mbegu za choroko,mbaazi na degu zilizotolewa msaada na mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mh. Mohammed Dewji.
Mjumbe wa halmashauri kuu CCM taifa (NEC) Hassan Mazala (katikati walioketi mwenye miwani) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wakulima wa kata ya Mwankoko wanaohudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa.
 
Baadhi ya wakulima wa kata ya Mwankoko jimbo la Singida mjini,wakisikiliza makini ufunguzi wa mafunzo yao ya kilimo cha kisasa.(Picha na Nathaniel Limu).
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa (NEC) manispaa ya Singida, Hassan Mazala, Alisema wafadhili au baadhi ya viongozi hasa wa kuchaguliwa,wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ikiwemo ya miradi ya gharama kubwa na lengo lao kuu likiwa, ni kuwaendeleza walengwa kijamii na kiuchumi.
Mazala alisema hayo wakati akifungua rasmi mafunzo ya kilimo cha kisasa yanayohudhuriwa na wakulima 70 wa vitongoji vya kata ya Mwankoko. hata hivyo, alisema kuwa uzoefu unaonyesha wazi kwamba miradi hiyo ikiwemo ya kilimo,malengo yake yamekuwa hayafikiwi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uwajibikaji hafifu.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa malengo ya mfadhili au kiongozi wa kuchaguliwa,yasipotimia,pamoja na mambo mengine,hali hiyo inaweza kusababisha kumudhoofisha mhusika akapunguza kasi ya kutoa misaada mingine zaidi.
“Kwa nini nayasema haya,ndugu zangu wakulima ninyi ni mashuhuda wazuri juu ya misaada mbalimbali ya miradi ambayo imekuwa ikitolewa na mbunge wetu, Mohammed Dewji kwa muda mrefu.Lengo la Dewji katika miradi hiyo, ni kumwendeleza mwananchi wa manispaa ya Singida kiuchumi, ili aweze kuishi maisha bora”alifafanua na kuongeza;
“Lakini miradi mingi haijatoa matunda aliyokuwa akikikusudia mbunge wetu.Na hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na wasaidizi wake ambao ni watendaji wa manispaa, kutokusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi husika”.
Mazala alisema wakati umefika sasa kuthamini na kutambua kuwa miradi inayotolewa misaada kwa wakulima na wananchi wengine, ni kwa ajili ya manufaa yao na si ya watoaji.
Katika hatua nyingine,alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wakulima hao kuacha kilimo cha mazoea na badala yake wajikite katika kilimo cha kisasa,kibiashara na chenye malengo.
Alisema ni kwa njia hiyo pekee,watakuwa wamejijengea mazingira mazuri ya kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo,kuongeza pato la mkulima na uhakika wa chakula katika kila kaya.
Kwa mujibu wa mtaalam wa kilimo wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Singida mjini,Casmir Joackim,mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo zaidi wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa,ni sehemu ya mradi mkubwa wa kilimo unaofadhiliwa na mbunge Dewji.
Mradi huo wa kilimo,utamgharimu mbunge Dewji zaidi ya shilingi milioni 250.Fedha hizo ni kutoka kwenye mfuko wake binafsi.

No comments: