ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 18, 2013

Hakimu aanzisha mahakama bandia


  Awalima watuhumiwa faini chapchap
  Atumia kibatari kuendesha kesi usiku
  Takukuru wamkamata live
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Lupata katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Andrew Siwale na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisegese, Gasper Bagomoke, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kushirikiana kuanzisha mahakama bandia kinyemela.

Hakimu na Mtendaji huyo, wanadaiwa kuitumia mahakama hiyo kuendesha kesi kuanzia jioni hadi usiku na kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa watu ambao wanashtakiwa kwao.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka, watuhumiwa hao walikamatwa juzi baada ya taasisi hiyo kufuatilia nyendo zao na kubaini mambo wanayoyafanya kinyume cha sheria.


Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja walishirikiana na kutumia jengo la Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisegese kuanzisha mahakama bandia kinyemela ambayo wamekuwa wakiitumia kusikiliza kesi kuanzia saa 12:00 jioni hadi 4:00 usiku.

Mtuka alisema Takukuru katika uchunguzi wake, ilifika kwenye ofisi za Msajili wa Mahakama wa Wilaya ya Rungwe kujua uhalali wa mahakama hiyo na kubaini kuwa haipo kwenye orodha za mahakama za mwanzo wilayani humo.

“Uchunguzi wetu umebaini kuwa mahakama hiyo iliyofunguliwa kinyemela, huanza kazi zake za kusikiliza kesi kuanzia majira ya saa 12:00 jioni na kuendelea hadi saa 4:00 usiku, kwa kuwa jengo la Ofisa Mtendaji ambalo ndilo wanalitumia kufanyia shughuli zao halina umeme, watuhumiwa walilazimika kuwasha vibatari ili wapate mwanga,” alisema Mtuka.

Kwa mujibu wa Mtuka, baada ya Takukuru kubaini uwepo wa mahakama hiyo, maofisa wake waliweka mtego kwa kutumia mwananchi mmoja aliyekuwa na kesi kwenye mahakama hiyo bandia ambaye alitakiwa kutoa rushwa ya Sh. 200,000 ili apewe upendeleo katika kesi iliyokuwa ikimkabili.

Alisema kuwa wakati watuhumiwa hao wakikabidhiwa fedha hizo na mwanachi huyo, ambaye Mtuka hakutaka kumtaja jina kwa kuwa uchunguzi wa suala hilo unaendelea, ndipo makachero wa Takukuru walipowakamata na kuwapeleka katika ofisi za Takukuru wilayani Rungwe kwa mahojiano.

Kamanda Mtuka alisema kuwa Takukuru pia ilipata wananchi wengine zaidi ya sita waliotoa ushahidi na malalamiko juu ya kudhulumiwa haki zao kupitia mahakama hiyo bandia.

“Watuhumiwa wote tunawafikisha mahakamani leo (jana) mchana kwa sababu taratibu zote za kuwafungulia kesi zimekamilika na tunao ushahidi wa kutosha baada ya wananchi zaidi ya sita kujitokeza na kutupatia ushirikiano wa kutosha kuhusiana na suala hili,” alisema Kamanda Mtuka.

Alisema tukio hilo limeishtua Takukuru Mkoa wa Mbeya na sasa imeamua kuweka kipaumbele na kuelekeza nguvu zake katika mahakama za mwanzo na kwenye mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata ili kuibua uozo zaidi kwenye maeneo hayo ambayo wanaamini kuwa wananchi wengi wanadhulumiwa haki zao.

Habari tulizozipata baadaye jana zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walisomewa mashitaka katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, na kwamba walikana na kuachiwa kwa dhamana hadi Februari 13, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: