Thursday, May 16, 2013

HATA KAMA NI MKOROFI NI WAKO, MTIBU!-2

INAWEZEKANA likaonekana ni jambo la kawaida tu, pengine si kubwa na linalopaswa kujadiliwa kwa ukubwa huu lakini likitafakariwa kwa kina, itagundulika kuwa ni jambo muhimu sana kujadiliwa. Wanaume wengi wanateseka na namna ya kuishi na wanawake ambao kiasili ni wakorofi.

Hebu nikuulize wewe mwanaume ambaye umeshagundua kwamba mwanamke wako ni mkorofi, sababu hiyo inatosha kuwatenganisha? La hasha! Kipo kitu cha kufanya. Ipo tiba sahihi ya mwanamke mwenye asili ya ukorofi tena wa kuzaliwa.
Kama mtakumbuka, wiki iliyopita nilisema jambo la msingi ni kujihakikishia kwamba mwanamke huyo yupo moyoni mwako, suala la ukorofi ni dogo sana linaloweza kutibika kwa hakika. Kikubwa ni kujiona mwenye jukumu la kumbadilisha. Hebu tuendelee kujifunza marafiki zangu.
MSIKILIZE
Ukishatambua jukumu lako la kuhakikisha unakomesha tabia yake, anza na hatua ya kuwa msikilizaji zaidi wakati unapozungumza naye. Mara nyingi ukorofi wa mwanamke huanzia pale utakapotoa hoja, akatakiwa kujibu.
Wakati mwingine, inawezekana alitoa hoja, ukamjibu lakini akaingilia kati. Hapo sasa unatakiwa kuwa msikilizaji zaidi. Usijali amekudharau, mwache azungumze mpaka achoke.
Usikivu wako kupitiliza, utamgongea alamu kichwani mwake na huenda akaelewa kwamba ‘kelele’ zake hazikufurahishi. Vichwa ngumu wanaweza wasielewe hilo, hatua inayofuata itakusaidia sana.

ZUNGUMZA KWA MIFANO
Jenga hoja zako kwa mifano, mweleze hisia zako lakini fananisha na tukio lingine la watu wengine. Zungumza kwa staha na uoneshe umakini na uhakika wa kila kinachotoka kinywani mwako.
Kama ni wa kuelewa atakuelewa tu lakini kama ni wale ambao ujeuri na ubishi upo kwenye damu yao, mpe dawa nyingine hapa chini.

USIMBISHIE SANA
Hata kama unaona anakushushia heshima kiasi gani, anakujibu jeuri kwa kiwango gani, usibishane naye sana. Mweleze msimamo wako halafu mwache aendelee kujibishia mwenyewe.
Siku zote wewe utabaki kwenye heshima, maana kunyamaza kwako kutaonesha umedharau ‘pumba’ zake.

KUBALIANA NAYE KWA KILA KITU
Hatua hii ni muhimu sana na yenye nguvu kuliko zote. Kama umeshagundua tabia yake ni kubisha na kupinga kila kitu akiamini yeye yupo sahihi zaidi, usiumize kichwa, kubaliana naye kwa kila kitu.
Hata kama anazungumza ‘utumbo’ muunge mkono na umweleze kuwa ana busara sana ya kufikiria. Faida katika hatua hii ni kwamba, kama alitoa mawazo yake katika mambo ambayo baadaye yanatoa matokeo mabaya, atajifunza kitu.
Matokeo mabaya ndiyo yatakayomshtua na kumfanya ajione fikra zake hazikuwa sahihi. Endelea kumuunga mkono kwa kila unachoona hakifai na mwisho kabisa, matokeo yasiyotarajiwa yakijirudia mara kwa mara, atajirudi na kuanza kukusikiliza.

MWONESHE NJIA SASA
Huu ni wakati wako sasa wa kuonesha kuwa kwa muda wote huo ulikubaliana naye kwenye mambo yake yote ili muweze kufikia hapa, kumrudisha kwenye mstari. Mweleze madhara yote yaliyopatikana na umfundishe njia sahihi ya kuwasilisha hisia zake.
Mfundishe namna ya kuzungumza na wewe, umweleze wazi kuwa hupendi ‘kupigiwa kelele’ kwa kuwa unampenda na anapaswa kukuheshimu wewe kama kiongozi wake (mpe nukuu za maandiko matakatifu).
Tumia fursa hii vizuri sana kumwelewesha juu ya wajibu na haki zake kama mpenzi wako/mume. Kwa kutumia kauli nzuri, atakuelewa na hata kama tabia hii ni sugu na ya muda mrefu itakoma.

TENGENEZA MAELEWANO
Hii ni hatua muhimu zaidi, unatakiwa kujenga masikilizano ya pande zote mbili. Pamoja na kwamba ametambua kuwa unapaswa kuheshimiwa na kusikilizwa, usimfanye akaamini kwamba wewe ni mbabe na unataka kumburuza!
Mpe nafasi ya kutoa hisia zake na umsikilize vizuri. Mpe thamani na heshima ya mawazo yake. Kama unapingana naye uwe na hoja. Hapo sasa rafiki yangu utakuwa umejenga uhusiano mzuri ambao hauna migogoro. Suala la ujeuri, kiburi na ubishi litakuwa limefikia ukingoni!

ONESHA MAPENZI YAKO YOTE
Sasa baada ya kumaliza kazi hii ngumu, onesha mapenzi yako yote kwake. Kwamba unampenda na sababu ya ukorofi wake si tatizo sana kwa sababu ulikuwa unampenda yeye. Jambo hili litamsisimua na kumfanya awe makini zaidi hata kwenye mambo mengine katika uhusiano wenu.
Suala la kuheshimiana ni msingi mkubwa wa uhusiano wenu. Mpende na aone hilo kwa uyakinifu wa kutosha, kwamba unampenda sana na upendo ndiyo nguzo thabiti katika uhusiano wenu. Kumaliza suala la ukorofi si mwisho wa matatizo lakini angalau mengine yanaweza kuisha kwa sababu sasa mwanamke wako si mkorofi tena.
Mmenipata?
Mada imeisha, wiki ijayo tutakutana tena kwa mada nyingine, SI YA KUKOSA!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: