Moshi. Mashahidi wawili wa upande wa mashtaka, wameieleza mahakama namna wanyamahai, wakiwamo twiga wanne, walivyosafirishwa kwenda Doha nchini Qatar kwa kutumia ndege ya jeshi.
Mashahidi hao, akiwamo mmoja wa madereva wa lori, walitoa ushahidi wao juzi wakiongozwa na jopo la mawakili watatu wa Serikali, Evetha Mushi, Pius Hilla na Stella Majaliwa.
Shahidi wa sita, Davis Kimei aliyekuwa dereva wa lori aina ya Mitsubish Fusso, alieleza namna alivyosafirisha wanyama hao toka Arusha hadi Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia).
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo shahidi huyo alidai Novemba 25, 2010 alikodishwa kubeba wanyama hao na watu watatu, wakiwemo wawili wenye asili ya kiasia hadi uwanja wa Kia kwa ujira wa Sh150,000.
“Baada ya kuelewana tulikwenda hadi kwenye nyumba moja eneo la Kwamrefu, Arusha na humo ndani nilikuta vijana wengi ambao walikuwa wakitengeneza mabox yaliyokuwa na Twiga na Swala,” alisema.
Shahidi huyo alidai baada ya kuwapakia wanyama hao, msafara wa malori manne ulielekea Kia na kufika saa 8:00 usiku na kuelekea moja kwa moja uwanjani ambapo walikuta ndege kubwa ya jeshi imeegeshwa.
“Maboksi yale yalishushwa na kupakiwa katika ndege hiyo usiku ule wa manane,” alisema.
Shahidi wa saba, alidai siku ya tukio saa 4:00 usiku aliwasikia wafanyakazi wawili uwanjani hapo, wakisema kuna wanyama wangesafirishwa usiku huo.
“Nilimdokeza mkuu wa upelelezi… Nilipokuwa nyumbani bosi wangu alinipigia simu na kuniambia ile taarifa niliyompa ilikuwa ni ya kweli kuna ndege ya Serikali inasafirisha wanyamapori,” alisema.
Shahidi huyo alidai kuwa saa 6:00 usiku alirudi kazini na ilipofika saa 8:30 usiku lilikuja basi aina ya Toyota Coaster ambapo walishuka watu wenye sare za jeshi wenye asili ya kiarabu.
Washtakiwa katika kesi hiyo inayovuta hisia za Watanzania wengi ni Kamran Ahmed, Hawa Mang’unyuka, Michael Mrutu na Patrick Paul na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Agosti 13 na 14.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment