Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema
Benki Kuu ya Uswissi imesema fedha za Watanzania zilizokuwa zimewekwa katika benki za nchi hiyo zimeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 3.6 bilioni mpaka Dola 5.4 bilioni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo kwenye Mtandao wa Reuters, zilisema kuwa fedha hizo zimeongezeka hivyo kwa kipindi cha kati ya mwaka jana na mwaka huu.
“Ingawa kiasi cha fedha hizo kimetofautiana kila mwaka kwa mwongo mmoja uliopita,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya Reuters ambayo ilikuwa ikinukuu ripoti za Benki Kuu ya nchi hiyo.
Taarifa za awali kutoka kwenye kamati ya Serikali inayochunguza mabilioni hayo, ilionyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwapo kwa fedha nyingi nchini humo kuliko zile zilizotolewa na ripoti ya benki hiyo ya mwaka 2012 iliyosema kuwa kulikuwa na Dola za Marekani milioni 3.6.
Taarifa hizo zinasema mbali na fedha kuna uwezekano mkubwa wa Watanzania kuwa na nyumba na rasilimali nyingine walizowekeza nchini humo.
Januari 11, mwaka huu, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave, aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu kuwa hakuna jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka ufumbuzi wa tuhuma za watu walioficha fedha nchini humo.
Siku chache baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alizungumza na gazeti hili na kusema kuwa hawezi kumjibu chochote balozi huyo kwa kuwa ni mtu mdogo kwake.
“Najua kuwa huyu balozi ana kinga, ila siyo adabu hata kidogo kuzungumza maneno yale kwenye nchi ya watu. Kama ingekuwa ni balozi wa Tanzania huko Uswisi kasema maneno haya, angeambiwa tu arudi nyumbani kupumzika hadi watakapomhitaji,” alisema Werema.
Werema alisema kwenye Bunge lililokaa Aprili mwaka huu wangekuwa na kitu cha kuwasilisha bungeni jambo ambalo halikutimizwa.
Baada ya ukimya huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alimwandikia Katibu wa Bunge barua akitaka Serikali iwasilishe majibu juu ya uchunguzi wa fedha hizo kwenye Bunge lijalo.
Gazeti hili lilipomtafuta Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ili kujua kama amepata barua hiyo alisema kuwa “Mimi sijaipokea hiyo barua na nimetoka ofisini leo saa kumi na sikuiona, labda kama alimtuma mtu na amekaa nayo.”
Kwa upande wake Zitto alisisitiza kuwa “Hiyo barua nimeipeleka leo (jana) saa tano na kawaida tunazipeleka masijala ndiyo wampelekee, hatumpi katibu mkononi moja kwa moja.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment