ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 26, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-7

WIKI iliyopita tulijifunza mambo kadhaa juu ya namna ambavyo ulimi unaweza kuwa sumu kubwa katika uhusiano wako. Leo tunaendelea pale tulipoishia.

Mfano; Kuna msomaji wangu anayeitwa Romeo, aliwahi kunisimulia stori yake ambayo nimeona itapendeza sana kama nawe nitakuhadithia japo kwa ufupi. Lengo langu ni kukuonesha namna ambavyo ulimi unavyoweza kusimama kama nyenzo imara ya ujenzi wa uhusiano, kama utautumia ipasavyo.
Romeo alinisimulia: “Huko nyuma niliwahi kuteswa na mapenzi, ingawa baadaye nikagundua nilikuwa najitesa mwenyewe. Nilijikuta nina wapenzi wawili lakini huwa sijilaumu kwa maana hiyo ilinisaidia kumtambua mpenzi wa kweli ambaye leo hii ndiye mke wangu wa ndoa na tuna watoto wawili.

“Mke wangu anaitwa Shantale, awali sikuamini kama ni mwanamke anayenifaa. Mwanamke ambaye niliwaza kwamba angekuwa wangu wa ndoa aliitwa Jannine. Nilimpenda sana na nikawa nampa kipaumbele kuliko Shantale ambaye kipindi chote alionesha utulivu na uvumilivu mkubwa.
“Niliponunua zawadi, moja kwa moja nilimpelekea Jannine. Shantale nilimuwazia tu kama mwanamke wa kupita. Niliona hawezi kukidhi matarajio yangu. Niliendelea kumbagua, wakati mwingine alinipigia simu sikupokea na SMS zake sikujibu. Siku tukikutana, aliniuliza maswali machache tena kwa upole na nilichomweleza alikielewa.

“Siku nyingine nilikuwa mkali sana kwake. Aliponipigia simu nilipokea na kumjibu kwa ukali. Kuna siku nilikuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa, kwa upendo kabisa, alininunulia shati, suriali, viatu, vilevile akanitengenezea keki nzuri sana, yote hiyo kuonesha namna anavyonijali.
“Basi nilimfanyia kitu kibaya sana, siku nzima nilimzimia simu, nikamchukua Jannine tukaenda hotelini na kufurahi pamoja siku nzima. Jannine pamoja na kutumia muda wangu wote nikiwa naye lakini hakuninunulia zawadi yoyote kunipongeza. Hata maneno happy birthday hakuniambia.

“Asubuhi nilitokea hotelini nikaenda kazini na Jannine naye alielekeza ofisini kwake. Jioni niliporudi nyumbani, nilikuwa zawadi zangu. Keki, nguo, viatu, ua pamoja na kadi nzuri kutoka kwa Shantale. Hiyo kidogo ikanifanya niwaze sana kuhusu upendo wa mwanamke huyo.

“Kipindi hicho Shantale hakuwa na kazi, ndiyo alikuwa amemaliza shahada yake ya chuo, akiwa anaendelea kutafuta ajira. Pamoja na kutokuwa na kazi aliweza kunifanyia mambo hayo. Kwa namna fulani ilinipa mwanga kwamba mwanamke huyo ananipenda sana.

“Jannine ana kazi lakini hakuonesha kujali chochote. Hata kunitamkia maneno ya kunitakia heri ya siku yangu ya kuzaliwa alishindwa. Hakunijali kwa zawadi na nilipomwambia habari ya kwenda kufurahia hotelini, alilipokea kwa moyo mmoja. Hapo nikaanza kuhisi kasoro ya upendo wa Jannine.

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

No comments: