Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amewaondolea mashtaka washtakiwa watatu katika kesi ya uhujumu uchumi, kula njama na kusafirisha na kuuza nje ya nchi wanyama 136.
Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma ya kuuza nje ya nchi wanyama hao aina 14 tofauti ambao ni nyara zenye thamani ya Dola za Marekani 113,715.00 sawa na Sh. 170,572,500.00, mali ya serikali ya Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na kufuta mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao, DPP ametoa kibali cha kuunganishwa kwenye kesi hiyo mtu mwingine, Michael Mrutu (30) ambaye ni afisa usalama wa kampuni inayosimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ya Development Company Limited (KADCO).
Wakili wa Serikali Arafa Msafiri akisaidiana na Evetha Mushin na Pius Hila, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Simon Kobelo, walidai mahakamani hapo kuwa, DPP amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa sheria inayompa nguvu ya kumwondolea mashtaka mtuhumiwa yoyote na kwamba Mrutu anakuwa mshatkiwa wanne kwenye kesi hiyo.
Walioondolewa mashtaka ni Jane Mbogo ambaye ni Mfanyakazi wa KIA raia wa Kenya, Veronica Beno Afisa Mkuu wa usalama na Locken Kimaro ambaye ni Afisa Usalama wa kampuni hiyo.
Baada ya Mrutu kupandishwa kizimbani na kuunganishwa katika kesi hiyo, aliiomba mahakama kumpa nafasi ya kuweka wakili, ambapo wakili wa serikali alieleza mahakama hiyo kuwa uwezo wa kutoa dhamana kwa mshtakiwa huyo haupo chini ya mahakama hiyo bali Mahakama Kuu.
Hakimu Kobelo alisema mshtakiwa huyo anapaswa kupeleka ombi Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata dhamana kutokana na kwamba mahakama hiyo haina nguvu kisheria ya kusikiliza kesi hiyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mfanyabiashara Kamran Ahmed raia wa Pakstani na mkazi wa Arusha, Hawa Mang’unyuka (51) mfanyabiashara na mkazi wa jijini Dar es Salaam, Martin Kimati (58) ambaye alikuwa afisa mifugo mwajiriwa wa serikali na sasa ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibosho.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kabla na baada ya Novemba 26 mwaka 2010, kinyume na kifungu na 57 (1) na 60 cha sheria ya
uhujumu uchumi na kudhibiti uhalifu, ambapo wanyama hao walisafirishwa hadi mji wa Doha nchini Qatar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment