Thursday, July 18, 2013

TFF yaifuta mechi ya Yanga, 3 Pillars

Shirikisho la soka (TFF) limeifuta mechi ya kirafiki baina ya klabu ya Yanga na 3 Pillars ya Nigeria iliyotarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja a Taifa jijini Dar es Salaam kwa sababu timu hiyo imewasilisha taarifa za uongo kwamba imepanda ligi kuu la Nigeria.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah aliiambia NIPASHE jana jioni kwamba wameifuta mechi hiyo baada ya kuwasiliana na shirikisho la soka la Nigeria (NFF) na kufahamishwa kwamba ziara ya klabu hiyo haijaidhinishwa.

"Hii ziara ni ya kitapeli, tumewasiliana na NFF wamekanusha madai kwamba klabu hiyo imepanda Ligi Kuu na wameikana barua waliyotuletea kwamba wameidhinishiwa na shirikisho hilo safari yao ya kuja huku," alisema Angetile.

Alisema kutokana na hilo TFF imeamua kuifuta mechi hiyo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alikiri kutaarifiwa kuhusu kufutwa kwa mechi hiyo.

"NI kweli TFF wametutaarifu kwamba mechi imefutwa kwa hiyo haitakuwapo. Hata juzi niliwaeleza wanahabari kwamba mechi hiyo itachezwa iwapo tu itaidhinishwa na TFF," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga.
Simu ya muandaaji wa mechi hiyo, Salum Mkemi iliita bila ya kupokewa.


Awali Mkemi alisema kwamba tayari Wanigeria hao wako hapa nchini tangu wiki iliyopita na lengo la ziara yao ni kufanya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Nigeria ambapo alidai wamepanda daraja.
"Safari hii tumeamua kuileta timu ya Afrika Magharibi ili kuwapa Yanga changamoto na vionjo tofauti, tunafahamu timu zetu zimekuwa zikisumbuliwa na timu za ukanda huo na kutolewa katika mashindano ya kimataifa," alisema Mkemi.

Aliongeza kuwa baada ya mechi dhidi ya Yanga, 3 Pillars ingeelekea jijini Mbeya kuvaana na wenyeji Mbeya City ambayo imepanda daraja msimu uliopita.

'Kuzagaa zagaa' kwa timu hiyo tangu nchini tangu juma lililopita huku ikifikia katika hoteli "za kawaida" kulizua maswali kuhusu timu hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: