Wednesday, December 5, 2012

Mfanyabiashara afia hoteli ilimopanga Timu ya Bunge

MFANYABIASHARA wa madini aina ya Tanzanite mkoani Arusha, Ngerii Olerumwa anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40 amekutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha ndani ya Hoteli ya Premier Palace ambayo Timu ya Soka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano imeweka kambi jijini Arusha.

Maiti ya mfanyabiashara huyo iligundulika saa 3:30 asubuhi jana mara baada ya mhudumu wa hoteli hiyo kugonga kwa muda mrefu mlango wa chumba alichokuwa amefikia marehemu huyo bila mafanikio na kisha kubaini alikuwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo akiwamo meneja wa hoteli hiyo, ambaye alikataa kutaja jina lake hadharani alisema kwamba marehemu huyo aliwasili hotelini hapo Desemba 3 mwaka huu, saa 1 :00 jioni na kukodi chumba kimojawapo hotelini hapo.

Meneja huyo akisimulia tukio hilo alisema kwamba marehemu aliwasili akiwa peke yake hotelini hapo na kubainisha kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kukodi chumba hotelini hapo.

Alisema ilipotimu jana saa 3:30 asubuhi wakati mhudumu wa hoteli hiyo akigonga mlango wa chumba alichofia marehemu kwa lengo la kufanya usafi mlango huo haukuweza kufunguliwa kwa wakati hali iliyosababisha kufanya juhudi za kuufungua mlango huo kwa lazima.

Alisema kwamba baada ya kufanikiwa kuufungua mlango huo walijaribu kumwamsha lakini hakuweza kuamka hali iliyowafanya wawaarifu polisi.

Polisi walifika eneo la tukio na kuchukua maelezo kwa baadhi ya watumishi wa hoteli hiyo wakiwamo walinzi wa hoteli hiyo huku baadhi ya wabunge wanaounda timu ya wabunge wakitaharuki kutokana na tukio hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndugu wa marehemu ambao walikusanyana nje ya hoteli hiyo walisema kwamba wameshtushwa na kifo cha ndugu yao na wanahisi kwamba aliuawa katika mazingira ya kutatanisha huku wakiwataka polisi kubaini chanzo cha kifo cha marehemu.

Akihojiwa na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabass alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisisitiza kwamba uchunguzi unaendelea.

Sabas alisema kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ndani ya Hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru na atatoa taarifa kamili ya tukio hilo kuanzia leo mbele ya waandishi wa habari.

Mwananchi

No comments: