Raia wa Afrika Kusini akiwa na bango la kumtakia kheri ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Mstaafu wa nchi hiyo, mjini Polokwane nchini humo. Picha na Mtandao.
Johannesburg: “Happy birthday Mzee Madiba.” Rais wa kwanza na mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo anatimiza umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.
Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern Cape na ametumia zaidi ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na usawa wa wananchi wa Afrika Kusini.
Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.
Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’ ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.
Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine ambao ni wahitaji katika jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo ambaye ni alama ya dunia.
Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa alianza kampeni na harakati za kutetea haki za binadamu mwaka 1942 na baadaye mwaka 1964 alikamatwa na kuwekwa gerezani alikokaa miaka 27 lakini alipotoka aliwatumikia Waafrika Kusini akiwa rais wao wa kwanza mzalendo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Sello Hatang aliwataka Waafrika Kusini kufanya shughuli yeyote ile au msaada ambao utakuwa ni mchango kwa jamii yao.
“Watu wafanye kile wanachoona kinawapendeza, watumie dakika 67 za kumuenzi Mandela. Ni vyema wakafanya kitu ambacho kinawafurahisha ili waendelee kukifanya kila mwaka katika maisha yao”, alisema Hatang.
Alisema Waafrika Kusini wanaweza kumuenzi Mandela kwa kuwasaidia wazee na watoto yatima katika vituo mbalimbali, kufanya usafi au kuwatazama na kuwapa chochote wagonjwa.
Miaka 15 ya ndoa
Siku hii pia inakwenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 15 ya ndoa yake na mke wake wa tatu; Graca Machel ambaye walifunga naye ndoa Julai 18, 1998 wakati wa kumbukumbu ya miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Pia siku hii inaadhimishwa siku tatu baada ya kutimia miaka 69 tangu Mandela alipofunga ndoa na mkewe wa kwanza Evelyn Mase Julai 15, 1944. Evelyn ambaye sasa ni marehemu alikuwa muuguzi, pia binamu wa aliyekuwa mpigania uhuru wa Afrika Kusini, Walter Sisulu.
Graca ndiye mtu wa karibu zaidi na Mandela kwa sasa na kwa siku 40 amekuwa akiishi hospitalini Medclinic akimuuguza mumewe na mchana kutwa amekuwa akikaa pembezoni mwa kitanda cha Mandela na pale anapochoka hasa usiku, hulala kwenye chumba kinachopakana na kile alicholazwa mumewe.
Ndugu wengine kutoka familia ya Mandela wamekuwa wakifika hospitalini mara kwa mara kumjulia hali kisha kuondoka. Miongoni mwao ni pamoja na mtalaka wake, Winnie Madikizela-Mandela pamoja na binti yake mkubwa, Makaziwe ambaye ni binti pekee wa Mandela aliye hai aliyemzaa kwa Evelyn miaka 60 iliyopita.
Nje ya Medclinic, kuta za uzio unaozunguka hospitali hiyo zimeendelea kupambwa kwa kadi, michoro, picha, maua na ujumbe ambao unamtakia heri ya kupona haraka Mzee Mandela. Hata hivyo, leo pengine na siku chache zijazo kuta hizi zitageuzwa kuwa mahali pa salamu za pongezi kwa Mandela kufikisha umri wa miaka 95.
Mbali na hayo, kwenye kuta za Medclinic, katika lango la kuingilia hospitalini hapo, nyimbo na sala vimeendelea kusikika kutoka makundi mbalimbali kumwomba Mungu ampe maisha marefu zaidi.
Miongoni mwa vikundi vilivyokuwapo hapo vikipaza sauti zao ni kwaya ya Shule ya Sekondari ya Juu ya Wasichana ya Oranje ambao ni siku chache tu ilirejea kutoka katika tamasha la muziki la vijana huko Slovakia na kupata ushindi dhidi ya vikundi vingine 22.
Mandela ni nani?
Kwa jumla, Mandela unaweza kumwita utakavyo kwa maana ya ukombozi na Afrika Kusini ya sasa. Kwa maana hiyo ni mwanasiasa, mpigania uhuru, mwanasheria, mfungwa wa uhaini, Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Chifu wa Wathembu na zaidi ya yote, Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini.
Nelson Rolihlahla Mandela ni mtoto wa Mama Nonqaphi Nosekeni na Mzee Henry Mgadla Mandela ambaye alikuwa Kiongozi wa Kimila (Chifu) katika jamii ya Wathembu.
Awali, kabla ya kuitwa Nelson, alijulikana kwa jina lake la kati, Rolihlahla ambalo maana yake ni ‘kungo’a tawi kutoka kwenye mti’ au kwa maana isiyo rasmi ‘mtu mkorofi’. Jina la Nelson alipewa na mwalimu wake alipojiunga na shule ya wamisionari.
Mandela aliishi na baba yake kwa miaka 12 tu kwani mzazi wake huyo alifariki dunia mwaka 1930 na kuanzia hapo alilelewa na mpwa wa baba yake, David Dalindyebo ambaye pia alikaimu uongozi wa katika jamii ya Wathembu.
Mwaka 1944, Mandela alioana na Evelyn ambaye alijaliwa kupata mtoto wa kiume mwaka 1945 na kumwita Madiba Thembekile (Thembi kwa kifupi). Hata hivyo, mtoto huyo alifariki katika ajali ya gari mwaka 1969 wakati Mandela akiwa jela.
Mandela na Evelyn walijaliwa kupata watoto wengine watatu; Makaziwe mkubwa ambaye hata hivyo, alifariki dunia akiwa mchanga 1948, Makgatho Mandela aliyezaliwa 1950 na kufariki 2005 na Makaziwe mdogo mwaka 1953 ambaye kwa jumla ndiye anayesimamia shughuli na mali katika familia hivi sasa.
Desemba 1956 alikuwa mmoja wa washtakiwa wa kesi ya uhaini na wakati kesi hiyo ikiendelea alioana na Nomzamo Winifred Madikizela mwaka 1958. Alibahatika kupata naye watoto wawili wa kike.
Kijijini Qunu
Kumekuwa na harakati nyingi za maadhimisho ya Siku ya Mandela na mojawapo ni tukio la Waafrika Kusini wawili waliopanda Mlima Kilimanjaro kumuenzi.
Katika Kijiji cha Qunu, vijana wamejipanga kusafisha mitaa, kupaka rangi shule, huku wanasiasa wakitumia kila mmoja dakika 67 kuzindua au kukamilisha mradi wowote wa kitaifa.
Watoto wote katika shule za msingi na sekondari wametakiwa kuanza vipindi vyao vya masomo kwa kuimba ‘happy birthday’ Mandela.
Msemaji wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, huko Port Elizabeth, Jean Makasiwe alisema kila mhadhiri, mwanafunzi na mfanyakazi wa chuo hicho atashiriki kwa namna moja au nyigine kumuenzi Mandela.
“Natumaini kuwa kila mmoja atashiriki, ingawa yeye Mandela hataifurahia siku hiyo muhimu kwake, lakini tuna hakika atafanya hivyo wakati akiadhimisha miaka 96 hapo mwakani,” alisema Makasiwe.
Alisema chuo hicho kilijengwa kwa kumbukumbu ya Mandela, hivyo ni lazima kila mmoja ajitoe kumuenzi baba huyo wa taifa.
Rais Zuma leo atakabidhi nyumba 300 kwa wazungu wa eneo la Bethlehemu huko Pretoria ambao wanaishi katika makazi duni.
Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki Moon amewataka watu wote duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya kazi nzuri kwa watu na kwa dunia.
“Hii ndiyo namna pekee ambayo tunaweza kumlipa mtu huyu wa kipekee ambaye alijitoa kwa namna ya pekee kuwasaidia watu wa taifa lake,” alisema Ban na kuongeza:
“Mandela alitumia miaka 67 kupigania haki za binadamu, usawa na umoja. Katika kuadhimisha siku hii, UN inashiriki kwa kuwataka watu ulimwenguni kutoa dakika 67 za muda wao kwa ajili ya kuadhimisha.”
Watu tisa kati ya 10 Afrika Kusini, wapo tayari kushiriki kikamilifu kusherehekea na kutoa muda wao kumuenzi Mandela.
Asilimia 89 ya watu 16,046 waliofanyiwa uchunguzi wamekubali kutoa dakika 67 za muda wao kwa ajili ya kufuata njia ya kujitoa kwa jamii kama Mandela alivyofanya.
Utafiti huo uliotolewa jana na Kampuni ya Pondering Panda ulionyesha kuwa karibu Waafrika Kusini wote wapo tayari kusherehekea Sikukuu ya Mandela kwa kujitoa kusaidia, kuchangisha fedha, kufanya usafi, kuhudumia wagonjwa na yatima.
“Idadi hii inaonyesha kuwa tutafanya mambo makubwa hapa nchini kupitia siku hii, hapo kesho (leo), tunataka kila mtu aonyeshe kuijali siku hii kama Mandela alivyosema,” alisema Msemaji wa Pondering Panda, Shirley Wakefield.
Alisema Siku ya Mandela iliundwa maalumu kwa ajili ya kuwaunganisha Waafrika Kusini wote wenye mapenzi mema kwa nchi yao na duniani kote.
Katika eneo la Upington, kundi la wazee linamuenzi na kumshukuru Madiba kwa kuwapa eneo la makazi na wanasema pasipo jitihada zake za 1998, wasingeweza kupata eneo hilo.
Huko Eastern Cape alikozaliwa Mandela, baadhi ya shule za msingi zilinufaika na Wiki ya Mandela baada ya kupata ufadhili wa seti zote muhimu za vifaa vya kompyuta ambavyo awali hawakuwa navyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment