ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 26, 2013

Wateja Vodacom wataka huduma mpya

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa
Kampuni ya Vodacom, Kelvin Twissa
Wateja wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania wameomba kuongezewa muda wa huduma mpya ya ‘Cheka Nao,’ ambayo inawawezesha wateja wa mtandao huo kupiga simu kwenda mitandao mingine kwa gharama nafuu huduma ambayo kwa sasa inapatikana kwa saa 12. Wakitoa maoni katika nyakati tofauti wateja wa kampuni hiyo pamoja na mambo mengine, walisema kuwa ingawa huduma hiyo imepunguza gharama za kupiga simu kwa kiasi kikubwa kutoka mtandao huo kwenda mitandao mingine ni vyema huduma hiyo ikaongezewa muda zaidi ili kuendelea kunufaisha watu wengi.

Wateja hao walisema kuwa ni wakati mwafaka sasa wa gharama za simu kupungua zaidi ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano kwa Watanzania walio wengi ambao muda mwingine wanaweza kushindwa kuwasiliana na watu wengine kutokana na gharama kubwa ya kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine.

Mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam, Mohamed Kazimoto, alisema: “Mawasiliano yamekuwa na umuhimu mkubwa baina ya mtu mmoja na mwingine hasa katika maendeleo ya taifa zima kwa ujumla tutakapo punguza gharama za upigaji simu kwa kiasi kikubwa tutaweza kuchangia uchumi wa taifa letu.”

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Kampuni hiyo, Kelvin Twissa, alisema kwa sasa wateja wa mtandao huo hawana haja ya kubadili kadi zao za simu ili kuwasiliana na mtandao mwingine kwani huduma ya Cheka Nao imekuwa rahisi zaidi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: