ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 27, 2013

CHAUKIDU inakuletea Sarufi ya Kiswahili na Dhana ya Ngeli

Wasemi wa lugha yo yote ile hukusudia kuwasiliana na wenzao. Mara nyingi maana ya kinachokusudiwa haipotei eti kwa sababu neno halikutamkwa vema au msemaji alikosea kisarufi.  Sarufi ni dhana pana: Wataalam huipa sarufi maana mbili. Maana ya kwanza ni sarufi inayoshughulikia mpangilio wa sentensi katika lugha. Mtazamo wa pili ni ule unaoitazama sarufi kwa mapana yake na kuhusisha mpangilio wa sentensi, uundaji wa maneno au mofolojia, maana au semantiki,  na hata pragmatiki yaani lugha inavyotumika kimuktadha.
Katika lugha ya Kiswahili kama lugha nyingine za kibantu, kuna dhana ya ngeli ambayo inayagawa majina/nomino katika makundi mbalilmbali. Kwa kweli kuna ngeli nyingi katika lugha ya Kiswahili.  Kutokana na hali hii, dhana ya ngeli  inawatatanisha wasemi wengi  sana wawe ni wasemaji wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya kwanza(hasa kwa sababu ya usanifishaji wa lugha na maneno mageni na mapya katika lugha) au Kiswahili kama lugha ya pili, na  wanafunzi wa Kiswahili kama lugha ya kigeni. Kumbukeni kwamba ikiwa msemaji anaongea lugha nyingine,lugha hiyo huenda ikaathiri jinsi anavyoitumia lugha ya pili. Kama nilivyotaja hapo juu,  sarufi ya lugha inaweza kujumuisha mpangailio wa sentensi, uundaji wa maneno, sauti zinazotumika kuunda maneno, na maana za maneno. Kwa bahati nzuri mawasiliano hayatatiziki sana kwa sababu ya kutoiweka nomino katika ngeli yake mwafaka lakini wale wanaojiita “askari wa lugha” hutatizwa sana na matumizi ya lugha yanapokiuka ngeli.
Mifano ifuatayo inaweza kusikika katika mazungumzo ya watu mbalimbali:
Je wewe kama msemaji wa Kiswahili unasema daraja hili au daraja hii; daraja hizi au madaraja haya? Na je, wingi wake utakuwa nini? Je ikiwa ni nyumba mbili, utasema nyumba nyingine ni ghali au utasema nyumba zingine ni ghali? Ni muhimu kuliwazia hili jambo kwa sababu tunasema nyumba nyingi na wala si nyumba zingi. Kwa nini  tunatatizwa sana mtu anaposema bafu hili badala ya bafu hii? Je, ni sawa basi kusema bafu hizi au mabafu haya?
Tatizo la lugha ya Kiswahili ni kwamba  ngeli za Kiswahili hazina vigezo maalum isipokuwa ngeli inayowashughulikia wanadamu na labda wanyama.  Hivi vigezo vya kimseto vinawakanganya wasemaji wengi ambao nao wana lugha zao asilia au ni wanafunzi ambao mifumo ya lugha zao za kwanza haifuati mfumo wa ngeli. Si ajabu kwamba, wakati msemaji wa Kiswahili anapojifunza lugha kama ya Kihispanyola hutatizika pia.
Haya basi, huu ni wajibu wenu kuiheshimu sarufi ya lugha ya Kiswahili lakini pia muelewe lugha hubadilika.  


Leonard Muaka
CHAUKIDU

No comments: