JAMHURI
YA MUUNGANO WA TAN ZANIA
WIZARA
YA FEDHA
MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA,
MHESHIMIWA
DKT. WILLIAM AGUSTAO MGIMWA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA
KWA
MWAKA 2013/14
DODOMA
6 Juni, 2013
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2013/14.
2.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru kwa namna ya pekee
Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake
Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa (Mbunge wa Mufindi Kaskazini) na Makamu wake
Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na
mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya
Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bajeti Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Mashariki)
pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao makini.
Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo
ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa
wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2012/13.
3.
Mheshimiwa
Spika, napenda pia
kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (Mb)
na Mheshimiwa Janeth Zebedayo Mbene (Mb). Aidha, napenda kutoa shukrani za
dhati kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wakiongozwa
na Katibu Mkuu, Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu Dkt.
Servacius B. Likwelile, Ndugu Elizabeth J. Nyambibo pamoja na aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu Ndugu Laston T. Msongole kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kusimamia
utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vile vile, napenda kuwashukuru Profesa Benno
Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali, chini ya
Wizara kwa michango yao katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
MAPITIO
YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13 NA
MALENGO YA MWAKA 2013/14
4.
Mheshimiwa
Spika, uandaaji,
utekelezaji na usimamizi wa Mpango na Bajeti ya Wizara unazingatia mambo
yafuatayo: Malengo ya maendeleo ya Milenia 2015; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
mwaka 2025; Awamu ya pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini
Tanzania (MKUKUTA II); Vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2011/12 - 2015/16; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2010; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Mwongozo wa Mpango
na Bajeti wa mwaka 2013/14-2015/16; pamoja na Programu ya Maboresho ya
Usimamizi wa Fedha za Umma - Public
Finance Management Reform Programme (PFMRP).
Usimamizi wa Uchumi
5.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2012, Pato la Taifa liliendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa
asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011, ikiwa ni zaidi ya lengo
la asilimia 6.8 mwaka 2012. Sekta ya
fedha ambayo inasimamiwa na Wizara ya Fedha ilichangia kikamilifu katika
shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa.
Katika mwaka 2012, sekta hii ya Fedha ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la
Taifa ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2011. Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na utekelezaji
madhubuti wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha.
6.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi hicho cha mapitio, Wizara pia ilitekeleza Sera ya Fedha na
bajeti kwa lengo la kupunguza ukwasi na mfumuko wa bei ambapo Benki Kuu ya
Tanzania iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko la fedha kama njia
mojawapo ya kudhibiti mfumuko huo.
Aidha, Benki ilipandisha kiwango cha chini cha akiba ya amana za
Serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40 pamoja na kupunguza
kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa mabenki kutoka
asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba 2012. Hatua zote zilisaidia kupunguza kiwango cha
mfumuko wa bei kutoka asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012 hadi asilimia 9.4 mwezi
Aprili 2013 pamoja na kusaidia kuimarika kwa kiwango cha ubadilishaji wa
shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.
Aidha, katika kuimarisha usimamizi na maendeleo ya sekta ya fedha,
Wizara imerekebisha muundo wake kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya
Fedha – Financial Sector Development
Division ambayo itasimamia uandaaji na utekelezaji wa sera za sekta ya
fedha na taasisi ndogo za fedha kama SACCOS na VICCOBA.
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali
7.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
iliendelea kusimamia uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya matumizi
ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Wizara imeratibu maboresho ya uandaaji wa bajeti ya 2013/14 kwa kuzingatia
mzunguko mpya wa bajeti. Aidha, Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha
2013/14, uliandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kusambazwa kwa
wakati. Vile vile, Wizara imeandaa na kusambaza nyaraka muhimu za bajeti ikiwa
ni pamoja na vitabu vya bajeti ya Serikali (volume
I, II, III na IV) kama vilivyopitishwa na Bunge na kitabu kinachotoa
maelezo ya Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati kwa mwaka 2012/13
- 2014/15. Kitabu hiki kinasaidia kuwajulisha wananchi na wadau wengine kuhusu
matokeo ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita pamoja na mwelekeo wa bajeti
ijayo kwa kipindi cha muda wa kati. Kadhalika, katika kuboresha uelewa wa
bajeti ya Serikali kwa wananchi, Kitabu cha Bajeti Toleo la Wananchi kwa mwaka
2012/13 kimeandaliwa na kusambazwa kwa wakati na kuwekwa kwenye tovuti ya
Wizara. Kitabu hiki kimesaidia kueleza bajeti kwa wananchi wa kawaida kwa lugha
rahisi na hivyo kuongeza uwazi katika kutoa taarifa muhimu za kibajeti.
8.
Mheshimiwa
Spika, katika kujenga uwezo wa kuandaa mipango na bajeti kwa
Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara
ilitekeleza yafuatayo: kufanya tathmini ya mchakato wa bajeti ya 2012/13 kuhusu
namna bajeti ilivyoandaliwa, changamoto zilizojitokeza na jinsi ya
kuzitatua; kuwajengea uwezo maofisa wa
bajeti wa Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuhusu kuandaa bajeti ya 2013/14, maboresho yaliyofanywa kwenye Mfumo wa Kugawa
Fedha za Bajeti - Strategic Budget
Allocation System (SBAS) na kuandaa bajeti inayozingatia utendaji -Performance Based Budgeting; na kuhuisha
Mwongozo wa kuandaa mipango na bajeti, ambao umezingatia mzunguko mpya wa
bajeti. Wizara imeendelea kusimamia malipo ya mishahara ya kila mwezi kwa ajili
ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi
na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Usimamizi wa Misaada na Mikopo
9.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeendelea kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ili kupata matokeo
yaliyotarajiwa. Mafunzo ya mfumo wa kutunza takwimu na kumbukumbu zingine za
misaada na mikopo yalitolewa kwa Maafisa kutoka Wizara 21 na Washirika wa
Maendeleo wapatao 20. Aidha, mapitio ya utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa Misaada
Tanzania (MPAMITA), 2006 – 2011 wenye lengo la kuimarisha usimamizi wa misaada,
yalifanyika.
10. Mheshimiwa Spika, katika
kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ya kibajeti, Wizara
iliandaa mkutano wa Mwaka wa Mapitio ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti - General Budget Support Annual Review meeting uliofanyika mwezi
Novemba 2012. Matokeo yaliyotokana na
Mkutano huo ni washirika wa Maendeleo kuipatia Serikali misaada ya
kibajeti yenye thamani ya sh. bilioni 1,163.13 fedha ambayo imepangwa kutumika
katika bajeti ya 2013/14. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Washirika wa
Maendeleo imeimarisha Mfumo wa Mapitio ya Matumizi ya Umma - Public Expenditure Review (PER) kwa kuanzisha Sekretarieti ya
pamoja yenye wajumbe wa upande wa Serikali na upande wa Washirika wa Maendeleo
pamoja na kuandaa Mpango Kazi wa mwaka.
11. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inatarajia kukamilisha Mfumo mpya wa Ushirikiano
wa Kimaendeleo -Development Cooperation
Framework , kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mfumo huu ndio
utakaoongoza usimamizi wa Misaada na Mikopo ya Kibajeti katika kutekeleza
mipango na programu za kitaifa za kukuza uchumi, kupunguza umaskini na kuleta
maendeleo. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya Mfumo wa Kutunza
Kumbukumbu za Misaada na Mikopo - Aid
Management Platform kwa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na Asasi za
Kiraia. Vile vile, Wizara itaendelea kuandaa mikutano ya kila mwaka ya Mapitio
ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti pamoja na Mapitio ya Matumizi ya Umma.
Uhimilivu wa Deni la Taifa
12. Mheshimiwa Spika, serikali inasimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia
Mkakati wa Taifa wa kusimamia Deni na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya
mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka
2012 Serikali ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa Deni la Taifa na
viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa
vinaonesha kuwa, deni la taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati.
Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt) kwa Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 18.9
ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50. Hii ni ishara kuwa kiwango cha
kukua kwa Deni la Taifa ni kidogo ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la
Taifa. Kiashiria kingine muhimu ni uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt) kwa thamani ya
mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi (export)
ni asilimia 56.2 ikilinganishwa na kiwango cha cha ukomo ambacho ni asilimia
200. Hii ni ishara nyingine inayotuhakikishia kuwa Deni la Taifa ni himilivu
kwa kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa ni ndogo ikilinganishwa na uwezo wan
chi kulipa deni hilo kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na humuma nje
ya nchi.
13. Mheshimiwa Spika, katika mkakati wa kuboresha mfumo wa usimamizi wa Deni
la Taifa serikali inakamilisha taratibu za kuanzishwa kwa Idara kamili ndani ya
Wizara ya Fedha pamoja na kupitia upya Mkakati wa taifa wa kusimamia madeni wa
mwaka 2002 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya
mwaka 1974 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004 na hivyo kuboresha muundo uliopo wa
usimamizi wa Deni la Taifa pamoja na sheria yake.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
14.
Mheshimiwa Spika, Katika
mwaka wa fedha 2012/13, Wizara ilitekeleza yafuatayo: kuboresha Mfumo wa Malipo
Serikalini – Integrated Financial
Management System(IFIMS) kutoka mfumo wa toleo la EPICOR 7.3.5 kwenda toleo la EPICOR
9.05 kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma;
kukamilisha zoezi la kutoa mafunzo ya kufanya malipo moja kwa moja benki kwa
njia ya kielektroniki -Tanzania
Inter-Bank Settlement System (TISS) kwa watumishi wa Hazina ndogo zote,
Bunge, Mikoa, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Idara ya Ushirika, ikiwa ni
maandalizi ya kuunganisha Taasisi hizo kwenye mtandao wa TISS ili kuboresha
usimamizi wa fedha za umma.
15.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Wahasibu
200 kutoka mikoa 25 walipata mafunzo juu ya usimamizi wa fedha za umma;
Wahasibu 425 kutoka wizara mbalimbali na Sekretarieti za Mikoa walipata mafunzo
juu ya Viwango vya kimataifa vya kiuhasibu vya kuandaa Hesabu za Serikali – International
Public Sector Accounting Standards
(IPSAS) na watumishi 120 kutoka katika Wizara na Taasisi walipata
mafunzo ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic Planning
kwa lengo la kujenga uwezo wa idara za
bajeti na Mipango katika kutekeleza maboresho ya usimamizi wa Fedha za umma.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – Public Finance Management Reform Programme
(PFMRP)
16. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea kutekeleza
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma-PFMRP ambapo Awamu ya Nne
ya Programu ilianza kutekelezwa Julai 2012 na itakamilika Juni 2017. Programu
ya PFMRP pamoja na mambo mengine, imewezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuanza kutumia akaunti sita za benki badala ya akaunti nyingi zilizokuwepo kwa
lengo la kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha za Umma. Aidha, Programu ilitoa
fedha za kuwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa Mpango Mkakati wake
wa Programu ya Usimamizi wa Fedha za Umma.
Vile vile, matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa programu yaliyofanywa
kama sehemu ya mapitio ya mwaka ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti yaliyofanyika
mwezi Novemba 2012 yalionesha kuwa utekelezaji wa Programu ulikuwa wa
kuridhisha, na uzingatiaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika kufanya ununuzi
ulifikia asilimia 74.
17. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutekeleza Mpango kazi
wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali Kuu kuandaa hesabu kwa Viwango vya
Kimataifa vya Uhasibu –International
Public Sector Accounting Standards (PSAS) accrual basis. Kwa mara ya
kwanza, hesabu za Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za
Mikoa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa
kutumia viwango hivyo. Aidha, Wizara imeandaa miongozo mbalimbali na kufanya
mikutano elekezi ili kuwajengea uwezo na uelewa wahasibu na wadau mbalimbali.
Katika kuimarisha usimamizi wa mapato na
matumizi ya Serikali pamoja na utoaji wa
taarifa zenye ubora na uwazi, Wizara imeendelea kusimamia na kuimarisha mtandao
wa malipo ya Serikali katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Hazina Ndogo pamoja
na Vikosi vya Jeshi.
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara itaendelea
kusimamia, kuimarisha na kudhibiti mapato na matumizi ya fedha za Serikali kwa
kuboresha mtandao wa malipo wa Serikali. Aidha, Wizara itatoa ushauri wa
kitaalamu na kuunganisha Hazina Ndogo na Sekretarieti za Mikoa ili kuziwezesha
kufanya malipo kwa njia ya ki-elektroniki (TISS)
kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Vile vile, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa
wahasibu wa Wizara, Mikoa, na Idara za Serikali ya kuandaa hesabu katika
viwango vya kimataifa –IPSAS Accrual basis na kuongeza uelewa
wa matumizi ya mtandao wa EPICOR 9.05.
Sera
ya Ununuzi wa Umma
19.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Sera ya
Ununuzi wa Umma, Wizara imetekeleza yafuatayo: kukamilisha rasimu ya Sera ya
Taifa ya Ununuzi wa Umma; kukamilisha rasimu ya Kanuni za Ununuzi wa Umma;
kuendelea kuhuisha taarifa za maofisa Ununuzi na Ugavi katika daftari ambapo
jumla ya Maofisa 989 wameingizwa katika daftari hilo. Aidha, Wizara imeendelea
na taratibu za kuanzisha kada ya Ununuzi Serikalini pamoja na kusimamia na
kuendeleza kada ya Ugavi nchini.
20.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2013/14, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuanza utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kufuatilia
na kufanya tathmini ya mfumo wa Ununuzi wa Umma; na kuendelea kuhakiki daftari
la taarifa za maafisa Ununuzi na Ugavi Serikalini.
Mpango wa Millenium
Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
21.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia MCA-T
imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya
Marekani kupitia shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC).
Utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea vizuri licha ya changamoto ambazo
zimeathiri kasi ya utekelezaji kama vile mvua nyingi kwa mikoa ya Ruvuma na
Rukwa na matatizo ya kiufundi. Ujenzi wa barabara ya Tanga- Horohoro
ulikamilika kwa kiwango cha lami na kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Oktoba 2012;
ujenzi wa barabara za ukanda wa Mtwara yaani Songea – Namtumbo na Peramiho –
Mbinga na ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kisiwa cha Mafia unaendelea. Aidha,
kazi ya kuweka lami katika barabara tano za Pemba ya Vijijini Kaskazini imeanza
na ujenzi wa barabara ya Tunduma – Sumbawanga ambao umegawanywa katika sehemu
tatu; Tunduma – Ikana, Ikana – Laela na Laela – Sumbawanga unaendelea.
22.
Mheshimiwa Spika, Miradi ya kupeleka umeme
Zanzibar kupitia chini ya bahari na ule wa ukarabati wa mtandao wa umeme kwa
mkoa wa Dodoma imekamilika. Utekelezaji wa miradi mingine ya ukarabati wa vituo
vya kupoozea umeme, ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mikoa ya Tanga, Morogoro,
Iringa, Mbeya, Mwanza na Kigoma, ikiwa ni pamoja na mradi wa umeme wa Jua Kigoma, inaendelea.
Aidha, miradi ya upanuzi wa mtambo wa maji Ruvu chini na ukarabati wa mfumo wa
maji kwa Manispaa ya Morogoro nayo pia inaendelea.
23.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji
wa kuridhisha wa miradi, katika kikao cha Bodi ya MCC kilichofanyika
mwezi Desemba 2012, kiliamua kuikubalia Tanzania kuidhinisha maandalizi ya
Mpango wa Pili wa miradi ya MCC (MCC Compact II). Serikali imeshaanza
maandalizi hayo baada ya kuunda
sekretarieti ya uratibu
Ukaguzi wa Ndani
24. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13,
Wizara imeandaa na kutoa miongozo ya Usimamizi wa vihatarishi katika Sekta ya
Umma pamoja na Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora wa Ukaguzi wa Ndani. Miongozo hii
ilizinduliwa mwezi Machi, 2013. Aidha, Wizara imetayarisha Mwongozo wa Ukaguzi
wa Ndani kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na unategemewa kuanza kutumika
rasmi mwezi Julai, 2013. Kadhalika, Wizara imekamilisha Mkataba wa Makubaliano
kati ya Wakaguzi wa Ndani na Wateja wake
na pia kutoa kanuni za maadili ya wakaguzi wa ndani. Miongozo hiyo ina
lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
iliendelea kutekeleza yafuatayo: kufanya ukaguzi wa hesabu za mafungu yote ya Wizara na Idara za
Serikali, Mikoa ya Tanzania Bara, Halmashauri, Mashirika ya Umma, Balozi na
Wakala wa Serikali; kukamilisha ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi -Value for Money Audit ambapo taarifa zote hizi zimewasilishwa hapa Bungeni
tarehe 11 Aprili 2013; ukaguzi wa Mashirika 50 ulikuwa unaendelea katika hatua
mbalimbali za ukaguzi; Ofisi imeendelea
kukiimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ufanisi kwa kutoa mafunzo kwa watumishi
saba na kukipatia vitendea kazi zaidi. Aidha, ofisi iliendelea kulipia mafunzo
ya muda mrefu kwa watumishi 53 waliopo katika vyuo mbalimbali na kugharamia
mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 400. Vile vile, ujenzi wa ofisi
unaendelea katika mikoa ya Dodoma na Rukwa na unatarajiwa kukamilika mwanzoni
mwa mwaka 2014.
26.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14,
Ofisi itatekeleza shughuli zifuatazo:
kuendelea kutekeleza mkakati wa kuwaondoa wakaguzi katika ofisi za
wakaguliwa; kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa
nchini ili kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa na kuendelea kufanya
mazungumzo na Msajili wa vyama vya siasa namna ya kutekeleza Sheria ya Gharama
za Uchaguzi; na kuziimarisha Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali – Public Accounts Committee (PAC) na Local Authorities Accounts Committee
(LAAC), Kamati ya Bajeti na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwa
kuzijengea uwezo.
27.
Mheshimiwa Spika, shughuli nyingine
zitakazotekelezwa ni pamoja na: kuhakiki matumizi ya fedha za Halmashauri; kushiriki
kikamilifu katika jukumu jipya la kukagua Taasisi za Umoja wa Mataifa ambapo
ofisi inaingia mwaka wa pili wa kuwepo kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa
Mataifa -UN Board of Auditors;
kufanya kaguzi sita za thamani ya fedha; kuendelea na uunganishaji wa ofisi za
Ukaguzi zilizoko mikoani na makao makuu kwa kutumia Mtandao Mpana -Wide Area Network (WAN); kuimarisha
ukaguzi wa kiutambuzi - Forensic audit;
na kuongeza idadi ya watumishi.
Sheria na Miswada ya Fedha
28.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2012/13, Wizara iliendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali ili
kuweka usimamizi mzuri wa kodi na fedha za umma. Baadhi ya sheria zilizofanyiwa
marekebisho ni sheria mbalimbali za kodi ambazo zilipitishwa kupitia Sheria ya
Fedha ya mwaka 2012 - The Finance Act, 2012 na Sheria ya Udhibiti wa
Fedha Haramu iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali iliyopitishwa na Mkutano wa Bunge wa mwezi Februari, 2013. Aidha,
marekebisho ya Mkataba wa Cotonou unaohusu ushirikiano baina ya nchi za Jumuiya
ya Ulaya, Afrika na Visiwa vya Caribbean ambapo Tanzania ni mwanachama,
yalipitishwa na Bunge kupitia Azimio la Bunge katika Mkutano wa mwezi Novemba,
2012.
29.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia
iliandaa kanuni mbalimbali ili kuwezesha usimamizi na utekelezaji wa Sheria za
Kifedha. Baadhi ya kanuni zilizotolewa ni zile za; kuanzisha credit
Reference Databank ya Utunzaji wa
Taarifa za Wateja wa Benki na Taasisi za Kifedha; Pamoja na Credit Reference
System. Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Kodi ya
Mapato; Usimamizi wa Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa abiria wa
ndege ambao sio raia wa Tanzania; Kanuni za Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;
na Kanuni za Sheria ya Uwekaji Stempu kwenye kazi za Wasanii.
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara itaendelea kukamilisha maandalizi ya kuwezesha kutungwa
kwa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani – Vale Added Tax (VAT), Sheria ya Utawala wa Kodi - Tax
Administration Act, Sheria ya Hoteli - Hotels
Tax Act, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mfuko
wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - Government
Employees Provident Fund (GEPF). Aidha, Wizara inatarajia kuwasilisha
Bungeni mapendekezo ya marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma,
pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ili kuihuisha kulingana na
mazingira ya sasa ya uchumi. Vile vile, wizara itaandaa kanuni mbalimbali
zitokanazo na sheria hizi ili kuwezesha utekelezaji wake.
Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
31. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utendaji wa Mashirika ya
Umma pamoja na Taasisi zake. Majukumu yaliyotekelezwa kwa kushirikiana na
Shirika Hodhi - Consolidated Holding
Corporation (CHC) ni pamoja na kuendelea na zoezi la urekebishaji wa
mashirika yaliyo na matatizo katika sekta za Usafirishaji, Madini, Mawasiliano,
Utalii na Fedha.
32. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepata ofisi katika jengo
la CHC Mtaa wa Samora na tayari watumishi wamehamia katika ofisi hiyo. Katika mwaka
wa fedha 2013/14, Wizara kupitia Ofisi
ya Msajili wa Hazina inatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia utendaji wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika
na Taasisi za Umma na kuboresha utawala bora kwa kuingia Mikataba ya Utendaji -Performance Contracts na Bodi za
Mashirika ya Umma; kusimamia mikakati ya kurekebisha Mashirika ya Umma na
uperembaji wa Mashirika ya Umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha usimamizi wa
Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na mapato ya Serikali.
Mafao ya Wastaafu na Mirathi
33. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za pensheni, Wizara imeanza
utaratibu wa kulipa Pensheni kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya
vipindi vya miezi sita sita kuanzia Januari, 2012. Katika utaratibu huu,
Wastaafu wanalipwa Pensheni ya miezi miwili mapema - in advance badala ya miezi
mitano iliyokuwa inalipwa katika utaratibu wa awali. Pensheni inalipwa mwishoni
mwa miezi ya Julai, Oktoba, Januari na Aprili. Aidha, Wizara imeendelea na kazi
ya kuweka kumbukumbu za Wastaafu waliopo kwenye daftari la Pensheni la Hazina
kwenye Mfumo wa Kompyuta ujulikanao kwa jina la SAPERION kwa lengo la
kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Hadi kufikia mwezi Aprili 2013, kumbukumbu
za Wastaafu 106,030 ziliwekwa kwenye mfumo wa kompyuta. Zoezi hili litaendelea
kufanyika katika mwaka 2013/14 ili kukamilisha uhifadhi wa kumbukumbu za
Wastaafu wote wanaolipwa kupitia Hazina.
34. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli za
mifuko ya pensheni iliyo chini ya Wizara ya Fedha. Mifuko hiyo ni Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma
(PPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF).
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma - PSPF
35.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2013 Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma ulisajili wanachama 332,067.
Katika kipindi hicho, Mfuko pia ulikusanya jumla ya shilingi bilioni
446.12. Kati ya makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni
374.76 na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 71.36.
Matarajio ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 749.10 ifikapo mwisho wa mwaka
wa fedha 2012/13. Aidha, thamani ya Mfuko hadi tarehe 30 Aprili, 2013 ilifikia
shilingi bilioni 1,112.24 na unatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,226.59
mwezi Juni, 2013. Jumla ya shilingi bilioni 422.16 zilitumika kulipa mafao
ikiwa ni pamoja na mafao ya kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi sawa na
asilimia 93.21 ya lengo la mwaka. Vile
vile, ili kuongeza wigo wa wanachama, Mfuko umeanzisha mpango maalum wa kuchangia
kwa hiyari kwa watumishi wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/14, Mfuko unatarajia
kukusanya jumla ya shilingi bilioni 680.55, kati ya
makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 539.18, na mapato
yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 141.37. Aidha, thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,522.01. Mfuko unatarajia kulipa kiasi
cha shilingi bilioni 522.32 kwa ajili ya mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi, ambapo jumla ya wanachama wapatao
7,647 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria. Vile vile, Mfuko unatarajia
kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1,211.39 kwenye maeneo mbalimbali ya vitega
uchumi.
Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - GEPF
37. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2013 Mfuko umesajili jumla ya
wanachama 6,755 wakiwemo wananchi waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo
rasmi. Katika kipindi hicho michango ya wanachama ilifikia kiasi cha shilingi
bilioni 22.74 sawa na asilimia 64.60 ya malengo ya mwaka mzima. Mapato
yatokanayo na vitega uchumi yamefikia shilingi
bilioni 11.64 ambayo ni sawa na asilimia 72.75 ya malengo ya mwaka mzima
na thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 190.0 Machi, 2013.
Aidha, Mfuko umelipa mafao ya shilingi bilioni 7.13 hadi kufikia Machi, 2013 na
kufungua ofisi katika Manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala kwa lengo la
kusogeza huduma karibu na wananchi.
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Mfuko utaendelea na
jitihada zake za kuboresha huduma kwa wanachama, kutanua wigo wa wanachama,
kukuza mapato yatokanayo na uwekezaji na kusajili wanachama wengi zaidi kupitia
Mpango wa Hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni na wa lazima. Aidha, Mfuko
unatarajia kusajili jumla ya wanachama 16,500 na kukusanya michango yenye
thamani ya shilingi bilioni 40.50. Vile vile, mapato ya vitega uchumi
yataongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 19.24 na thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 227.
Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma - PPF
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Mfuko ulikusanya shilingi bilioni
229.1 kutokana na michango ya wanachama ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia
21.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 188.1 zilizokusanywa mwaka 2011. Ongezeko
hili lilitokana na waajiri kuzingatia sheria kwa kuleta michango kwa wakati na
uandikishaji wa wanachama wapya. Aidha, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka
180,049 mwaka 2011 hadi 203,981 mwaka 2012. Mfuko pia ulilipa mafao ya jumla ya
shilingi bilioni 99.4. Mafao hayo ya PPF yalijumuisha na mafao ya elimu ambayo
hulipwa kwa ajili ya kusomesha watoto wasiozidi wanne wa mwanachama aliyefariki
akiwa kazini. Mwaka 2012 mfuko ulisomesha watoto 1,333 kwa gharama ya shilingi
milioni 683 ikilinganishwa na watoto 1,392 waliosomeshwa mwaka 2011 kwa gharama
ya shilingi milioni 573. Watoto hawa husomeshwa kuanzia elimu ya chekechea hadi
kidato cha nne.
40. Mheshimiwa Spika, mapato yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kutoka
shilingi bilioni 91.4 mwaka 2011, hadi kufikia shilingi bilioni 105.5 kwa mwaka
2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.4. Aidha, thamani ya Mfuko kufikia
Desemba 2012, ilikuwa imeongezeka kufikia shilingi bilioni 1,089.8 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 21.8 ikilinganishwa na thamani ya Mfuko ya shilingi
bilioni 894.5 ilivyokuwa Desemba 2011.
