Moja ya kasoro ambayo inaweza kukusababishia ukawa kwenye maisha ya mateso kwenye uhusiano wako ni kutaka kuoneka upo juu kila siku. Lazima ukubali kujishusha wakati mwingine kwa lengo la kupata suluhu hasa pale unapoona kwamba makosa yapo upande wako.
Unapogoma kujishusha ilhali kila kitu kipo wazi kwamba wewe ni mkosefu, kwanza utamuumiza mwenzi wako. Hapohapo utamfanya naye siku zijazo aanze kuwa mgumu kukubali makosa yake. Nyakati hizo zitakapowadia, maumivu yatakuwa upande wako. Hebu jikosoe, siyo ujinga kujishusha. Fanya hivyo uone faida zake.
Mpe thamani yake. Ona umuhimu wake kisha chukulia uzito unaostahili pale mwenzi wako anapojishusha. Elewa kwamba wakati mwenzi wako anaponyenyekea kwako, yupo anayetamani kupata mpenzi atakayeweza kumtamkia neno nakupenda japo mara moja kwa mwezi.
Maana, aliyenaye ni majanga mtindo mmoja. Mapenzi hayana maelewano. Kila siku malumbano na kukomoana. Mtu anakosea lakini hataki kusema samahani. Anayemwita mwenzi wake wa maisha ni mbabe afadhali ya Mobutu. Mazingira yanamfanya kila siku atamani kutoka ila anashindwa jinsi ya kuanza.
Sasa, inapotokea huyo mtu anakuona wewe unampuuza mwenzi wako anayejishusha kwako, anakuona kama mchezea bahati. Ukweli ni kwamba binadamu wana sifa zinazofanana kwa nje lakini ndani yetu, kila mmoja ana vitabia vyake. Ndiyo maana wewe unaweza kuwa mwepesi kusema samahani lakini mwenzio hilo haliwezekani hata ukimuwekea kisu shingoni.
Mwenzio kumwambia mwenzi wako kuwa anampenda ni kama utaratibu aliojiwekea kwamba kabla hajalala lazima amtamkie neno hilo, kadhalika wakati wanaagana nyakati za kwenda kwenye mihangaiko ya kimaisha, vilevile kila wanapoongea kwenye simu, hawamalizi mazungumzo bila kumwambia anavyompenda.
Siyo kumwelewa anapojishusha tu, unapaswa pia kujishusha pale inapohitajika. Fanya mazoezi ya kusema samahani na hakikisha unajizoesha mpaka uelewe thamani ya msamaha. Uelewe thamani hiyo katika vipengele viwili mahususi, unapotamkiwa uwe mwepesi kuheshimu, kwani thamani yake ni kubwa, unapokosea tamka mapema ili kumwonesha mwenzi wako namna unavyomthamini kwa kumwambia neno lenye thamani.
Ukweli ni kwamba kuna njia nyingi zinazoweza kukufanya ujione dhalili kwenye uhusiano wako; mathalan, pale unapowasilisha hisia zako za kweli jinsi unavyompenda mwenzi wako. Hapo ni lazima uwe umejishusha, kwani unakuwa umemuweka juu mwenzi wako kwamba yeye ana thamani kubwa kwenye maisha yako.
Fikiria kuwa unamwambia kuwa yeye ni kila kitu kwako. Hapo unakuwa umejishusha sana na kumdhihirishia kuwa bila yeye maisha yako yatakuwa na pengo kubwa. Ikiwa mwenzi wako ni mwelewa, naye atatafuta neno lenye thamani inayokaribiana na hilo kisha atakwambia. Mfano; atakwambia wewe ni dunia yake.
Mapenzi ni sanaa nzuri sana. Haihitaji watu wa nje kuweza kuwaunganisha. Nyoyo zinapokuwa zinakubaliana, fedha hukosa nafasi kabisa. Huboreshwa na hisia zinazoingia na kutoka, yaani kila mmoja awe na mguso wa hisia za mwenzake. Kwa kifupi, mapenzi bora ni yale yanayojengwa na hisia za kubadiliashana (give and take).
Usione shida kabisa. Kubali kujishusha kadiri inavyowezekana. Pengine ukawa unajiona dhalili pale unapoelezea namna ulivyo au mapito yako ya nyuma. Unaweza kujihisi mnyonge unapokuwa unakiri kosa. Usikubali kiburi kikutawale, usipende mamlaka kwa mwenzi wako. Yeye ajishushe, nawe jishushe, utaona uhusiano wenu utakavyokuwa bora.
Nguvu na mamlaka vinavyokutawala, hukufanya ushindwe kujidhibiti. Unaweza kumtamkia mwenzo wako neno lolote. Kujishusha, hukusababishia wewe kujiongezea sifa na uhalali wa kuitwa mpenzi. Yaheshimu mapenzi, maana yakikunyookea na maisha huwa bora pia. Ukiogopa kuwa mnyonge, ukataka uonekane upo juu, mapenzi kwako yatageuka mateso.
8. FIKIRI KABLA HUJAFANYIA KAZI HISIA
Unapoongozwa na hisia, utajikuta unafanya makosa mengi kila siku. Fikiria kuwa kuna kitu kinakunong’oneza kuhusu ubaya wa mwenzi wako. Kila baada ya muda, kitu hicho kinakukumbusha ndani kwa ndani. Kama hutakuwa makini, unaweza kujikuta unafanya uamuzi wa kijinga ambao kwako baadaye utakusababishia mateso.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment