Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kinyan’ganyiro cha Urais wa Zimbabwe, Rais Robert Mugabe (89), amefikisha mihula saba ndani ya Ikulu ya nchi hiyo.
Mugabe juzi alishinda tena kiti cha urais. Matokeo rasmi yalionyesha kuwa aliibuka na ushindi wa asilimia 61 wa kura dhidi ya mpinzani wake, aliyekuwa Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai ambaye alipata asilimia 34.
Chama cha Zanu-PF kinachoongozwa na Mugabe na kile cha MDC cha Tsvangirai, viliunda Serikali ya Muungano mwaka 2008.
Juzi, Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC), ilimtangaza Mugabe kuwa mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika Jumatano iliyopita.
Zanu-PF pia kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wabunge baada ya kujinyakulia viti 137 kati ya 210.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa hali inaweza kuwa tete hasa baada ya matokeo hayo ambayo yalipingwa na Tsvangirai na chama chake cha MDC.
Tsvangirai alisema Chama cha MDC kitaisusia Serikali ya Mugabe na kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani. Wasimamizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Aidha, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ilimtaka Tsvangirai akubali matokeo ya uchaguzi.
Wasiwasi
Malalamiko yanayotolewa sasa na wapinzani kuhusu uchaguzi huo yanazidisha uwezekano wa kuibuka machafuko kama yaliyotokea 2008.
Mwaka huo, Tsvangirai aliongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na Zanu-PF kilipinga ushindi huo. Ghasia na machafuko vilitokea na kusababisha kuuawa kwa mamia ya wafuasi wa Tsvangirai.
Umwagaji damu uliotokana na uchaguzi huo ulimfanya Tsvangirai ajitoe kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo kutoa mwanya kwa Mugabe kutangazwa kuwa mshindi wa duru hiyo kirahisi.?
Hata hivyo, shinikizo la kimataifa lililofuata, lilimlazimu Mugabe kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuishirikisha MDC.
Tayari wananchi wa Zimbabwe katika Mji Mkuu wa Harare wanaamini kwamba wanapaswa kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kujiepusha na kuibuka kwa machafuko.
-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment