ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 4, 2012

Mpangaji amfikisha mwenye nyumba kortini

MPANGAJI wa nyumba  namba 608 iliyopo eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, Diana Philibert (41) amefungua kesi ya madai ya zaidi ya Sh24.2 milioni  katika Mahakama ya Nyumba ya Kinondoni  dhidi ya  msimamizi wa nyumba hiyo, Godfrey  Lubomola.
Katika kesi hiyo, iliyofunguliwa na  Diana kupitia wakili wake  Sabasaba  Mashiku, anaiomba mahakama iamuru alipwe kiasi hicho cha fedha kama fidia ya  kung’olewa kwa mita ya Luku na Service line katika nyumba  hiyo aliyokuwa amepanga.
Kubomolewa madirisha,  milango na kuibiwa baadhi ya vitu vyake  ikiwamo fedha taslimu Sh5 milioni, kompyuta aina la Laptop, simu ya mkononi na nyaraka zake mbalimbali.
Pia  anaiomba mahakama iamuru alipwe Sh10 milioni kama fidia ya usumbufu, kukosa amani  kwa kumuhofia kuwa muda wowote angeweza kwenda kumfanyia kitu chochote kibaya  na kwamba adhabu nyingine mahakama hiyo ya Nyumba iiangalie itakayoiona inafaa.
Katika kesi hiyo, Lubomola anadaiwa kuwa  Mei 12, mwaka huu, akiwa msimamizi wa nyumba hiyo inayomilikiwa na  Redemta Kalemela anayeishi nchini Uingereza  alibomoa nyumba hiyo aliyokuwa anaishi Diana bila  ya kuvunja mkataba wa upangaji wala kumpa taarifa ya kufanya tukio hilo.
Diana akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Hemed wa Mahakama hiyo ya Nyumba ya Kinondoni alidai kuwa, Lubomola alibomoa alikwenda nyumbani kwake na kutoa milango na madirisha wakati mvua ilikuwa ikinyesha.
Alidai kuwa  wakati Lubomola akifanya uharibifu huo, jirani yake  alimpigia simu na kumuuliza uko wapi mbona nyumba yako inabomolewa na kutolewa milango, nyavu na  madirisha.
Aliendelea kudai kuwa Lubomola wakati akifanya tukio hilo alikuwa na vijana wahuni wa Sinza ambao waliiba droo zake mbili  zilizokuwa na nyaraka zake mbalimbali ikiwamo mikataba ya upangaji aliyoingia na mtuhumiwa huyo.
Aliongeza kwa kudai kuwa baada ya kufika nyumbani kwake na kushuhudia tukio hilo alimuita balozi na baadaye alikwenda katika kituo cha polisi cha Urafiki kuripoti na kupewa RB  namba UPR/3876/2012  na UPR/4585/2012 kwa ajili ya kumkamata.
Diana alidai kuwa alipomuuliza Lubomola kwanini  alifanya hivyo kwa kinywa chake alimwambia kuwa “amepata mtu wa hela ndefu”.
Mwananchi

No comments: