Tuesday, March 26, 2013

UNACHOKULA LEO, NDICHO KINACHOAMUA AFYA YAKO YA KESHO!


TUKUBALI au tukatae, lakini ukweli ni kwamba jinsi tulivyo kiafya, kunatokana na vyakula tunavyokula kila siku na staili ya maisha tunayoishi kila siku. Katika kila aina ya chakula tunachokula, kuna virutubisho na hivyo virutubisho vina kazi yake mwilini, vinapopungua husababisha tatizo mwilini.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa wastani mtu mzima anapaswa kula milo ya matunda na mboga kati ya mitano hadi tisa kwa siku, kiwango ambacho ni watu wachache sana wanakifikia kwani hawajui wala hawapendi kujua umuhimu wake.
Kutokana na hali hiyo, shirika hilo limesema kwamba asilimia 95 ya watu duniani hawapati virutubisho vinavyohitajika mwilini na asilimia 75 hula vyakula ambavyo huwaletea madhara zaidi mwilini kuliko faida. Kutokana na ukweli huo, maradhi yataendelea kuongezeka na tutaendelea kuteseka kiafya mpaka hapo tutakapokubali kubadili staili zetu za ulaji.Kuna dhana potofu imejengeka miongoni mwetu kwamba chakula kizuri ni kile kilichopikwa kwa mafuta mengi kama chips, pilau yenye mafuta mpaka yanatiririka mkononi, nyama za kukaanga kwa mafuta na vyakula vingine vinavyopikwa kwa ‘kukarangiza’.

Ukweli ni kwamba mwili wako hauhitaji sana aina hiyo ya vyakula, bali unahitaji zaidi mboga za majani, matunda na nafaka. Hivyo kama una matatizo ya kiafya usifikiri hali hiyo imekuja tu yenyewe, la hasha, bali imekuja baada ya mwili wako kukosa kile inachokihitaji ili kukulinda dhidi ya maradhi.

Na unapaswa kuelewa kwamba chakula unachokula leo, ndicho kinachoamua hali yako ya kiafya kesho, au matatizo ya kiafya uliyonayo leo, ni matokeo ya ulaji wako wa jana na juzi. Ulaji sahihi unatakiwa kufuatwa na kila mtu, ili kuimarisha kinga ya mwili ambayo kazi yake ni kupambana na magonjwa au matatizo mengine ya kiafya bila wewe kutumia dawa.

Mwili unapokosa virutubisho inavyovihitaji, kinga ya mwili (Body Immunity System) hupungua na kuisha kabisa na inapoisha mwili huwa wazi kushambuliwa na ugonjwa wowote utakaoingia kwa wakati huo. Ni vyema tukaelewa kwamba hali mbaya ya kiafya tuliyonayo leo, ni matokeo ya ulaji mbaya wa jana.
Halikadhali, hali mbaya ya kiafya au maradhi yatakayotupata kesho, itakuwa ni matokeo ya ulaji vyakula usio sahihi tunaoufanya hivi sasa. Tunahitaji kupeana elimu ya kutosha kuhusu suala la lishe na tukielewa, naamini idadi kubwa ya watu wataishi maisha marefu bila kusumbuliwa na magonjwa hatari.
GPL.

No comments: