ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 6, 2013

MAMBO 10 YA KUKUEPUSHA NA TABIA YA KUBADILI WAPENZI KILA KUKICHA!

WENGI wamejikuta wakiitwa wahuni kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na idadi kubwa ya wanaume au wanawake. Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya wapenzi siyo kigezo sahihi cha kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.

Wataalam hao wanataja safari ya kupata chaguo halisi la mwanaume/mwanamke wa maisha kuwa ndiyo inayowaponza wengi kiasi cha kujikuta wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na rundo la wapenzi.
Wanasema msichana/mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano kutoka kwa wazazi wake.

Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mwanaume/mwanamke asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana na huyo na kwenda kwa mwingine kujaribu bahati tena ya kupata penzi la kweli.

Zinatajwa zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa ni vichocheo vinavyowaangusha wengi kwenye mapenzi na wasiowafaa.Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ‘ujinga’, huwa hakatwi kiu ya penzi na mwanaume/mwanamke asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia uamuzi wa kujiingiza katika uhusiano mpya mara 2,3,4,5 na kujikuta wakiambulia wanaume/wanawake walewale wasio sahihi kwake.

Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Queen aliwahi kuniomba ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi huachia ngazi au kutemwa huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.

Nia ya swali lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya naye mapenzi? Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya naye mapenzi na wakati huo huo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa wamtakaye.
Najua kuna wanawake/wanaume wengi ambao hujiingiza katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa kitoto wa patapotea.
Lengo la mada hii ya leo ni kukuelekeza mambo ambayo ukiyazingatia yanaweza kukuepusha na ile tabia ya kubadili wanaume kila kukicha.

KWANZA
Ni ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza iliumtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewa na kuumizwa moyo bure.

PILI
Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.

TATU
Anza kumsaka huyo mtu wako kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kuridhika na mwili kusisimka.

NNE
Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.

Itaendelea wiki ijayo.

Mwananchi

No comments: