ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 4, 2012

DNA: Nusu ya watoto ni wa kusingiziwa

Ni wale wanaofanyiwa utafiti na mkemia mkuu wa Serikali

Florence Majani
ASILIMIA 44 ya wapenzi wanaokwenda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupima vinasaba (DNA), kwa ajili ya kujua uhalali wa watoto kwa baba, wamethibitishiwa kuwa watoto hao si wa kwao.
Takwimu za mwaka 2012 kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, zimeainisha kuwa kati ya watu 90 waliokwenda kupima DNA, 40 ambao ni sawa na asilimia 44, wameonekana kubambikiziwa watoto.
Takwimu hizo za kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, zilionyesha kuwa katika kesi 50 za waliokwenda kupima, matokeo yalionyesha kuwa ni wazazi halisi wa watoto wao.
Hata hivyo, idadi hiyo inayoonyesha kuwa kinababa siyo wazazi halisi wa watoto, imeshuka ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2008/2009 ambazo zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliochukua vipimo hivyo wamebainika kuwa si wazazi halisi wa watoto hao.
Mkemia na Mtambuzi wa Vinasaba vya Makosa ya Jinai, Gloria Machuve alisema jana kuwa ni vyema ikitambulika kwamba takwimu hizo zinatokana na watu waliokwenda kupima baada ya kutokea migogoro ya kimapenzi na siyo takwimu iliyochukuliwa kutoka kwa Watanzania wote.
“Hatusemi kuwa sasa  wanaume wote Tanzania wanalea watoto ambao si wa kwao. Hizi ni takwimu za waliokuja kupima; yaani wale wenye matatizo,” alisema.
Machuve alisema katika maabara hiyo, kesi nyingi zinazoonyesha kuwa watoto hao si halali, zimetokana na uhusiano wa ziada au usio rasmi baina ya wenza.
“Kwa mfano, mwanamume ana mwanamke wa nje ya ndoa au mwenye uhusiano usio rasmi, halafu mwanamke huyo anadai mtoto ni wa huyo mwanamume, mara nyingi  matokeo huwa si mazuri,” alisema Machuve.
Aidha, Machuve alisema takwimu za kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 zinaonyesha kuwa tabia ya upimaji imeongezeka miongoni mwa Watanzania.
Alisema mwaka 2005/2006, kesi za upimaji wa vinasaba zilikuwa 96 na mwaka 2008/2009 kesi hizo zilikuwa 113 wakati mwaka 2009/2010, kesi za waliokwenda kupima zilifikia 125.
Alisema watu wengi wanaojitokeza kupima katika miaka ya karibuni wanataka kufahamu uhalali wa watoto wao ili wawajibike kuwalea kihalali.
“Lakini pia kuongezeka kwa kesi za utambuzi wa vinasaba kunatokana na kukua kwa uelewa na uwezo wa kiuchumi,” alisema Machuve.
Alisema kuwa idadi ya upimaji wa DNA imeongezeka pia kwa watu wanaotaka kugawana mirathi na masuala ya uhamiaji.
“Wale wanaoishi Ulaya wanapotaka kuchukua watoto au ndugu zao, ni lazima wapimwe ili kuhakikisha, hivyo wanatuma vielelezo vyao kisha tunavifananisha na vielelezo vya walio hapa,” alisema.
Machuve alisisitiza kuwa katika kesi nyingi, wanawake hukimbia katika hatua za upimaji na ni mara chache wanaume wakaukwepa mchakato huo.
Aidha, Machuve alisema upimaji wa vinasaba vya makosa ya jinai umefanikiwa kwa asilimia kubwa na asilimia 80 ya kesi zilitoa majibu chanya, yaani vielelezo vilivyoletwa viliwanasa watuhumiwa wa makosa ya jinai.
“Kuna kesi kama za ubakaji na mauaji ambazo tunaletewa vielelezo kama mbegu za kiume au silaha na tulipofanya utambuzi wa vinasaba tuliupata ukweli  kwa kuwanasa watuhumiwa katika asilimia 80 ya kesi,” Machuve.
Upimaji wa jinsia tawala
Aidha, mkemia huyo alisema maabara hiyo inapima jinsia tawala kwa wale wanaozaliwa na utata wa jinsia.
Alisema wapo watoto wanaozaliwa wakiwa na utata katika jinsia, kwa mfano ana sura ya kiume na sauti lakini ana sehemu ya siri ya kike.
“Watu kama hao wakifika hapa, tunaweza kuwapima ni jinsia ipi inatawala ili wapatiwe matibabu na kisha waitumie jinsia inayotawala. Wanaweza kufanyiwa upasuaji au kupewa vichocheo vya jinsia inayotawala,” alisema.
Machuve pia alizungumzia suala lililojitokeza hivi majuzi kwamba Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kariuki alisema baadhi ya kesi za upimaji DNA zitolewe bure akisema hilo haliwezekani kwani mchakato mzima wa upimaji una gharama kubwa.
“Upimaji wa DNA una gharama nyingi ambazo zinahitaji fedha, kuna gharama za kuendesha mtambo, kuna dawa  ambazo punje ndogo tu inagharimu Sh200,000, hatuwezi kutoa bure huduma hii labda Serikali ilipie gharama hizo,” alisema.
Mwananchi

No comments: