“Wahamiaji haramu” ni msemo haramu!?
‘Wahamiaji haramu’ sio tu kwamba ni msemo ama neno ambalo kwa sasa linatawala katika vinywa vya Watanzania bali pia baadhi ya wananchi – wasomi na wasowasomi, watawala na watawaliwa, wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wao, mabloga, n.k – wanaelekea kuona fahari kubwa kulitumia katika kuahabarisha au kutoa taarifa rasmi kama sio amri kwa umma. Na kwa bahati mbaya au nzuri, vyombo vya habari huwa ni wakala wakubwa sana wa kushamirisha maneno au misemo mipya na hata mitindo ya uzungumzaji. Kwa maoni yangu, msemo wenyewe ni ‘haramu’ tukizingatia utu wa Mwafrika ambao humtofautisha na kumpambanua na makabila mengine. Kumwita binadamu mwenzio ‘mhamiaji haramu’ kunakinzana na utamaduni wa Kitanzania wa kumthamini kila binadamu kama binadamu na ambao huko nyuma uliiletea heshima kubwa jamii ya Kitanzania – jamii ya watu waungwana na wakarimu. Uhamaji ni mchakato wa kawaida katika historia ya binadamu. Na ninaelewa kabisa kuwa msemo huu umetokana na tafsiri sisisi ya msemo wa Kiingereza “illegal immigrants” ambao unatumiwa na jamii za wazungumzaji wa Kiingereza. Tafsiri sisisi ambayo nayo inaakisi uzembe haiwezi kuhalalisha matumizi yasiyozingatia utu.
Lugha huathiriwa na mitazamo au fikira (worldview) zinazotawala katika jamii ya wazungumzaji wa lugha hiyo na vivyo hivyo lugha huweza kuathiri mitazamo na fikira za wazungumzaji. Uhusiano wa mitazamo/fikira na lugha huweza kumsaidia mgeni kujua jamii ina mtizamo gani juu ya dhana fulani. Hakuna binadamu ye yote ambaye anapenda kuhama nyumbani kwao na kwenda kuishi kwingineko bila sababu. Na leo hii kila binadamu alipo huenda mababu na mababu zake walihama kutoka mahali pengine. Utawala wa leo wa kidola unaofuata mipaka madhubuti ya nchi humtaka mtu kutoka himaya moja kwenda nyingine sharti awe na nyaraka za vibali vya kuwemo katika nchi husika. Ni kweli watu wengine wanaweza kuwa wameingia nchini bila nyaraka hizo lakini sio wahamiaji haramu bali ni wahamiaji ambao hawajasajiliwa rasmi au hawajajisajili. Lugha ya Kiswahili inatumiwa na waungwana na haina budi iakisi huo uungwana. Na lugha hubadilika kadri mitazamo ya kijamii inavyobadilika. Ndiyo, ni kweli katika Kiswahili, kwa mfano, tuliwahi kuwa na neno “mwanaharamu” (bado limo katika makamusi) lakini msomaji anayesoma kichokonozi hiki anaweza kukumbuka ni lini mara ya mwisho alisikia au kusoma neno “mwanaharamu”. “Wahamiaji haramu” ni neno haramu kijamii. Tukitendee haki Kiswahili na jamii ya wazungumzaji wake. (cbwenge@ufl.edu )
No comments:
Post a Comment