41. Mheshimiwa Spika, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni
281.7, kuandikisha wanachama wapya 72,000 kutoka sekta ya umma na binafsi,
na kukusanya shilingi bilioni 125.6
kutokana na uwekezaji ifikapo Desemba 2013. Aidha, thamani ya Mfuko inatarajiwa
kufikia shilingi bilioni 1,302.68.
42. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na changamoto kadhaa katika Mifuko ya
Hifadhi ya jamii ikiwemo: Wanachama kulalamikia kiwango kidogo cha mafao
kitolewacho na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pale wanapostaafu. Vile
vile, kuna suala la malimbikizo ya madeni yanayotokana na Mifuko kugharimia utekelezaji wa miradi ya Serikali. Aidha, katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto
hizo Serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii imepanga
kutathmini uwezo wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kupendekeza viwango vya
mafao; na kuhakikisha kwamba, mifuko hiyo inakuwa endelevu. Vile vile, Serikali inaendelea kulipa madeni
ya mifuko ya jamii kwa awamu na pia imeunda kamati ya kuchambua na kuhakiki
madeni mengine ya baadhi ya mifuko ili
kupendekeza njia endelevu ya kuyalipa.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania - TRA
43. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutekeleza
Mpango wa tatu wa Maboresho wa mwaka 2008/09 - 2012/13 ambao umekuwa msingi wa
kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Katika jitihada za
kuongeza mapato ya ndani, Wizara kupitia TRA imetekeleza yafuatayo: kuanzisha
mfumo wa kimtandao wa kuwasilisha ritani za kodi - tax returns; kufanya tathmini ya maeneo hatarishi katika Utawala wa
Sekta za Umma; kuweka mfumo wa taarifa wa RADDEX 2 na kutoa mafunzo kwa
watumiaji; kusambaza Mfumo wa Ki-elektroniki wa Ufuatiliaji Usafirishaji Mizigo
(Electronic Cargo Tracking System); na kuboresha mfumo wa utunzaji kumbukumbu
na Taarifa za Magari. Aidha, TRA imekamilisha uandaaji wa Awamu ya Nne ya
Mpango wa Maboresho (2013/14 - 2017/18) unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika
mwaka wa fedha 2013/14.
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa
kushirikiana na TRA itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato
ya ndani kwa kupanua wigo wa makusanyo na kuchukua hatua mbalimbali za kisera
na kiutawala katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi.
45. Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Mei 2013 kulitokea tatizo la mlundikano wa makonteina Bandarini Dar es
Salaam kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kuyaondoa. Kutokana na tatizo
hili Wizara ilikutana na wadau wote pamoja na wafanyabiashara ili kuondoa adha
hiyo. Katika kikao hicho Mamlaka ya Mapato ilielekezwa kushughulikia suala hilo
kulingana na sheria na taratibu ili wafanyabiashara waweze kulipia makonteina
yao na kuyaondoa bandarini. Tunapenda ieleweke kwamba katika tatizo hili hakuna
kodi yoyote iliyoongezwa kwa makonteina hayo ya wafanyabiashara na walitakiwa
kulipa kodi stahili.
Huduma
za Kibenki
Benki
Kuu ya Tanzania
46.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kwa kupitia Benki
Kuu imeendelea kutekeleza mabadiliko chanya katika sekta ya fedha ili kuhakikisha
kuwa sekta hiyo inachochea maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi. Mabadiliko
ya sekta ya fedha yamesababisha utendaji mzuri wa Taasisi za Fedha ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa
idadi ya mabenki kutoka benki 49 mwezi
Februari, 2012 mpaka benki 51 mwisho wa mwezi Februari 2013. Aidha,
rasilimali za mabenki zimeimarika zaidi na kufikia shilingi trilioni 17.3 mwezi
Februari ambapo mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imefikia shilingi trilioni
8.8.
47.
Mheshimiwa
Spika, katika kuendelea na jitihada za kuboresha upatikanaji
wa mikopo, Benki Kuu imeanzisha mfumo wa
ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za
wakopaji (Databank) na utaratibu wa utoaji wa taarifa za wakopaji kwa kutumia
kampuni binafsi (Credit Reference Bureaux). Mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa
kumbukumbu za wakopaji umeshaanza kufanya kazi na mabenki yameshaanza kupeleka
taarifa za wakopaji. Kampuni mbili za utoaji wa taarifa za wakopaji zimeshapewa
leseni na wapo katika maandalizi ya mwisho ili waanze kutoa huduma ya kutoa
taarifa hizo. Mfumo huu utaboresha upatikanaji wa mikopo ya muda wa kati na
muda mrefu.
48. Mheshimiwa
Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imetoa Mwongozo wa Huduma za Kibenki kwa
Kutumia Wakala wa Mwaka 2013 (Guidelines on Agent Banking for Banking
Institutions, 2013) ambao ulianza kutumika mwezi Februari, 2013. Kutolewa kwa
mwongozo huu ni sehemu ya mpango wa kuweka mazingira yatakayowezesha kupanua
wigo wa huduma za kibenki na kuhakikisha usalama wa benki mbalimbali
zitakazojihusisha na mfumo wa utoaji huduma za kibenki kwa kutumia mawakala.
Mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa huduma bora na nafuu za kibenki.
49.
Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Benki Kuu imeunda Kamati ya Kitaifa ya Uthabiti wa Mfumo wa Fedha
(Tanzania Financial Stability Forum) ili kusaidia kuimarisha ushirikiano na
kubadilishana taarifa kati ya wadhibiti wa sekta ya fedha kama msingi imara kwa
ajili ya kuhakikisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini na kupanua wigo wa
usimamizi katika mfumo wa fedha kutoka usimamizi unaolenga taasisi moja moja
kwenda usimamizi wa mfumo wa fedha unaolenga sekta nzima ya fedha kwa ujumla
wake. Aidha, taarifa inayoonesha hali
halisi ya uthabiti wa sekta ya fedha inatolewa kila baada ya miezi sita.
50. Mheshimiwa
Spika, Benki Kuu za
Afrika Mashariki zilikubaliana kutengeneza mfumo wa malipo utakaorahisisha
malipo kwa kutumia sarafu za nchi husika. Mfumo huu ujulikanao Kama East African Cross Border Payment System
- EAPS, umefikia hatua ya majaribio kupitia mifumo ya Malipo Makubwa (Real Time
Gross Settlement System – RTGS) ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Mategemeo
ni mfumo huu kuanza kutumika kwa nchi hizi tatu, ikiwa taratibu zote za
kujiunga na mfumo huu zitakuwa zimekamilika, mwezi Julai 2013. Aidha, Nchi za
Rwanda na Burundi zitakapokuwa tayari zitajiunga na mfumo huo. Kuanza kwa mfumo
huu wa malipo kutarahisisha malipo katika Jumuiya na kukuza shughuli za
kibiashara na uchumi.
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu itaandaa
mapendekezo ya kutunga Sheria ya kusimamia
mifumo ya malipo nchini (National Payment Systems Act). Aidha, Benki kuu itaendelea kuandaa sera za kifedha
na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile, Wizara kwa kushirikiana na Benki
Kuu itafanya tathmini ya mpango wa
utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maboresho ya Sekta ya Fedha
unaoishia Juni, 2013 na kuandaa mpango wa utekelezaji wa awamu ya tatu.
Kadhalika, Benki Kuu itahakikisha mwongozo wa kitaifa kuhusu elimu ya masuala
ya fedha (Financial Education Framework) unazingatiwa. Mwongozo huu unalenga
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kutumia huduma za fedha
katika shughuli zao za kila siku.
Benki
ya Maendeleo TIB - TIB Development Bank
52.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13
Benki ya Rasilimali (TIB) iliendelea na utekelezaji wa marekebisho ili kuwa
benki imara ya maendeleo tangu Novemba 2012 benki ilibadilisha jina na kuitwa
TIB Development Bank ili kuweka wazi dhana ya benki ya maendeleo. Aidha,
mchakato wa uanzishwaji wa benki ambayo kampuni tanzu inayojishughulisha na
shughuli za biashara (TIB Corporate Bank) ambapo usajili wake upo katika hatua
za mwisho. Mara taratibu zote zitakapokamilika, TIB itafanya kazi katika mfumo
wa makampuni mawili yanayotegemeana moja likijikita kwenye shughuli za
maendeleo (TIB Development Bank) na lingine kwenye shughuli za kibiashara (TIB
Corporate Bank). Benki hizi zitakamilisha muundo wake ifikapo mwezi Septemba,
2013.
53.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
2012/13, Benki ilifungua tawi mkoani
Mbeya na ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hii inafanya benki kuwa na
jumla ya matawi matano na
ofisi tatu za kanda. Aidha, hadi
kufikia Desemba 2012, Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni
242.9 ikilinganishwa na mikopo ya shilingi bilioni 181.7 Desemba 2011 sawa na
ongezeko la asilimia 74.8. Mikopo mingi ilitolewa kwenye sekta ya kilimo na
usindikaji wa mazao ya kilimo (mikopo hii ni tofauti na ile ya Dirisha la
kilimo). Vile vile, mtaji wa benki ulifikia shilingi bilioni 142.1 baada ya
Serikali kuongeza shilingi bilioni 40. Benki ilipata faida kabla ya kodi ya
shilingi bilioni 8.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 48 toka shilingi bilioni 5.8
zilizopatikana mwaka ulioishia Desemba 2011.
54. Mheshimiwa Spika,
Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo TIB liliendelea kutoa mikopo kwa
wakopaji mbalimbali kwa riba nafuu. Tangu kuanza kwa dirisha mwaka 2010 hadi
kufikia Desemba 2012, maombi yenye thamani ya shilingi bilioni 40.1
yaliidhinishwa ambapo shilingi bilioni 20.0 (asilimia 49.9) zilikopeshwa kwa
makampuni; shilingi bilioni 5.7 (asilimia 14.2) kwa taasisi ndogo za fedha
zinazokopesha wakopaji wadogo; na shilingi bilioni 14.4 (asilimia 35.9) kwa
vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) ambavyo pia vinafaidisha wakopaji wadogo.
Hii inamaanisha asilimia 50.1 ya mikopo imetolewa kwa wajasiriamali wadogo.
Aidha, kuanzia Julai, 2013 Dirisha la Kilimo lililopo TIB litahamishiwa katika
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
55.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba
2013, mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo TIB katika sekta mbalimbali
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 379.2 na faida kabla ya kodi inatarajiwa
kufikia shilingi bilioni 16.6.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo - TADB
56. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea na utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuanzisha Benki ya Maendeleo
ya Kilimo Tanzania – TADB. Lengo la kuanzisha benki hiyo ni kutoa mikopo ya
muda mfupi, wa kati na mrefu katika sekta ya kilimo inayojumuisha uvuvi na
mifugo. TADB ilisajiliwa BRELA chini ya Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 kwa jina la Tanzania Agricultural Development Bank Limited
(TADB Ltd). Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 90.0 kati ya lengo la
shilingi bilioni 100 kimeshatolewa kama kianzio cha Mtaji. Vile vile, Muundo wa benki ya kilimo na
majukumu ya wafanyakazi katika nafasi mbalimbali umeandaliwa. Mwenyeketi na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wameteuliwa na ajira za maafisa waandamizi wa
benki hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Katika
mwaka 2013/14, shilingi bilioni 10 zimetengwa ili kukamilisha lengo la mtaji wa
kuanzia wa shilingi bilioni 100.
Twiga
Bancorp
57.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi kinachoishia Desemba 2012 Taasisi iliendelea kupanua
shughuli zake kwa kufungua tawi moja mkoani Dodoma na kuifanya taasisi kuwa na
matawi matano. Katika kipindi hicho, amana za wateja zilifikia shilingi bilioni
58.41 ikilinganishwa na shilingi bilioni 54.2 Desemba 2011 sawa na ongezeko la
asilimia 7.8. Aidha, mikopo iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 39.43
ikilinganishwa na shilingi bilioni 35.9 kwa mwaka ulioishia Desemba 2011 sawa
na ongezeko la asilimia 9.8. Vile vile, Taasisi iliwekeza shilingi bilioni 4.7
kwenye Dhamana za Serikali na Amana katika Benki zingine ikilinganishwa na
shilingi bilioni 19.0 zilizowekezwa katika kipindi kama hicho mwaka 2011.
58.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka unaoishia
Desemba, 2013, amana za wateja zinatarajiwa kufikia shilingi bilioni 73.25
kutoka shilingi bilioni 58.41 za Desemba, 2012; mapato kutokana na shughuli
mbalimbali za kibiashara yanatarajia kufikia shilingi bilioni 12.66
ikilinganishwa na shilingi bilioni 9.56 zilizokusanywa Desemba, 2012; na mtaji
ghafi wa Benki (Owners’ Equity) unatarajiwa kukua kutoka shilingi bilioni 5.81
hadi shilingi bilioni 7.24 ifikapo
Desemba 2013. Aidha, thamani ya mikopo kwa wateja inatarajia kufikia
shilingi bilioni 49.10 na uwekezaji katika Dhamana za Serikali na Amana za Muda
Maalum kwenye mabenki unatarajia kufikia shilingi bilioni 16.80. Vile vile,
Taasisi inatarajia kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 0.48.
Benki
ya Posta - TPB
59.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
2012 Benki ilianzisha huduma mpya ya Platinum Account inayolenga vijana
walio katika Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine za elimu ya juu. Manufaa ya huduma hii ni kuwawezesha vijana
kujiwekea akiba na kupitishia mikopo ya elimu. Aidha, Benki iliendelea kupanua
mtandao wake kwa kufungua matawi madogo
katika ngazi ya Wilaya katika vituo vya Shirika la Posta. Vile vile,
Benki ilianzisha huduma ya POPOTE Quick Account, inayomuwezesha mteja
kupata huduma za benki mahali popote kupitia simu ya mkononi kwa lengo la
kuwafikia Wananchi walio wengi wanaoishi vijijini.
60.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, amana
za wateja zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 120.92 mwaka 2011 hadi kufikia
shilingi bilioni 144.56 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.4. Aidha, benki ilitoa
mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 103.34 ikilingalishwa na shilingi
bilioni 66.75 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 54.83. Vile vile,
uwekezaji katika vitega uchumi vya Benki ya Posta umeongezeka kutoka shilingi
bilioni 117.67 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 146.96, ikiwa ni
ongezeko la asilimia 24.9. Kadhalika, Benki imepata faida baada ya kodi ya
shilingi bilioni 3.59 ikilinganishwa na shilingi bilioni 2.58 mwaka 2011 ikiwa
ni ongezeko la asilimia 39.4. Katika mwaka 2012/13, Serikali iliiongezea Benki ya
Posta mtaji wa shilingi bilioni 1.5 na kufanya mtaji wa benki kuwa jumla ya
shilingi bilioni 16.82.
61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, benki itaendelea na mkakati wake wa
kuimarisha huduma zitolewazo kupitia Shirika la Posta kwa kukarabati na kuunganisha
katika mtandao wa benki vituo 10 vya Posta vilivyoko Temeke, Tunduma, Kahama,
Geita, Masasi, Peramiho, Njombe, Kyela, Simiyu na Kasulu hivyo kuvipa uwezo wa
kutoa huduma za haraka. Vituo hivi vitakuwa ni matawi madogo na hivyo kufanya
benki kufikisha jumla ya matawi 23. Aidha, benki itafunga vifaa vya ki-elektroniki katika
vituo vya mauzo. Vile vile, Benki inatarajia kupanua wigo wa mikopo kwa kuingia
mikataba na Sekretarieti za Mkoa na Jeshi la Kujenga Taifa, na kuongeza kipindi
cha marejesho kutoka miaka mitatu hadi minne. Kadhalika, Benki inatarajia
kupata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 5.11 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 25.5 ikilinganishwa na faida ya shilingi bilioni 4.07 iliyopatikana
mwaka 2012.
Taasisi
za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
62. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea kusimamia taasisi za kitaalam na huduma nyinginezo ambazo ziko
chini ya Wizara ya Fedha ambazo ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS; Bodi ya
Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi – NBAA; Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi –
PSPTB; na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha. Aidha, huduma nyingine
zinajumuisha: Usimamizi wa shughuli za Bima; Masoko ya Mitaji na Dhamana; na huduma
za dhamana ya uwekezaji.
Taasisi
za Mafunzo
63. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2012/13, Wizara imeendelea kusimamia taasisi za mafunzo zilizo
chini yake. Taasisi hizo ni Chuo
cha Usimamizi wa Fedha – IFM, Taasisi ya Uhasibu Arusha – IAA, Taasisi ya
Uhasibu Tanzania – TIA Chuo cha Mipango
na Maendeleo Vijijini – IRDP, na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC
.
CHANGAMOTO
64. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na
changamoto kadhaa zikiwemo zifuatazo:-
i)
Kudhibiti matumizi ya fedha
za umma sambamba na kuongeza mapato ya Serikali;
ii)
Kuzingatia
kanuni na taratibu zilizoainishwa kwenye Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) na upatikanaji wa fedha kutoka kwa
wafadhili wa nje;
iii)
Kuwa na Sera ya Mali
ya Serikali.
iv)
Kufikiwa kwa malengo
ya ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi;
v)
Kuwepo kwa mahitaji
makubwa ya fedha nje ya bajeti;
vi)
Kuwepo kwa mchakato
mrefu wa upatikanaji wa fedha za kugharamia Miradi ya Maendeleo hasa mikopo ya
kibiashara (non-conscessional borrowing); na
vii) Kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani katika
mafungu mbalimbali ambayo yameshindwa kuingizwa kwenye viwango vya bajeti.
65.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto
hizo, Wizara itachukua hatua kupitia mipango na bajeti zake ili kuhakikisha
kuwa changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi katika mwaka 2013/14 na kuendelea.
Hatua za ufumbuzi wa changamoto hizi zitaelezwa katika hotuba ya bajeti ya
Serikali itakayowasilishwa Juni 13,
2013.
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, majukumu ya Wizara
yalitekelezwa katika mafungu sita ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 -
Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni
la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja
ya Fedha. Aidha, Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, linaombewa fedha Bungeni
na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sheria.
Fungu
50 – Wizara ya Fedha
67. Mheshimiwa Spika, Wizara ilitarajia
kupata shilingi bilioni 124.42 kutoka
vyanzo mbalimbali vya mapato
yasiyo ya kodi kupitia Fungu 50. Vyanzo hivyo ni pamoja na mauzo ya
mali, uuzaji wa nyaraka za zabuni na mapato kutoka katika Mashirika ya Umma na
Taasisi za Serikali yakiwemo Gawio, Michango na Marejesho ya mikopo.
Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, makusanyo
yalifikia shilingi bilioni 37.27 sawa na asilimia 29.97 ya lengo. Makusanyo
zaidi yanatarajiwa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha baada ya Mashirika
mengi kuandaa hesabu za mwaka na ukaguzi
wa hesabu hizo kukamilishwa.
68. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 50 kwa mwaka 2012/13
yalikuwa shilingi bilioni 98.41 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 546.51 kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 70.32 sawa na asilimia 71.46 ya makadirio na matumizi ya
maendeleo yalifikia shilingi bilioni 311.28 sawa na asilimia 56.96 ya
makadirio.
Fungu
23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
69. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 23 kwa mwaka 2012/13
yalikuwa shilingi bilioni 75.12 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 6.12 kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 49.34 sawa na asilimia 65.67 ya makadirio, na matumizi ya
maendeleo yalifikia shilingi bilioni 1.29 sawa na asilimia 21.05 ya makadirio.
Fungu
22 - Deni la Taifa
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 makadirio ya
matumizi ya Fungu 22 yalikuwa shilingi bilioni 2,735.91. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013 matumizi ya fungu
hili yalifikia shilingi bilioni 2,226.70 sawa na asilimia 81.39 ya makadirio.
Fungu
21- HAZINA
71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiria kukusanya mapato ya shilingi bilioni 8,070.
Hadi kufikia Aprili, 2013, TRA ilikusanya shilingi bilioni 6,580 sawa na
asilimia 97.84 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 6,725 katika kipindi
hicho.
72. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 21 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi bilioni 725.57 kwa ajili ya matumizi
ya kawaida na shilingi bilioni 101.95 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Aidha, kiasi cha Shilingi
bilioni 50.66 kilifanyiwa uhamisho kuongezea katika zoezi la Sensa ya Watu na
Makazi na kufanya makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka 2012/13 kuwa
shilingi bilioni 152.61. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida
yalifikia shilingi bilioni 516.61 sawa na asilimia 71.2 ya makadirio, na
matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 131.95 sawa na asilimia 86.46
ya makadirio.
Fungu 13 – Kitengo
cha Udhibiti wa Fedha Haramu
73. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 13 kwa mwaka 2012/13
yalikuwa shilingi bilioni 2.16 kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 0.26 kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 1.01 sawa na asilimia 46.62 ya makadirio, na matumizi ya
maendeleo yalifikia shilingi bilioni 0.04 sawa na asilimia 14.72 ya makadirio.
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
74. Mheshimiwa Spika, makadirio ya
matumizi ya kawaida kwa Fungu hili yalikuwa shillingi bilioni 1.99, hadi kufikia Aprili, 2013 matumizi
yalifikia shilingi bilioni 1.33 sawa na asilimia 66.83 ya makadirio.
Fungu
45- Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
75. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 45 kwa mwaka 2012/13
yalikuwa shilingi bilioni 55.02 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 9.62 kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 39.51 sawa na asilimia 71.81 ya makadirio, na matumizi ya
maendeleo yalifikia shilingi bilioni 3.18 sawa na asilimia 33.0 ya makadirio.
MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14
76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, majukumu ya Wizara
yatatekelezwa katika mafungu saba ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 -
Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni
la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya
Pamoja ya Fedha na Fungu 7- Ofisi ya
Msajili wa Hazina. Aidha, Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
ambayo inajitegemea litaendelea kuombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa
mujibu wa Sheria.
Mapato
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ya Fedha
inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi 2,718,102,000
(bilioni 2.72) kupitia Fungu 50 -
Wizara ya Fedha na shilingi 124,013,512,000
(bilioni 124.01) kupitia Fungu
7- Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Maombi ya Fedha
78. Mheshimiwa Spika,
baada ya kueleza kwa kina utekelezaji wa majukumu na kazi za Wizara kwa mwaka
2012/13 na mpango na malengo ya bajeti kwa mwaka 2013/14, sasa napenda kuwasilisha rasmi mapendekezo ya
maombi ya fedha kwa mwaka 2013/14 kwa ajili ya matumizi ya Fungu 50, 23, 22,
21, 13, 10, 7, na 45 kama ifuatavyo:-
Fungu 50 – Wizara ya Fedha
79. Mheshimiwa Spika,
katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi
ya kawaida Shilingi 53,011,091,000
(bilioni 53.01). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 4,564,609,000 (bilioni 4.56) na matumizi mengineyo shilingi 48,446,482,000 (bilioni 48.45).
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi
233,669,169,000 (bilioni 233.67). Kati ya hizo:-
(i) Fedha za Ndani - Shilingi 10,200,000,000 (bilioni
10.20).
(ii) Fedha za Nje - Shilingi 223,469,169,000 (bilioni 223.47).
Fungu
23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali:
80. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida
- Shilingi 80,831,672,000 (bilioni 80.83). Kati ya hizo Mishahara
shilingi 4,434,410,000 (bilioni 4.43) na matumizi mengineyo
shilingi 76,397,262,000 (bilioni 76.40).
(b)
Miradi ya Maendeleo – Shilingi 4,755,547,000
(bilioni
4.76) Kati ya
hizo:-
(i)
Fedha
za Ndani -Shilingi 400,000,000 (bilioni
0.40).
(ii) Fedha za
Nje -Shilingi 4,355,547,000 (bilioni
4.36).
Fungu 22- Deni la Taifa
81.
Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba
kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 3,319,017,772,000 (bilioni 3,319.02). Kati
ya hizo Mishahara ni shilingi 6,311,772,000 (bilioni 6.31) na
matumizi mengineyo ni shilingi
3,312,706,000,000 (bilioni 3,312.71).
Fungu
21 - HAZINA:
82. Mheshimiwa Spika,
katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi
ya kawaida Shilingi 1,378,142,566,000
(bilioni 1,378.14). Kati ya hizo
mishahara ni shilingi 2,632,424,000
(bilioni 2.63) na matumizi mengineyo shilingi 1,375,510,142,000 (bilioni 1,375.51) ambazo ni kwa ajili ya
matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili, nyongeza ya mishahara
ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.
(b)
Miradi
ya maendeleo ni shilingi 38,190,162,000
(bilioni 38.19). Kati ya hizo:-
(i)
Fedha za Ndani-
Shilingi 7,893,000,000 (bilioni 7.89)
(ii)
Fedha za Nje-
Shilingi 30,297,162,000 (bilioni 30.30)
Fungu 13 – Kitengo
cha Udhibiti wa Fedha Haramu:
83. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya
kawaida - Shilingi 1,944,790,000 (bilioni 1.94).
(b) Miradi
ya Maendeleo, fedha za nje Shilingi 399,985,000 (bilioni 0.39).
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
84. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,064,424,000 (bilioni 2.06)
kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi 362,771,000 (bilioni 0.36) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 1,701,653,000 (bilioni 1.70) ni matumizi mengineyo.
Fungu 7 – Ofisi
ya Msajili wa Hazina:
85. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida
- Shilingi 38,088,142,000 (bilioni
38.08). Kati ya hizo shilingi 303,192,000 (bilioni 0.30) ni
kwa ajili ya mishahara na shilingi
37,784,950,000 (bilioni 37.78) ni matumizi
mengineyo.
(b)
Miradi
ya Maendeleo - Shilingi 1,665,300,000 (bilioni 1.67) Kati ya hizo:-
(i)
Fedha
za Ndani -Shilingi 600,000,000 (bilioni
0.60).
(ii) Fedha za
Nje -Shilingi 1,065,300,000 (bilioni
1.07).
Fungu
45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
86. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi
ya kawaida shilingi 57,406,414,000
(bilioni 57.40). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 6,692,935,000
(bilioni 6.69)
na matumizi mengineyo shilingi 50,713,479,000
(bilioni 50.71).
(b) Miradi
ya maendeleo shilingi 21,449,100,000 (bilioni 21.45), kati ya hizo:-
(i)
Fedha za ndani
shilingi 15,250,000,000 (bilioni 15.25).
(ii)
Fedha za nje
shilingi 6,199,100,000 (bilioni 6.20).
HITIMISHO
87. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba ya bajeti ya Wizara inapatikana katika
tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz) Aidha, naomba hotuba kama ilivyo
kwenye kitabu iingizwe kwenye “Hansard”.
88. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment