Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Mtwara wakiwaonyesha waandishi wa habari majeraha yanayodaiwa waliyapata baada ya kupigwa na wanajeshi wa JWTZ.
Viongozi watano wa Chama cha Wananchi (CUF), wamesimulia mateso na vipigo walivyovipata wakati wakiwa mikononi mwa Jeshi la Wananchi (JWTZ) mkoani Mtwara.
Viongozi hao ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi (Taifa) Shaweji Mketo, Mwenyekiti Jumuiya ya Vijana (JUVICUF) wilaya ya Mtwara Vijijini, Ismail Njalu na Mwenyekiti wa wilaya ya Mtwara Mjini, Salum Mohamed.
Wengine ni Mwenyekiti wa wilaya ya Mtwara vijijini, Ismal Jamal, Katibu wa wilaya ya Mtwara Mjini, Said Kulagwa na dereva wa gari walilokuwa wakilitumia siku ya tukio, Kashinde Kalumbwana.
Pamoja na taarifa hizo kwa wanahabari, wameeleza kusudio lao la kwenda mahakamani baada ya kuwasiliana na mwanasheria wao pamoja na asazi zinazotetea haki za binadamu.
Viongozi hao wanadai kukamatwa Juni Juni 27, mwaka huu na kupata mateso yaliyowasababishia majeraha, wakiyaonesha kwa waandishi wa habari, kwamba yalifanywa na askari wa JWTZ.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mketo, alidai kuwa siku ya tukio walikuwa wakitoka kufuatilia madai yaliyowafikia kuhusu kuwapo wanajeshi watatu waliombaka mtoto (hawakumtaja jina).
“Taarifa tulizopata nyumbani kwa mtoto huyo ni kwamba wanajeshi hao walifika hapo na kumkuta (mtoto huyo) akiwa jikoni, wakamdanganya kuwa watampa Shilingi 3,000, wakamkamata kwa nguvu wakambaka ila walitumia mipira,” alidai.
Mketo alisema katika kufuatilia zaidi tukio hilo, alibaini uchunguzi wa daktari uligundua kuharibika sehemu zake za siri za mtoto huyo.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, aliamua kulikabidhi suala hilo kwa viongozi wa chama eneo husika ili kuendelea kufuatilia hatma yake.
Alisema baada ya kulikabidhi, wakati wakirudi Mtwara mjini, walikutana magari mawili ya JWTZ yakiwa yameziba barabara.
Alisema eneo hilo kulikuwa na wanajeshi zaidi ya 50 ambao baada ya wao kusimama, walikamatwa na kuanza kupigwa.
“Nilikuwa na Shilingi 85,000 mfukoni wakati tunatembezewa kipigo, mmoja wa askari alitaka kuzichukua katika kupambana naye, mwanajeshi huyo alinihoji kwa nini nagombana na kanali wa jeshi,” alidai.
Alieleza kuwa baada ya kipigo hicho, walichukuliwa kupelekwa katika kambi ya jeshi ya Lembele, ambapo waliposhushwa, mmoja wa wanajeshi aliwataka wenzake waandae peni na panadol kwa ajili yao, lakini hawakujua ilimaanisha kitu gani.
“Tulivuliwa nguo zote na kuanza kupigwa bila kujali unapigwa wapi, tulipata majeraha na kuvuja damu nyingi, “ alidai na kuongeza:
“Cha ajabu kilichofuata, yalitengenezwa maji yenye barafu ambayo ndani yake yaliwekwa pilipili na ndimu, tukawa tunamwagiwa kwenye majeraha.”
Mketo alidai kuwa kwa upande wake, aliwahi kufanyiwa upasuaji eneo la ubavuni, hivyo kutokana na mateso hayo, aliamua kuwaweka wazi wanajeshi hao juu ya tatizo lake.
Alisema licha ya kufanya hivyo, kilichotokea ni kwamba aliitwa mwanajeshi (daktari) ambaye baada ya kudhibitisha hilo, waliamriwa wanajeshi wengine wawili wamshike mikono juu na kuambulia kipigo eneo lililofanyiwa upasuaji.
“Ilifikia hatua nikatamka maneno haya, nipigeni najua mmetumwa na Pinda, baada ya mateso makali, walimuita Mkuu wa upelelezi Mtwara na polisi ili watuhoji,” alisema.
Mketo alisema baada ya mahojiano, siku iliyofuata jioni walisomewa mashtaka yao na kupelekwa gerezani ambapo huko walikataliwa kutokana na majeraha waliyokuwa nayo.
“Jeshi la magereza liliamua kutuchukua kutupeleka hospitali ya Igula kwa matibabu na baadaye waliturudisha gerezani, hadi hapo tulipoachiwa,” alisema.
Akielezea zaidi hali ya Mtwara, Mketo alisema kuwa, sio shwari na kwamba wananchi wamekuwa wakipigwa bila hatia.
Kufuatia mateso hayo, CUF imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala hilo kwa sababu kazi ya polisi ni kulinda sio kutesa raia.
MAJIBU YA JWTZ
Julai Mosi mwaka huu, JWTZ ilikanusha askari wake kuhusika katika vitendo vya kubaka, wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao mkoani Mtwara.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi wa Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya jeshi Upanga, ilisomeka hivi:
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepokea taarifa kwamba waandishi wa Habari kadhaa wamepelekwa Mtwara kwenda kumhoji msichana mmoja kwa madai ya kubakwa na wananjeshi wa JWTZ.
JWTZ linapenda kuwafahamisha wananchi kuwa endapo taarifa hizo zitatangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya Habari wazipuuze kwani hazina ukweli wowote zaidi ya kuwa ni za upotoshaji.
Msichana huyo amepandikizwa ili kuharibu taswira nzuri ya JWTZ. Ifahamike kwamba maafisa na askari wa JWTZ waliopo huko Mtwara wanafanya kazi kwa uangalizi wa karibu na vitendo hivyo vya aibu hawawezi kuvifanya.
Jeshi letu linafanya kazi kwa nidhamu na si kama baadhi ya watu wenye maslahi binafsi wanavyolipaka matope.
Tunapenda kuwafahamisha watanzania wote kuwa JWTZ lipo kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote.
Tunasikitika sana kama wapo watanzania wenye mawazo hayo machafu ya kulichafua JWTZ lenye sifa nyingi ndani na nje ya nchi yetu.
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
KIKWETE, PINDA,SAID MWEMA NA WENZAKO MUNALO LA KUJIBU KESHO MBELE YA MUNGU? FIKIRIENI MUTAENDA KUULIZWA... SHAURI YENU...
Kama ninyi ndo mliokuwa manachochea Fuji huko Mtwara wala siwaonei huruma maana mlifanya Mtarwa kama eneo la vita, wamama walipoteza watoto wao, watoto walipoteana na mama zao, nyumba zilichomwa na watu walipoteza maisha yao pasipo sababu maaalumu. Mliteswa bila sababu kwani?? Kama mliteswa bila sababu fungueni mashtaki Police kesi ianze.
Post a Comment