Dar es Salaam. Mtu anayetaka kuwania ubunge kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, atapaswa kuwa na umri wa kuanzia miaka 25, ikiwa rasimu ya Katiba Mpya itapitishwa.
Hilo ni moja ya mapendekezo yaliyotangazwa Jumatatu iliyopita na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba. Katiba ya sasa inaruhusu mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 21 kugombea nafasi hiyo.
Rasimu ya Katiba Mpya katika ibara yake ya 117 inazungumzia masuala ya sifa za mtu kuchaguliwa kuwa mbunge. Hata hivyo, haijaweka ukomo wa umri wa mtu kuwania nafasi hiyo.
Kuhusu elimu, rasimu hiyo inataka mgombea wa kuwa na elimu ya kuanzia kidato cha nne wakati katiba ya sasa, haitaji kiwango cha elimu na badala yake, inamtaka mgombea kujua kusoma na kuandika katika lugha za Kiswahili au Kiingereza.
Sifa za kugombea ubunge ambazo zimeongezwa ni pamoja na mgombea kuwa mwadilifu, anayeheshimu haki za binadamu na asiyedharau wala kubagua watu kwa misingi ya kabila, dini, jinsi, maumbile au hali zao katika jamii.
Ibara ya 122 ya rasimu hiyo inazungumzia vitu vinavyoweza kuwafanya wananchi kmng’oa mbunge.
Inasema wananchi watakuwa na haki ya kumwondoa mbunge wao madarakani kama atafanya mambo mbalimbali ikiwamo kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero ya wapigakura.
Rasimu hiyo pia inasema mbunge ataondolewa ikiwa anaunga sera zinapingana na masilahi ya wapigakura au masilahi ya taifa.
Pia mbunge akiacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka katika eneo la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila ya sababu za msingi, wananchi wanaweza kumwondoa katika nafasi hiyo.
Sababu nyingine, ni mbunge kutohudhuria vikao vitatu vya Bunge mfululizo bila ruhusa ya spika. Mbunge akiajiriwa au kufanya kazi nyingine na kuacha kuzingatia kazi yake ya kuonana na wapiga kura wake, anaweza kuondolewa na wananchi.
Maoni ya wabunge
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema rasimu hiyo ya katiba ni nzuri na kwamba itawafanya wabunge wawajibike kwenye majimbo yao.
Alisema kifungu hicho kitawafanya wabunge kufanya kazi za umma badala ya kutumia muda mwingi kujishughulisha na kazi binafsi.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali, alisema ingawa hajaisoma kwa umakini rasimu hiyo lakini anaunga mkono mbunge kuondolewa na wananchi kama atakuwa ameishi nje ya jimbo lake kwa zaidi ya miezi sita bila kutoa taarifa.
No comments:
Post a Comment