ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 18, 2013

Hukumu ya Ponda na wenzake leo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini iliwaona wana kesi ya kujibu katika mashtaka yote matano yanayowakabili. Katika moja ya mashtaka hayo, Sheikh Ponda na wenzake anadaiwa kula njama na wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni.

Awali, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa alitoa uamuzi kuwa kina Sheikh Ponda wana kesi ya kujibu baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa mashtaka, ikaonekana shauri hilo limetokana na kipande cha ardhi.

Kesi hiyo iliposikilizwa mara ya mwisho, Hakimu Nongwa alisema kuwa baada ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kubadilisha ardhi ya ekari nne iliyopo Chang’ombe Markazi na ekari 40 za Kampuni ya Agritanza Ltd zilizopo Kisarawe, kuna baadhi ya Waislamu hawakuridhika.

Mbali na mashtaka hayo, Ponda na mshitakiwa mwingine Sheikh Mukadam Abdallah Swalehe wanakabiliwa na shtaka la uchochezi wakidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka jana katika eneo la Chang’ombe Markazi, wakiwa viongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, waliwashawishi wafuasi wao kutenda makosa hayo.

Pia inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 21 na 16, mwaka jana katika eneo hilohilo, washtakiwa hao pasipo uhalali wowote, walijimilikisha ardhi ambayo ni mali inayomilikiwa kihalali na Kampuni ya Agritanza Ltd na kusababisha uvunjifu wa amani.

Kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka jana, huko Chang’ombe Markazi, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vifaa na malighafi mbalimbali za ujenzi, yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh59,650,000 mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd.
Mwananchi

No comments: