ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 5, 2013

Wanafunzi 8,805 wakwama kuchaguliwa TCU

Dar es Salaam. Wanafunzi 8,805 walioomba kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2013/14, wameshindwa kuchaguliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kufanya makosa kwenye fomu zao za maombi, lakini wamepewa nafasi zaidi hadi Agosti 9, mwaka huu kurekebisha kasoro.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Sifuni Mchome imetaja moja ya sababu za baadhi ya wanafunzi hao kutokuchaguliwa ni sifa zao kutokukidhi masomo waliyoomba.
Alisema watatakiwa kuomba kwa kupitia mfumo wa udahili wa TCU ambao ulifunguliwa Julai 29, mwaka huu hadi Agosti 9, mwaka huu utakapofungwa.
Kutokana na hali hiyo, TCU katika taarifa hiyo imesema wanafunzi wana nafasi nyingine ya kuomba kwa kuchagua kusoma fani ambazo wana sifa nazo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanafunzi anatakiwa kuangalia jina lake katika orodha ya ambao hawakuchaguliwa ambayo inapatikana kwenye tovuti ya tume hiyo na kisha kufuata utaratibu.
“Baada ya mwanafunzi kuthibitisha jina lake kwenye orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa iliyoko kwenye tovuti ya TCU, anatakiwa kuchagua programu moja tu kutoka kwenye orodha ya programu inayopatikana kwenye tovuti ya TCU,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia mwanafunzi anatakiwa kufungua mwongozo wa udahili unaopatikana kwenye tovuti hiyo na kuthibitisha kwamba anayo sifa stahiki ya kujiunga na programu aliyoichagua.
Masharti hayo pia yanamtaka mwanafunzi ambaye hakuchaguliwa, kuingia kwenye sehemu ya taarifa za mwanafunzi (profile) kwa kuingiza jina analotumia na namba yake ya siri, kubofya kitufe cha kuomba, kuchagua programu moja tu, kubofya kwenye makasha ya kuthibitisha na hatimaye kuwasilisha maombi yake.
“Baada ya kuwasilisha maombi yako, mfumo wenyewe utakutaarifu kuwa ama unastahili kuomba programu hiyo au la na uchaguzi utakaoegemea kwenye msingi wa kwanza mwombaji huyo ndiye atakayehudumiwa mwanzo.”
“Pindi programu moja itakapojaa, haitaonyeshwa kwenye orodha ya programu zinazohitaji kujazwa kwenye mfumo wa udahili, hivyo utahitajika kujaza programu nyingine.”
Mwananchi

No comments: