Rafiki zangu, kwa wale ambao walianza kunisoma tangu mwaka 2006 katika safu hii na nyingine ya Let’s Talk About Love katika gazeti damu moja na hili, Ijumaa watakuwa mbali sana kiufahamu kuhusu uhusiano.
Najua nina wasomaji wengi wapya ambao wameongezeka hapa katikati. Sasa basi, inawezekana kwa namna moja au nyingine, nitakuwa nawaacha kutokana na mada ninazozungumzia hapa kwenye safu yetu.
Wakati mwingine huwa nakwenda mbali zaidi nikiwa na imani kwamba, nina wasomaji wenye ufahamu mkubwa kuhusu mambo ya uhusiano. Inawezekana wewe ni mmoja wao.
Kutokana na kugundua hilo, nitakuwa naendelea na mada za mbele kama kawaida kwa mada tatu kisha narudi nyuma kwa mada moja ili kwenda sawa na wengine ambao wamekuwa wadau wa kona hii kwa miaka ya karibuni.
Leo nitarudi nyuma kidogo, lakini nikiwa na imani somo hili litakuwa dawa kwa wengi katika uhusiano wao. Nazungumza kuhusu
KUJITAMBUA.
Wapo baadhi ya marafiki hawajitambui. Wapo kwenye uhusiano ilimradi siku zinakwenda wakiwa hawana malengo wala kufikiri juu ya mambo yajayo katika uhusiano wao. Hili ni tatizo.
TUONE MIFANO
Kwa kawaida, baada ya mada zangu kutoka gazetini, wapo baadhi ya wasomaji hunipigia simu na wengine kunitumia meseji wakitaka ushauri juu ya mambo mbalimbali yanayowasumbua katika mapenzi.
Baadhi yao, naweza kusema wanauliza maswali ya kawaida sana. Maswali ambayo kwa yeyote ANAYEJITAMBUA anaweza kupata jibu la moja kwa moja. Hebu tuone baadhi ya maswali niliyotumiwa wiki hii kisha tuendelee na mada yenyewe.
MSOMAJI WA KWANZA:
Kaka mimi nina mpenzi wangu, nimewahi kwenda kwao, nikimwambia aje kwetu ananipiga kalenda. Unanipa ushauri gani? (hajasema yeye ni jinsia gani).
MSOMAJI WA PILI:
Hey kaka Jose. Mimi ni kijana wa miaka 19, ni mwanachuo na napenda sana kusoma kwa bidii. Kuna wasichana wanne ambao nasoma nao darasa moja, wananitaka kimapenzi (kila mmoja kwa wakati wake).
Nimefikiria sana lakini nashindwa kuelewa cha kufanya. Naomba ushauri wako tafadhali maana nimechanganyikiwa sana katika hili.
MSOMAJI WA TATU:
Kaka Shaluwa naomba msaada wako. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20. Nina mpenzi wangu anafanya kazi katika kampuni moja maarufu. Hivi karibuni nilimsaliti kwa kutembea na rafiki yake wa karibu, akagundua.
Alivyoniuliza nilimkubalia na kumuomba msamaha, akakubali kunisamehe na kuendelea na mapenzi yetu. Kitu cha kushangaza kila nikikutana naye amekuwa akikumbushia makosa yangu.
Nifanyeje ili anisamehe na kusahau? Nakutegemea sana kaka yangu.
MSOMAJI WA NNE
Pole na kazi kaka Joseph. Naitwa (naficha jina lake). Nina mpenzi wangu wa muda mrefu sana, ambaye alinisaidia kunisomesha hadi chuo baada ya baba yangu kufariki. Tatizo huyo jamaa ana mke na amefunga ndoa ya kanisani.
Mimi ni Muislam yeye ni Mkristo. Hivi karibuni amejitokeza mwanaume mwingine ambaye hajaoa na amesema ana lengo la kufunga ndoa na mimi, lakini tatizo yeye ni Mkristo na anataka nibadili dini ili tufunge ndoa.
Yule jamaa wa mwanzo naye hataki kuachana na mimi ingawa ana mke wake na imani yake hairuhusu ndoa ya mke zaidi ya mmoja. Nifanyeje?
SASA PATA SOMO
Bila shaka kuna mambo ya msingi ambayo umejifunza katika maswali ya wasomaji hao. Kitu kikubwa cha msingi ambacho kipo hapo ni suala la kujitambua.
Nafasi yangu ni ndogo, wiki ijayo nitakuwa hapa katika mwendelezo wa mada hii, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandikia vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment