ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 6, 2013

Watendaji Dar waonywakuhusu wamachinga


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, ametangaza kiama kwa watendaji wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam watakaoshindwa kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi kwa biashara watawajibishwa.

Sadick, alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa katika kipindi cha `Kumepambazuka' kinachorushwa na Radio One jijini Dar es Salaam jana.

Alisema watendaji wa Halmashauri za Kinondoni, Ilala na Temeke wanapaswa kudhibiti wamachinga wasirejee kwenye maeneo waliyoondolewa kwa sababu wanachangia kukithiri kwa uchafu.Alisema suala la usafi katika Jiji la Dar es Salaam ni la kudumu, hivyo kama wapo viongozi na wanasiasa wanaowadanganya wamachinga warejee kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kufanya biashara wakibainika watachukuliwa hatua.

Naye Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Abdallah Chaurembo, alisema jiji hilo limepanga kuanza kuwatumia polisi jamii katika kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wasiozingatia masuala ya usafi.

Chaurembo alisema wapo baadhi ya watu wanadhani suala la usafi katika Jiji la Dar es Salaam ni la kisiasa na kuwataka wanaodhani hivyo wajaribu kukiuka kanuni za usafi waone kama hawatachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda alisema baadhi ya wasimamizi wa sheria katika halmashauri wamekuwa siyo waaminifu kutokana na kula njama na baadhi ya wamachinga ili waendelee kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Mwenda alisema kutokana na tabia hiyo ambayo inazorotesha utekelezaji wa zoezi la usafi, Manispaa ya Kinondoni ipo katika mkakati wa kufanya uchunguzi kuwabaini watendaji wenye tabia hiyo ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alisema mfumo wa halmashaiuri za Jiji la Dar es Salaam wa kuendesha operesheni za safisha jiji, ni wazi kuwa hauwezi kuwa endelevu badala yake kunahitajika kuanzisha kitengo maalum cha kushughulikia suala la usafi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: