Mwanahamisi Majube amelala katika kitanda cha hospitali moja ya umma (jina linahifadhiwa) ikiwa ni saa chache baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua.
Analia na kuugulia kwa uchungu, akilalamikia maumivu makali ya tumbo.
Kwa sababu hiyo, anamwita daktari akimweleza kuwa anahisi kuna kitu tumboni mwake na kinamuumiza mno, lakini daktari anamjibu kuwa maumivu hayo yatatulia.
“Nisaidieni nitakufa kabla ya kumwona mtoto wangu, naumwa daktari, nakufa jamani,” anasema Mwanahamisi.
Anapoendelea kuita, wakunga ndani ya wodi hiyo wanaibuka na kumjibu: “Acha kudeka, ulifikiri kuzaa ni kama kucheza kamari. Nyamaza, unawapigia kelele wenzako.”
Anaendelea kuita kwa zaidi ya saa lakini bila msaada wowote na baada ya kulia kwa muda mrefu, anatupa miguu huku na kule…ananyamaza, kisha anatulia. Kumbe… Mwanahamisi amekata roho!
Mwanahamisi ni miongoni mwa wanawake wengi nchini ambao hukumbana na vifo vya kuepukika wakati wa kujifungua au muda mfupi baadaye.
Vifo hivyo, vingi vinasababishwa na uzembe wa madaktari, huduma dhaifu, ukosefu wa vifaa na sababu nyingine zinazozuilika wakati wa kujifungua.
Pamoja na uchungu wa kujifungua anaoupata mwanamke, ukosefu wa vifaa tiba, maumivu mengine huyapata toka kwa baadhi ya wahudumu wa afya.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wanawake, hasa wale wanaojiweza kukimbilia katika hospitali binafsi ambapo wanapata huduma bora zaidi.
Hata hivyo, ni wanawake wachache nchini wenye uwezo huo na zaidi ya asilimia 80 wanategemea hospitali za Serikali ambazo baadhi, ndizo zenye changamoto.
Katika mdahalo wa afya ya uzazi uliondaliwa na Dk Tausi Kida na Riziki Pansiano, wadau walikiri kuwa kuna matatizo mengi yaliyowakumba wanawake wakati wa kujifungua, kubwa likiwa rushwa na matusi.
Kwa mfano, wadau walieleza kuwa watoa huduma wengi, yaani wauguziwamelalamikiwa kuwa wanadai hongo ili waweze kutoa huduma kwa wagonjwa.
Hii ni sababu mojawapo muhimu inayowafanya kinamama wasijifungue chini ya uangalizi wa wataalamu wa tiba kwenye vituo vyetu vya afya na hivyo kuwa kwenye hatari zaidi ya kupata matatizo wakati wanapojifungulia nyumbani.
“Niliwahi kushuhudia mama mjamzito kuachwa mapokezi mpaka kafariki bila hata kuhudumiwa. Ndugu wa dada huyu waliambiwa kuwa bila ya elfu 75 mgonjwa wenu hapati huduma kwa daktari.
Kinamama hawa wakiendelea kuchangishana mmoja hadi mwingine wakifuata fedha hadi huko Morogoro, mwishowe baada ya saa karibu nane baada ya pesa kutopatikana mwenzetu akafariki.”
Wachangiaji pia walihusisha matatizo ya vifo na matusi na maneno ya kukatisha tamaa wanayoyatoa manesi kwa wajawazito.
“Mama akiomba msaada utasikia mfuate huyo aliyekupatia mimba”. Alisema mchangiaji mmoja.
Maneno mengine yanayowatoka wauguzi ni kama vile usitusumbue hatupo kwa ajili yako hapa, mara unataka nijigawe ili nimhudumie huyu na wewe.
“Nimepata kumsikia nesi akisema kuwa huyu mwanamke asije akatulaza macho, anasema Dk. Salatiel Moyo, mchangiaji katika mjadala huo.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa vifo vya uzazi Tanzania ni 578 kati ya vifo 100,000 ambayo ni sawa na asilimia 18 ya vifo vyote vya wanawake wa kati ya miaka 15 hadi 49.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaeleza kuwa, asilimia 46 tu ya wanawake ndiyo husaidiwa na mtaalamu wa afya wakati wa kujifungua.
Faraja Mujuni, alimpoteza mtoto wake na kujikuta akiondolewa kizazi baada ya kupata uchungu pingamizi kwa muda mrefu.
“Kila nilipomwambia mkunga kuwa mtoto anatoka alikataa, kila nililomweleza alikuwa akiniangalia na kunifyonza, mwishowe, mtoto alifariki na mimi kuondolewa kizazi, kwani kilipasuka,” anasema Faraja.
Mwanamke mwingine, Anastazia Simwanza, mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam anasema alipofikishwa katika wodi ya wazazi, alikuta vitanda vimejaa, hivyo akaambiwa alale chini.
“Ilikuwa saa tisa usiku. Wakati huo uchungu ulikuwa ukiniuma kwa kasi, nikamwita nesi, lakini akaniambia bado kabisa mtoto hajashuka,”anasema Simwanza.
Simwanza anaeleza kuwa, baada ya dakika kadhaa, chupa ilipasuka na mtoto akaanz saa kutoka, jambo lililosababisha ajifungue mwenyewe, bila msaada wa muuguzi na mtoto aliangukia chini sakafuni.
“Mwanangu alipata matatizo kwa sababu aliangukia sakafuni ndiyo maana hajatembea mpaka sasa wakati ana miaka sita,” anasema.
Paschal Msechu anaeleza jinsi yeye na mkewe mjamzito walivyotukanwana na wauguzi wakati mke wake alipokuwa akiugulia maumivu ya uchungu wa kujifungua.
“Kila nikijaribu kuwaeleza waliniambia niwaache wao wanajua kazi yao, walianza kumtukana mke wangu kwa sababu alikuwa hawezi kutembea, wakamrushia maneno mazito,” anasema Msechu.
Si huyo tu, Yohana Mwanga, anaeleza jinsi mke wake mpenzi alivyopoteza maisha kwa sababu tu ya kukosa vifaa.
“Hatukuwa tumebeba vifaa vyote, wakati muuguzi ananiambia hayo, mke wangu alikuwa katika hali mbaya mno. Wakati natafuta hela za kununua, mke wangu alifariki kwa kukosa huduma.” Anasema Mwanga
Mwanga, kwa masikitiko anasema: “Nimempoteza mke wangu kwa kukosa fedha tu, wala si kingine.”
Idadi kubwa ya vifo vya uzazi katika baadhi ya maeneo duniani inaonyesha ni kutokana na kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa huduma za afya, na inaonyesha pengo kati ya matajiri na maskini.
Karibu wote, vifo vya uzazi (asilimia 99 hutokea katika nchi zinazoendelea.
Mhadhiri wa Chuo cha Wakunga katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili, Dk Sebalda Leshabari, anasema wakunga wenye tabia zinazolalamikiwa na wanawake wanafanya makosa kwani hawakufundishwa hivyo vyuoni mwao.
“Hakuna mkunga anayefundishwa kuwa jeuri au kutukana, sisi tunawafundisha mawasiliano mazuri na mama mjamzito na ujuzi mwingine,’ anasema Dk Leshabari.
Anasema hata Chama cha Wakunga Tanzania (TMA) wakati wa makongamano hutoa elimu na kuwakumbusha wakunga kuhusu huduma nzuri kwa wajawazito.
“Hizo shutuma tunazisikia zote na tunawapa mifano wanafunzi wetu wasirudie tabia hizo,” anasema
Dk Leshabari pia anatoa angalizo zaidi na kusema mpaka sasa ni asilimia 61 tu ya wanawake Tanzania wanaojifungulia hospitali, je, wengine wanajifungulia wapi?
Mwananchi
6 comments:
serekari imeoza fukuza wahudumu wote tena peleka ndani miaka 25 na madactari wote wanaozembea funga vifungo vya maisha walio baki watatia adabu
Sasa kwani tatizo ni Madaktari au tatizo ni serikali haiwajali wakina mama hapa. Madaktari wao wafanye nini sasa? Jamani tusiwe wa kutoa comment haraka haraka bila kufikiria ndugu zangu. Serikali ndo iliyo watupa wamama waja wazito na sio madaktari, hao madaktari wenyewe hawalipwi mshahara wa kutosha na wala hawalipwi on time sasa wao wafanye nini???
halafu wakishakufukuzwa na kufungwa nani atasaidia katika kuzalisha? hilo sio solution! ni hivi kuwekwe CCTV au camera zitakazoonesha matendo ya kila nurse na daktari then kila siku zikaguliwe na watu maalum, ikigundulika nurse au daktari kafanya kinyume na matakwa yake katika kiapo cha kuhudumia wagonjwa kwa ukarimu na upole. hapo atumikie kazi ya huduma ya jamii bila ya kulipwa mshahara kuanzia miezi 3 na akipinga aende jela miaka 3 na faini juu vitaifishwe vitu vyake vyote, Ahhh Allah nijaalie one day nije nichaguliwe waziri wa afya au katibu tu watakoma,,, mana na mimi ni daktari but siwezi kumfanyia mgonjwa hivyo. kama wanavyofanya hao wajuba ma-nurse, na ukiwaambia wanapinga kama hawafanyi, wakati mimi binafsi nishapata ajali ya gari mwaka 2004 nikalazwa Muhimbili basi nurse ananiambia kua usijitandaze kitandani anakuja na mwenzako hahaha tena kwa kunishushua na macho kuyarembusha, nikamtazama mana nilikua na maumivu makali ya majeraha kwahio sikujibu kitu ,, aahh hatari, mwishowe wakatuibia handbag yetu ambayo kulikua na simu ndani na vitu vya dhahabu na hela... WHAT A KIND OF HUMANITY?
Kwa kweli hali hii inasikitisha sana, watu wengine wamekosa ubinaadam kabisa, yaani mtu anashuhudia mkewe akifariki hivihivi kwa sababu hana fedha za kulipia huduma? Mabadiliko ya haraka yanahitajika kwenye hii sekta ya afya nyumbani ila wahusika hawako tayari, hilo ndio tatizo.
Mdau Haji Jingo, California.
SASA KWANINI AMKUITAJA HIYO HOSPITALI.????? Aaarrrggghhhhhh .
kama watu wote tutakuwa na HOFU YA MUNGU na kutambua kuwa ipo siku tutaulizwa kwa kila punzi, matendo na hatua tunazozipitia katika maisha yetu. na kujua kwamba tutalipwa kutokana na hayo tuyatendayo basi lazima utakuwa na huruma kwa kila nafsi na sio tu ya binadamu mwenzako, naamini utahofia hata kumkanya mdudu mdogo kama sisimizi kwani utahisi kuwa unaidhurumu nafsi. Na kama wafanyakazi na watumishi wote watajua kuwa Mungu Atawauliza kutokana na hizo kazi wanazozifanya basi watakuwa na haruma kwa watu wanaowahudumia. na serikali ni lazima itambuae kuwa lazima wafanyakazi wengine wapewe upendeleo kutokana na ugumu au hata mazingira yao ya kazi kuwa ni hatarishi zaidi ili kuwanyanya wawe na furaha na kazi yao. BINADAMU TUMUOGOPE MUNGU. KWANI HAKUNA JAMBO TUNALOLIPATA AU KUMILIKI ILA KWA UWEZO WAKE MUNGU. NA KAMA MUNGU AKIAMUA IPO SIKU WEWE UNAEHUDUMIA WENZAKO VIBAYA, NAWE UTAOMBA KUHUDUMIA.
Post a Comment