ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 13, 2013

Zuma: Afya ya Madiba yaanza kuimarika

Pretoria. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amesema amefahamishwa na madaktari wanaomtibu Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela kuwa hali yake inaendelea vizuri.
Akizungumza kutoka katika Hospitali ya Mediclinic ya mjini Pretoria, Zuma alisema kwamba madaktari wamesema hali ya Mandela ambayo ilizua simanzi na mashaka kwa siku tano zilizopita inaimarika.
Rais Zuma alisema amefurahishwa na jinsi hali ya rais huyo inavyoendelea kuimarika.
Juzi Zuma, aliwataka wote wenye nia njema na afya ya kiongozi huyo wa zamani wazidi kumwombea ili apate ahueni haraka.
Rais huyo mstaafu wa Afrika Kusini,alilazwa hospitalini kwa siku ya sita sasa ambako anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa mapafu.
Taarifa kutoka ofisi ya Rais Jacob Zuma, zinasema kuwa Mandela mwenye umri wa miaka 94, yuko katika hali mbaya ingawa imeweza kudhibitiwa.
Jamaa zake pamoja na aliyekuwa mkewe Winnie Madikizela- Mandela, walimtembelea hospitalini Jumatatu
Mtoto wa kwanza wa Mandela, Zenani Mandela-Dlamini, pia alirejea kutoka nchini Argentina, ambako yeye ni balozi.
Mandela yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi tangu alipolazwa hospitalini hapo Jumamosi iliyopita ikiwa ni mara ya tatu kwa mwaka huu.
Kumekuwa na taarifa za simanzi kwa mara ya kwanza huku familia yake ikikusanyika kando yake, baadhi ya watu wakisema kuwa wamwache Mandela aende zake.
Kwa mujibu wa taarifa za ofisi ya rais, Mandela amekuwa akiugua kwa muda mjini Johannesburg baada ya kukumbwa tena na ugonjwa wa mapafu.
Msemaji wa Rais Zuma, Mac Maharaj alisema kuwa maofisa katika hospitali wanataka kudhibiti idadi ya watu wanaozuru hospitali hiyo ili wampunguzie Mandela usumbufu.
Mwananchi

No comments: