ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 19, 2013

Waziri: Nimeshidwa

  Anyoosha mikono kusimamia usafi Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, amesema ameshindwa kuzichukulia hatua Manispaa za Jiji la Dar es Salaam zilizoshindwa kusimamia usafi katika maeneo yao.

Kutokana na hali hiyo, amesema ameamua kulipeleka suala hilo kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kwa madai kuwa ndiyo mwenye mamlaka ya kuwachukulia hatua.

Waziri Huvisa alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuhusu kampeni ya usafi wa miji na majiji, itakayofanywa jijini humo na Makamu wa Rais, Julai 21 na 22, mwaka huu.


Ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa kampeni ya usafi kwa miji na majiji iliyozinduliwa Februari 12, 2011 na watendaji wa mamlaka hizo kuagizwa kusimamia.

Alisema hali ya usafi kwa jiji la Dar es Salaam si ya kuridhisha na mara kwa mara amezihimiza manispaa kusimamia sheria na kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi, lakini wamekaidi.

“Halmashauri za Kinondoni na Temeke ndizo sugu kwa uchafu. Afadhali kidogo Manispaa ya Ilala. Iwapo halmashauri zitaamua kusimamia usafi, jiji litakuwa safi kama ilivyo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kata zake,” alisema Waziri Huvisa.


Alisema kilichokosekana ni uwajibikaji na kwamba, kwa mujibu wa sheria, waziri ni msimamizi wa sera na hana ‘meno’ ya kuwachukulia hatua watendaji wanaokaidi.

Hivyo, akasema anampelekea Makamu wa Rais akajionee hali halisi baada ya suala hilo kumshinda.

Alisema watendaji wa maeneo yatakayotembelewa na Makamu Rais, wameandikiwa barua kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi na kinachokaguliwa na iwapo wametii agizo husika.

“Kwa kuwa wameshindwa kutii agizo langu, sasa ninawapeleka kwa anayehusika nao, waeleze kwa nini hakuna vifaa vya kuzolea na kuhifadhia taka. Magari ya taka hayako mtaani na haijulikani yalipo,” alisema Waziri Huvisa.

Alisema kampeni ya usafi ilianza mwaka 2011, bado usafi hauridhishi, taka ngumu katika maeneo muhimu kama masoko na machinjio hazizolewi kwa wakati, utunzaji wa mifereji ya maji ya mvua na utunzaji wa bustani za burudani haujafikia kiwango.

Waziri alisema usafi uliofanyika kabla ya ujio wa Rais wa Marekani, Barrack Obama, ni utamaduni wa kawaida kuhakikisha eneo analotembelea mgeni linakuwa safi.

“Kabla ya ugeni kulikuwa na kampeni ya usafi, hivyo ilikuwa inaendelea, lakini hakuna ubaya iwapo utafanya usafi mgeni anapokuja kwako,” alisema.

Alisema kinachotakiwa ni wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi na kuachana na tabia ya kuona jukumu hilo ni la serikali pekee.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais, atatembelea maeneo ya masoko, barabara, maeneo ya kuhifadhia taka na makazi kwa jiji la Dar es Salaam na maeneo machache ya mkoa wa Pwani.

Wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi katika maeneo hayo, kwani watapewa nafasi ya kuuliza maswali kwa Makamu wa Rais.

Mwaka 1996 aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye, alivunja iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kushindwa kusafisha jiji hilo.

Baada ya kuivunja aliunda Tume ya Jiji iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Charles Keenja. Chini ya Tume hiyo operesheni kabambe iliendeshwa ikiwa ni pamoja na kubomoa vibanda vya biashara visivyotakiwa katikati ya jiji, kusafisha masoko na hata kujenga barabara na kukurabati majengo ya jiji ambayo yalikuwa yemekithiri kwa uchafu. Tume hiyo ilifanya kazi hadi mwaka 2000 wakati wa uchaguzi mkuu.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Jamani! Obama si kaondoka juzi tu? Let's just keep pretending na endeleeni kutangaza anakuja tena labda mji utabaki msafi au zoezi la usafi utaendelea, sasa kaka wewe waziri unasema umeshindwa basi achia ngazi wapewe wanaoweza ama?

Anonymous said...

Usafi ni juu ya wazawa wote wa jiji la Dar sio manispaa peke yake. Waswahili hadi kusafisha tunapoishi tunashindwa. God help us