Dar es Salaam. Zaidi ya mgambo 30 kwa kushirikiana na polisi wametumia nguvu kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga, eneo la Ubungo Dar esSalaam.
Hatua hiyo ilisababisha taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.Operesheni hiyo ilifanyika kwa kushtukiza saa 12.00 jioni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Manispaa ya Kinondoni kuwaondoa machinga hao.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Stanley Athanas alisema mgambo hao walivamia na kuanza kubeba bidhaa zao mbalimbali walizokuwa wametundika katika eneo hilo.
“Tumeshtukia wamevamia na kuanza kutushambulia, ikabidi tukimbie ndipo wakaanza kuchukua nguo zikiwamo za kwangu zenye thamani ya Sh1.7 milioni,” alisema Athanas na kuongeza:
“Tulishakutana na uongozi wa halmashauri na tukawaomba eneo la maeneo ya hapa Ubungo, waturuhusu kufanya biashara lakini tulichoambiwa tusubiri.”
Akichangia kwa jazba, Thomas Mpandachalo alisema kama Serikali itaendelea kutumia njia hiyo, itasababisha vita isiyokwisha baina yao na mgambo.
“Tunaweza kuamua kupambana mpaka kieleweke, lakini hatutaki tufikie huko, ila tunaomba Serikali ijaribu kutumia busara watuite na kuzungumza, kwa nini iwe ni Machinga wa Ubungo tu siyo wale wa Mwenge, Kariakoo na Manzese ambao wanafanya biashara katikati ya barabara,” alisema Mpandachalo.
Vurugu hizo zilichukua takriban dakika 30 na kusababisha usumbufu mkubwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipita eneo hilo.
Akisimulia tukio lilivyokuwa, Hussein Mohamed alisema uamuzi huo siyo wa busara na kwamba, hautakuwa na matokeo mazuri kutafuta mwafaka wa wafanyabiashara wa Ubungo.
“Hawa wafanyabiashara ndogondogo wanaangalia pia ni sehemu yenye soko, haiwezekani leo hii uwapeleke eneo ambalo halina biashara, ni vizuri Serikali ikajaribu kukutana nao kwa mara nyingine kutafuta mwafaka,” alisema Hussein.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Camilius Wambura hazikufanikiwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment