Thursday, December 6, 2012

Mtwara walipwa Sh.130 kupisha bomba la gesi

Abdallah Nyodo akiwa amebeba mfano wa shina la muhogo likiwa na mihogo yake walilolipwa fidia y ash. 130 ili kupisha ujenzi wa bomba la gesi. 
Picha na Abdallah Bakari. 
WAKULIMA wa Kijiji cha Mangamba Manispaa ya Mtwara-Mikindani ambao bomba la gesi linajengwa na Serikali Kijiji cha Msimbati katika Halmashauri ya Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam na kupita kwenye mashamba ya wakulima hao  wameulalamikia mradi huo badala ya kuufurahia.
Kwanini wakulima hao wanalalamikia mradi huo mzuri wa gesi? Hilo ni moja ya maswali ambayo watu wengi wamekuwa wakijiuliza.  Wananchi hao wanaulalamikia mradi huo kwa sababu wamedhulumiwa.
Wanasema fidia waliolipwa kwenye mashamba yao ambako bomba la gesi limepita ni kidogo na kwamba hailingani na kipande cha muhongo wa kukaanga ambao unauzwa Sh100.
Fidia ambayo inalalamikiwa na wakulima hao ni ya mazao, hususani zao la muhogo ambapo wamelipwa  Sh130 kwa shina moja. Wakulima hao kwa nyakati tofauti wanasema kiwango kidogo kuliko thamani ya zao hilo.
Wakulima hao wamewatupia lawama wathamini waliothamini mazao yao huku wakisema ndio matunda ya kuwa na wasomi wasiojua thamani ya mazao ya kilimo.
Mkazi wa Mangamba, Abdallah Rahisi Nyodo (34) ni miongoni mwa wakulima ambao wamepoteza mashamba yao baada ya bomba la gesi kupita katika eneo hilo.
Anasema hawakutendewa haki kwa kuwa walipaji wameshusha thamani ya zao hilo.
“Hadi leo hatuamini kama kweli Serikali inaweza kufanya dhuluma hii kwa wakulima wake, shina la Muhogo wametulipa kwa Sh130 hivi kuna haki hapo?. Shina hili la muhogo, mkulima ametumia misimu miwili hadi mitatu kulihudumia leo analipwa bei ya kipande cha muhogo wapi haki?
“Malipo haya yamefanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), hebu jiulize leo hii shina la Muhogo ukiuuza kwa wachuuzi utapata Sh5,000 hadi 7,000, hii ni bei ya shamba, ukipeleka mjini tenga la mashina matano ya muhogo mbichi utauza Sh50,000 hadi Sh40,000”
Anabainisha kuwa shamba lake lilikuwa na mihogo 486 ambayo amelipwa fidia ya Sh130 kwa shina na kupata jumla ya Sh63,180 badala ya Sh2.4 milioni iwapo mashina hayo angeyauza kila shina moja kwa bei ya Sh5,000.
Gesi siyo mkombozi’
“Muhogo kwetu ndiyo zao kuu la chakula, ndiyo kimbilio letu, kwenye shina moja unaweza kupata mihogo mikubwa hadi 10 ambayo ukiamua kuiuza kwa rejareja kila muhogo unaweza kutoa vipande kumi vya Sh100 kwa kila kimoja.
“Hapa gesi hatuwezi kuitazama kwa jicho la ukombozi bali ni janga linalopora kidogo tulichonacho, kama wapo wanaosema gesi ni neema basi ni kwa upande wa Serikali, sio sisi wakulima,”anasema.
Mkazi mwingine wa Mangamba, Ali Abdallah Mabangi (38) anasema shamba lake lenye mashina ya mihongo 280 amelipwa fidia ya Sh36,400 baada ya  kulipwa Sh130 kwa kila shina.
“Fidia ya zao la muhogo kwa kweli imenigandamiza, ni heri wangeniambia ning’oe mihogo yangu nikatafute kwa kuuza kuliko kulipwa fidia hii, ningeuza zaidi ya Sh5000 kwa shina, mihogo yangu nimeihudumia kwa miaka mitatu leo nalipwa Sh130 kwa shina, sio haki.
“Mbegu ya mihogo nimeichukua katika  kituo cha utafiti cha Naliendele, tumenunua wastani wa Sh200 kwa mti, leo shina tunalipwa Sh130i, shina ambalo unaweza kula wewe na familia yako mkashiba, hivi kosa letu ni kuwa wakulima? Hizi ndizo athari za kuwa na wataalam wasiojua thamani ya kilimo na mazao au wataalam wasiojali haki,” anasema.
Akionyesha mwenye jazba Mabangi anasema: “Sisi waathirika wa gesi sio wafaidika, leo hii tukitaka kula muhogo tunanunua kwa wasioathirika, kwa fidia hii siwezi kununua shamba lingine tena, kwa sisi wakulima ukikosa shamba ndiyo masikini daima.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangamba Mwanusa Hassan (47) anathibitisha wakulima wake kulipwa fidia isiyoendana na thamani ya zao la muhogo
Hassan anasema wakulima hao hawajui mtu wa kumlalamikia kwa sababu kazi ya kuliopa fidia imefanywa na maofisa wa TPDC kutoka Dar es Salaam na kuondoka.
“Wakulima walijaribu kupinga fidia hiyo, lakini wakaambiwa haiwezi kubadilishwa kwa sababu ndiyo iliyotolewa na Serikali, wamebaki wanauguza maumivu ya kuporwa nguvu zao na Serikali,” anasema Hassan ambaye wakati wa ulipaji fidia alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangamba.
Shina la muhogo linauzwa Sh4,000
Mkazi wa Majengo Manispaa ya Mtwara Mikindani, Yusuf Namkwinda (30) ni mchuuzi wa biashara ya mihogo mibichi ambayo amekuwa akiikaanga na kuiuza (chips dume), anasema kwa sasa mihogo mibichi ananunua kati ya Sh4,000 hadi 5,000 kwa shina la muhogo.
“Ninapokwenda shambani kununua mihogo nanunua shina kwa bei kati ya Sh4,000 hadi 5,000 kutokana na ukubwa wa shina, nanunua tenga moja la mihogo kati ya Sh40,000 hadi Sh45,000.
“Tenga linakuwa na mihogo kati ya 70 mpaka 80, nikiuza shina moja naweza kupata kati ya Sh10,000 hadi 12,000, nauza kipande cha muhogo mbichi Sh200, muhogo mmoja unaweza kutoa vipande kati ya saba mpaka 10, nakaanga ‘chips dume’ kipande kimoja nauza Sh100, muhogo mmoja unaweza kutoa vipande mpaka 20, tenga moja napata kati ya Sh55,000 hadi 70,000,”anasema.
Mmoja wa wataalam wa kilimo Manispaa ya Mtwara-Mikindani Salum Mnyitu anasema thamani ya uzalishaji wa zao la muhogo kwa shina moja inakadiriwa kufikia kati ya Sh2,500 hadi 3,500.
“Si haki kulipa Sh130 kwa shina la muhongo hata kama lina msimu mmoja tangu lilipopandwa bado gharama za kulitunza ni zaidi ya Sh130, ukizingatia mbegu nayo wanainunua, wameshindwa kuthaminisha zao hili, thamani yake ingeangaliwa kwa kuangalia umuhimu wa zao hilo kwa wakulima wenyewe,”anasema Mnyitu.
Mbunge wa Mtwara mjini, Asnain Murji anasema hajapata malalamiko rasmi kutoka kwa wakulima hao licha ya kukiri kuwa kiwango walicholipwa ni kidogo ukilingalisha na thamani ya zao hilo na gharama za uzalishaji.
“Nitafuatilia hilo, nipe muda, ninachofahamu ni kwamba Serikali ndiyo iliyopanga viwango hivyo, kama wamelipwa hivyo si haki, thamani ya muhogo kwa walaji ni kubwa,”anasema Murji.
Profesa Sospeter Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani na mwandishi wa makala haya kupata ufafanuzi wa madai ya wakulima hao alionekana kulikwepa kuzungumzia jambo hilo.
Baada ya mwandishi kuomba ufafanuzi wa suala hilo Waziri Muhongo aliomba apigiwe baadae, alipopigiwa baadae hakupokea simu bali alijibu kwa ujumbe wa maneno uliosomeka “I’m in meeting” (nipo kwenye mkutano).
Mwananchi

No comments: