Jeraha katika mkono wa David Kweka |
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, David alifika Sinza akiambatana na kaka yake, Elnadia Kweka kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo iliyokuwa inaoneshwa katika runinga ya baa hiyo na wote walikuwa wakishabikia klabu ya Chelsea.
Wakati Man United ikiwa inaongoza mabao 2-0, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakitamba na kutoa maneno ya kejeli kuonesha kwamba wao ndiyo wababe wa soka nchini England. David na kaka yake hawakuwa na la kusema hadi Chelsea iliposawazisha mabao hayo na ubao wa matokeo kusomeka 2-2.
Pamoja na hali hiyo, mashabiki wa Man United waliendeleza tambo kwa kudai kwamba lazima watapata bao la tatu wakati wowote na kumaliza mchezo huo wakiwa washindi. Wakati tambo hizo zikiendelea, Elnadia alishikwa na haja ndogo na kutaka kwenda msalani, ndipo mtu aliyejulikana kwa jina moja la Wambura aliyekuwa akishabikia Man United alipomzuia na kumwambia kuwa alikuwa akitaka kukimbia.
“Ulitokea ubishi mkubwa kati ya Elnadia na Wambura ambaye alijitambulisha kama afisa usalama na ulipozidi, shabiki huyo wa Man United alichomoa bastola na kumtishia.“Hali hiyo ilizua kizaazaa ndipo David alipoamua kumvaa Wambura na kutaka kumnyang’anya bastola yake ili kumuokoa kaka yake. Wawili hao walinyang’anyana bastola hiyo kwa muda mrefu hadi ilipofyatuka risasi tatu kwa bahati mbaya,” alisema shuhuda mmoja.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, risasi moja kati ya hizo ilimpata David katika mkono wake wa kulia.
Watu walitawanyika na baada ya muda David alichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Palestina ambako alishonwa nyuzi 12 katika mkono wake.
Taarifa zaidi za tukio hilo zinasema kuwa David alipoteza shilingi milioni moja la laki saba ambazo alipewa na mteja wake kwa ajili ya kwenda kumnunulia ‘gear box’.
Habari zaidi zinasema, jalada la kesi hiyo limefunguliwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, Ubungo jijini Dar kwa namba URP/RB 17878/2013, KUJERUHI KWA SILAHA.
Kwa mujibu wa askari mmoja wa kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, Wambura anashikiliwa katika kituo hicho.
GLP
No comments:
Post a Comment