ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 25, 2013

Finland yatoa Sh60 bilioni kusambaza umeme Dar

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri anayeshughulika na masuala ya Ulaya na biashara za nje wa Finland, Alexander Stubb walizindua mradi wa Umeme ulioko katika jiji la Dar es Salaam jana, unaofadhiliwa na nchi hiyo. kushoto ni balozi wa nchi hiyo nchini Sinikka Antila

Dar es Salaam. Serikali ya Finland imeipatia msaada wa Sh60 bilioni Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kusambaza umeme katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuangalia mfumo wa umeme unaokwenda kwa wateja.
Akiweka jiwe la msingi la mradi huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kwa kipindi kirefu jiji hilo limekuwa na matatizo ya umeme, ikiwamo kukatika mara kwa mara.
Muhongo alisema matatizo hayo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara yanachangiwa na uchakavu wa miundombinu na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutakuwa ni mwarobaini wa kutibu tatizo hilo lililodumu kwa muda mrefu katika mkoa huu.
“Hii itakuwa ni neema kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambayo ilikuwa inasubiriwa siku nyingi,”alisisitiza kusema Profesa Muhongo.
Mradi huu utakuwa unaangalia mfumo mzima wa umeme ikiwamo kupunguza kasi inayokwenda moja kwa moja kwa wateja kwa namna moja ama nyingine, ambayo husababisha madhara ikiwamo kuunguza vitu,”alisema waziri huyo.
Aliongeza kuwa eneo la Kisutu ulipo mradi huo, ndiyo patakuwa stesheni ya kusambaza umeme na kuangalia mfumo mzima wa umeme unavyokwenda kwa wateja ili kuweza kukidhi mahitaji.
Waziri wa Biashara wa Mambo ya Nje wa Finland, Dk Alexander Stubb alisema Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania kwa sababu uhusiano wao unazidi kukua kila siku.
Alisema lengo la msaada huo ni kuboresha sekta ya miundombinu ya umeme na kuiboresha ili jamii ipate huduma hiyo kwa uhakika.
“Nimefarijika sana kuungana na waziri kuweka jiwe hili la msingi, tutahakikisha tatizo hili lililodumu muda mrefu linatatulika ndani ya miezi 24,”alisema Dk Stabb.
Mwanachi

No comments: