ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 5, 2013

DR.SLAA AMKOSOA RAIS KIKWETE KUHUSU RWANDA

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, amemkosoa Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kauli ya kumshauri Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuzungumza na waasi wa serikali yake.

Dk. Slaa amesema haoni busara kwa Rais Kikwete kuwaambia viongozi wa Rwanda, akiwamo Rais Kagame, kuzungumza na wafuasi wa chama cha FDRL walioko Congo kwa vile wanatambulika kama wauaji.

Alisema hayo wakati akizungumza katika kongamano la vijana wa Chadema (BAVICHA) la uchumi na ajira lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Alimshangaa kuwataka kuzungumza na watu ambao Kagame anawaita wauaji wenye asili ya kundi la jeshi la Nterahamwe, lililokuwa linaangamiza Watutsi.

“Rais Kikwete hapa nyumbani hawezi kuzungumza na wapinzani, hajachukua hatua dhidi wauaji wa mwandishi Daudi Mwangosi, alishauriwa amuwajibishe Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda, amempandisha cheo,” alisema.

Alisema Rais alitakiwa kuwaambia waje awapatanishe lakini si kuwaambia wazungumze na watu anaowatuhumu kuua Watutsi.

Kumezuka sitofahamu ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda, baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri huo wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni.

Ushauri huo ulionekana kumchukiza Rais Kagame, anayedaiwa kuhutubia mikutano kadhaa nchini kwake na kutumia lugha ya matusi, kejeli na dhihaka dhidi ya Rais Kikwete na Tanzania.


CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Naichukia sana CCM na napenda sana kuona Chadema ikiingia Magogoni siku moja na kusafisha nchi yetu iliyosheheni ufisadi kila kona..... Hapa dr.sikuungi mkono hata kidogo!! Rais Kikwete alitoa ushauri na unaposhauriwa una chaguo la kufuata ushauri au kutofuata.. yote si lazima!! Muungwana husema nimesikia.. Ni wazi Kagame analake jambo.. Kikwete anawakilisha Tanzania! Kumtukana ni kututukana waTanzania!! Tofauti zetu kisiasa zisitugawanye ktk masuala yenye mustakbala wa nchi! Kagame ni muuaji na mwisho wake hautokuwa mzuri! Ni wangapi wanamnyooshea vidole? Huyu jamaa ni hatari sana! Si wakuunga mkono hata kidogo!! Ni muuaji na siku moja atalipa damu yote iliyomwagika Rwanda ( genocide) Tusisahau ujambazi wake kule Congo pia!! Hawezi kutupenda hata kidogo!! EAC imegawanyika!! Tukae chini tujipange.. tusianze kutoelewana wenyewe ndani ya nchi! Tanzania imetengwa na Kenya ,Rwanda na Uganda... tutafakari tufanye nini kuokoa mipango yote ya kiuchumi ambayo ililenga soko la Waganda na Kenya ! Tumu unge mkono Rais wetu dhidi ya Muuaji Kagame.