ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 6, 2013

SMZ: Hotuba za Ponda zililenga kuvuruga amani, utulivu Z`bar


Katibu Mkuu wa Taasis za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, amesema hotuba zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Taasis za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, kwenye baadhi ya misikiti ya Zanzibar, hazikubeba ujumbe wa kiroho.

Badala yake, amesema hotuba hizo zilikukusudia kuvuruga na kutikisa misingi ya amani na utulivu visiwani humu.

Balozi Seif aliyasema hayo baada ya kumalizika kufuturu futari maalum ilioandaliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya UVCMM katika ukumbi wa Gymkhana kisiwani hapa jana.

Alisema mikusanyiko na dhifa zenye muktadha wa kujenga ushirikiano na udugu, aghalabu hufanyika kwenye nchi na mahali kwenye mazingira ya ustawi wa amani na ni nadra kuzikuta zikifanyika nchi zinazokabiliwa na misuguano au mivutano ya kijamii.


“Mikusanyiko ya aina hii haipo kwenye nchi zenye migogoro, mivutano na kuporomoka kwa ustawi wa amani, inaongoza kufanyika Tanzania kutokana na amani, utulivu, umoja na mshikamano uliopo,” alisema Balozi Seif.

Akizungumzia hotuba zilizotolewa na Sheikh Ponda kwenye Misikiti ya Kwarara, Mbuyuni na Nungwi, alisema zilijiegemeza katika taswira ya kisiasa, uchochezi na dhamira ya kupandikiza chuki na mgawanyiko.

Alisema jukumu la kulinda amani, ni lazima liwahusishe wananchi wote na kusema kuwa amani ikitoweka ni sawa na mtu aliyechezea shilingi kwenye tundu la choo kwani kuipata kwake si rahisi.

Aliwaasa wananchi kutomshangilia mtu wa aina hiyo na kuwataka kuchukua tahadhari kwani kama machafuko yangetokea, Ponda asingepoteza ndugu wala jamaa visiwani Zanzibar.

“Ponda hana jamaa wala ndugu wa damu Pemba na Unguja. Uchochezi wake kama ungeibua maafa na vurugu, angeiachia Zanzibar msiba...hana mnasaba, angekaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune,” alisema Balozi Seif.

Aliwataka watu wanaoonyesha CD za mihadhara ya Ponda kuacha kufanya hivyo mara moja kwani mantiki ya hotuba zake zimepambwa na jinai inayohatarisha umoja na upendo miongoni mwa watu.

Akitoa neno la shukrani baada ya Balozi Seif kumaliza mazungumzo yake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema Zanzibar bado haijawa na dhiki ya wasomi wa elimu ya dini zote na kuwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaotumia dini kumomonyoa amani.

Vuai alisema historia ya Zanzibar inaonyeha ndiyo chimbuko la dini zote na kuenea katika maeneo mengine hadi kufika Kigoma, hivyo kuna hazina kubwa ya viongozi wenye upeo, weledi na maarifa ya kufikisha ujumbe wa Mungu

“Hata watoto wadogo hapa Zanzibar humudu kuhifadhi maneno ya Mungu kwa imani zao, ni rahisi watu kumjua mhamasishaji wa imani za kidini na anayepandikiza chuki na hasama. Tusikubali kupoteza umoja wetu,” alisisitiza Vuai.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: